Monday, November 16, 2020

MKUU WA MKOA WA TANGA ATAKA TAASISI ZA UTOAJI HAKI ZIBORESHWE ILI ZIWEZE KUTOA HAKI KWA WAKATI

 


XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Martin Shigella ataka taasisi za utoaji haki ziendelee kuboreshwa ili haki iweze kupatikana kwa wakati.

Mhe. Shigella aliyasema hayo wakati akifungua mafunzo kwa kamati za usalama za mkoa na Wilaya, kamati za maadili ya Mahakimu na Kamati za Parole mkoani Tanga ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Msaada wa Kisheria.

Mhe. Mkuu wa Mkoa aliwaambia viongozi hao kuwa wana dhamana kubwa ya kuhakikisha nchi ina utulivu, amani na usalama hivyo waitumie fursa hii ya kupata mafunzo hayo vizuri na kushirikishana na wengine.

“Tuna dhamana kubwa ya kuhakikisha utulivu, usalama na amani ya nchi tunaitimiza kwa Pamoja, tutumie fursa hii vizuri na tushirikishane” alisema Mhe. Shigella.

Aidha, Mkuu wa Mkoa amesema mamlaka za kutenda haki mkoani humo ikiwemo Mabaraza ya ardhi ya kata yamekuwa yakilalamikiwa sana kutokana na ufanisi wake ambao unasababishwa na watumishi wachache waliopo ambayo inasababisha ucheleweshwaji wa majukumu yao ikiwemo kupatikana kwa nakala za hukumu.

Aliongeza, Mkoani Tanga chama cha wanasheria kimeendelea kutoa msaada mkubwa sana wa kisheria kwa wananchi lakini bado hautoshelezi kwani matatizo ya kisheria ni mengi hivyo awaomba waendelee kujitangaza ili wananchi waweze kuwafahamu na kwenda kupata msaada wa kisheria. Pia aliahidi ofisi za Wakuu wa Wilaya na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa zipo tayari kusaidia gharama ndogondogo ambazo zitahitajika kuendesha kesi za wananchi zinapoenda mahakamani.

“Msaada mnaotoa ni ibada na sehemu ya sadaka kwani unagusa Maisha ya watu wengi tena wengine kutoka mbali na mlipo hivyo mjitahidi kuwasikiliza na kuwasaidia” alisema Mhe.Shigella.

Aidha, Mkuu wa Mkoa alisema mafunzo haya yanayohusisha viongozi wengi wakiwemo mahakimu yamekuja wakati muafaka na wakati serikali ya awamu ya tano muhula wa pili unapoanza hivyo ana imani yatawasaidia katika kutekeleza majukumu yao.

 


Sunday, November 15, 2020

WAJUMBE WA MABARAZA YA ARDHI ACHENI KUPOKEA RUSHWA – MHE. NGUVIRA

 


XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

 

Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga Mhe. Toba Nguvira awaasa wajumbe wa mabaraza ya ardhi wilayani humo kuacha tabia ya kupokea rushwa na kunyima haki wananchi.

Mhe. Nguvira aliyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya utawala bora, Wosia na Mirathi kwa watendaji kata na wenyeviti wa mabaraza ya ardhi wilayani humu ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Msaada wa Kisheria ambayo kitaifa yalizinduliwa tarehe 12 Mkoani Tanga.

Mkuu wa wilaya huyo aliwaambia watendaji kata na wenyeviti wa mabaraza ya kata hao wayatumie mafunzo hayo vizuri ili kumaliza migogoro mingi iliyopo ambayo inaanzia kwenye kata na inasababishwa na rushwa na hivyo kunyima haki baadhi ya wananchi.

“Migogoro ya ardhi na mirathi ni mingi sana nchini na inasababishwa na rushwa” alisema Mkuu wa wilaya huyo.

Aidha Mhe. Nguvira alisema sheria zimewekwa kuhakikisha haki inatendeke kwani kukosekana kwa haki kunapelekea machafuko katika jamii.

Mhe. Nguvira aliwasisitiza wajumbe wa mafunzo hayo kuyatendea haki kwa kuyatumia mafunzo watakayopata kuyatafsiri katika mabaraza ya kata.

Aimshukuru Mkuu wa Wilaya kwa nasaha zake kabla ya kuanza kw mafunzo mwezeshaji wa mafunzo hayo amabye pia ni Naibu Katibu kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Bw. Calist Luanda alisema amepewa jukumu la kiutoa mafunzo kwa wajumbe hao hivyo awasisitiza wajumbe kuyafanyia kazi mafunzo watakayopewa ili waweze kuboresha kazi zao na kutoia haki kwa wananchi.


WATANZANIA TUWE NA UTAMADUNI WA KUANDIKA WOSIA KUEPUKA CHANGAMOTO ZA MIRATHI- JAJI MRUMA

 
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX


Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Tanga Mhe. Jaji Amir Mruma amesema watanzania tuwe na utamaduni wa kuandika wosia kwani suala la usimamizi wa mirathi huwa linakuwa rahisi sana pale kunapokuwa na wosia wa marehemu kuhusu mgawanyo wa mali zake pindi atakapoondoka duniani.

“Mara nyingi wosia umekuwa ukirahisisha na kuondoa migogoro ya umiliki wa mali za marehemu na pia umekuwa ukibainisha nani atasimamia mali hizo kwa maendeleo ya familia husika” alisema Jaji Mruma.

Jaji Mruma ameyasema hayo wakati akizindua rasmi Maadhimisho ya Wiki ya Msaada wa Kisheria yanayofanyika kitaifa Mkoani Tanga kuanzia tarehe 12 hadi 18 Novemba, 2020 yakilenga kupunguza changamoto za kisheria kwa wananchi.

Mhe. Jaji Mruma alisema kwa utafiti walioufanya baada ya kukaa muda mrefu mahakamani wamegundua changamoto kubwa zaidi ya mirathi katika jamii inasababishwa na familia nyingi kutoandika wosia mapema kabla ya kufariki.

Aliongeza kuwa usimamaizi bora wa mirathi ni ule ambao unalenga kuleta manufaa na maendeleo kwa walengwa wa mali zilizoachwa na marehemu na si kumnufaisha msimamizi ambaye si mke au mume au mtoto wa marehemu.

Alisema “Wajane na watoto yatima wamekuwa wahanga wakubwa na wamedumbukia kwenye dimbwi la umasikini kutokana na baadhi ya wasimamizi au watu wasiohusika katika usimamiaji kujinufaisha na mali hizo jambo ambalo linaleta umasikini kwa baadhi ya familia”

Alisisitiza “usimamizi bora wa mirathi una muda mahsusi wa kuifunga mirathi husika na unabainisha mali itagawanywa au kuuzwa na warithi kugawana mali husika ili waweze kujiendeleza nayo”

Vilevile, Jaji Mruma alitoa rai kwa watoa elimu waliopangwa kuhudumia wananchi katika maadhimisho hayo wajue kuwa eneo hilo ni muhimu na linagusa wananchi wengi hivyo wanapaswa kutoa elimu na ushauri ipasavyo.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Ndg. Amon Mpanju alisema Wizara hiyo inalengo la kutatua kero za wananchi hususan za kisheria ili kupunguza mashauri kwenye mfumo wa upatikanaji haki, hivyo Wizara ya Katiba na Sheria inahakikisha elimu inawafikia wanachi popote walipo ili kujua haki zao na namna gani wanaweza kuzifikia.

Aidha, Msajili wa Watoa Huduma za Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Bi . Felistas Joseph alisema Wizara na wadau wake wameamua kubadili mtindo wa kutoa huduma ya msaada wa kisheria kwa kuangalia upande mmoja wa wananchi peke yake na badala yake  kujenga uwezo wa upande wa pili ili wahitaji na watoaji wote wawe na uelewa wa masuala ya kisheria lakini pia uwezo wa kutatua kero hizo.

Bi. Felistas alisema “ katika mafunzo haya kutakuwa na makundi mbalimbali kuanzia ngazi ya kata, wilaya na Mkoa ambapo mada mbalimbali zitatolewa na wataalamu kutoka Wizara mbalimbali, Chama cha Wanasheria Tanganyika na Mashirika yanayotoa msaada wa kisheria”.

Aliongeza kuwa mafunzo hayo yanayofanyika Mikoa yote Tanzania Bara yanaenda sambamba na utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria katika mikoa hiyo.

Maadhimisho haya yanaratibiwa na kusimamiwa na Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria kwa mara ya nne tangu kupewa mamlaka hayo chini ya sheria ya Msaada wa Kisheria ya mwaka 2017.

 

 

 


Monday, October 26, 2020

MAANDALIZI YA WIKI YA MSAADA WA KISHERIA YAANZA JIJINI TANGA


 


Kikao kazi cha maandalizi ya Wiki ya Msaada wa Kisheria chafanyika jijini Tanga na kufunguliwa na Katibu Tawala wa Mkoa Bi. Judica Omary.

Wednesday, October 21, 2020

WIZARA YA KATIBA KUSHIRIKIANA NA UNDP KUJENGA UELEWA KWA WANANCHI JUU YA UTAJIRI WA ASILI NA RASILIMALI ASILIA


 Kikao kati ya Menejimenti ya Wizara ya Katiba na Sheria na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) cha kujenga uelewa wa jukumu la Wizara kuhusiana na Uangalizi na Usimamizi waUtajiri wa Asili na Rasilimali za nchi chafanyika Wizarani hapo Mtumba, jijini Dodoma.


Wataalam kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) wakifuatilia majadiliano wakati wa kikao chao na Menejimenti ya Wizara ya Katiba na Sheria.


Mkurugenzi wa kitengo cha Uangalizi wa Utajiri wa Asili na Rasilimali Asilia cha Wizara ya Katiba na Sheria  Bi Neema Mwanga akielezea jambo wakati wa kikao kati ya  Menejimenti ya Wizara ya Katiba na Sheria na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).


Bi. Getrude kutoka kitengo cha mazingira UNDP akichangia mada.Mkurugenzi Idara ya Huduma za Kisheria kwa Umma Bw. Griffin Mwakapeje akichangia mada.


Bw. Godfrey Mulisa kutoka UNDP akichangia mada.


Picha ya pamoja ya Menejimenti ya Wizara ya Katiba na Sheria na wataalam kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) baada ya kumaliza kikao chao.


XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria yakubaliana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kujenga uelewa kwa wananchi juu ya kulinda Utajiri wa Asili na Rasilimali Asilia za nchi.

Makubaliano hayo yamefikiwa katika kikao kati ya Menejimenti ya Wizara ya Katiba na Sheria na Maafisa kutoka UNDP kilichofanyika wizarani hapo Mtumba, jijini Dodoma.

Katika kikao hicho UNDP waliahidi kuandaa andiko ambalo ndilo litakalokuwa muongozo wa namna ya kutoa elimu kwa wananchi waweze kulewa dhana nzima ya utajiri wa asili na rasilimali asilia na namna ambavyo zinaweza kuwaletea maendeleo kwa wao binafsi na nchi pia.

Bw. Godfrey Mulisa ambaye ni mtaalam kutoka UNDP alisema Shirika lao litasaidia kuangalia ni namna gani watashirikiana kuongeza usimamizi wa utajiri wa asili na rasilimali asilia na kuhakikisha faida inapatikana kwa watanzania.

“Kubwa la kuangalia ni kuongeza usimamizi na kuhakikisha faida inapatikana kwa watanzania” alisema Bw. Godfrey

Naye Bi. Getrude kutoka kitengo cha mazingira kwenye shirika hilo alisema UNDP itashirikiana na kitengo cha Uangalizi wa Utajiri wa Asili na Rasilimali Asilia kilichopo wizarani hapo ili kukijengea uwezo kitengo hicho kiweze kufuatilia rasilimali na utajiri uliopo Tanzania ili kuweza kuinua uchumi wa nchi na wananchi kwani shirika hilo linaangalia sana maendeleo ya watu.

Awali akielezea kuhusu jukumu ililonalo Wizara ya Katiba na Sheria la kusimamia utajiri wa asili na rasilimali asilia Mkurugenzi wa Kitengo cha Uangalizi wa Utajiri wa Asili na Rasilimali Asilia Bi. Neema Mwanga alisema jukumu kubwa lililonalo ni kuangalia mifumo au mikataba iliyopo inahakikisha inalinda rasilimali za Taifa.

Aliongeza kuwa kitengo hicho kilianzishwa mwaka 2018 ili kuratibu na kuangalia maendeleo endelevu ya uvunaji na matumizi ya utajiri wa asili na rasilimali, pia kusajili na kuangalia mikataba inayohusu rasilimali asilia, na kupitia sheria, sera na miongozo ili zisiathiri matakwa ya Katiba.

Aidha, Mkurugenzi huyo alisisitiza Katiba inahitaji wananchi walinde rasilimali hivyo ni vyema wakapata elimu ya namna ya kulinda kwani uelewa mdogo wa jamii kuhusu sheria ni kikwazo katika kulinda rasilimali asilia.

Thursday, September 24, 2020

MAZUNGUMZO YA AMANI YATAJWA KUWA NJIA BORA NA SALAMA YA UTATUZI WA MIGOGORO NCHINI.
 
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Mazungumzo ya amani ni muarobaini uliothibitika kutumika kama tiba ya migogoro ya ardhi Mvomero Mkoani Morogoro.

 

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mhe. Albinus Mgonya wakati akitoa taarifa ya hali ya amani wilayani humo kwa Kamati ya Kitaifa ya Ujenzi wa Amani na Kuzuia Mauaji ya Kimbari iliyofika walayani kwake hivi karibuni.

 

Wakulima na wafugaji ni watanzania wanaoishi pamoja na kushirikiana katika shughuli mbalimbali za kijamii, kisiasa na kiuchumi katika maeneo wanaoishi na zaidi, wengi wao ni wakulima na ni wafugaji kwa wakati mmoja hivyo njia ya mazungumzo ya amani imejipambanua kuwa tiba ya utatuzi wa migogoro inayowakabili.

 

"Unajua, hawa wakulima na wafugaji wanafahamiana kwasababu wanaishi pamoja, matumizi ya nguvu hususani vyombo vya ulinzi na usalama isingekuwa muarobaini, badala yake kwa kuwakutanisha na kuzungumza nao kumeonesha kuwa ni suluhisho la migogoro na ujenzi wa amani na utulivu baina yao."

 

Kwa niaba ya wakulima na wafugaji ndugu Moringe Kwinasei ameungana na Mkuu huyo wa Wilaya kwa kuthibitisha hali ya uwepo wa utulivu na amani uliotokana na utatuzi wa migogoro kwa njia ya mazungumzo ya amani na kuwataka wakulima na wafugaji kuacha tabia ya uchochezi kwa kisingizio cha migogoro baina yao.

 

"Unajua sisi ni ndugu na wote tunahitajiana katika mambo mengi ikiwemo mazao ya mifugo na mimea ambayo ndiyo yanatugombanisha, tunagombana shambani baadae tunakaa hotelini tunakula wali-nyama! sasa kwanini tuendelee kugombania mambo ambayo ni sehemu ya mahitaji yetu muhimu? Ameongeza kwa kuuliza Martine Matingise.

 

Aidha, Mhe. Mgonya amesema Wilaya yake imeanzisha programu ya michezo mbalimbali hasa mashindano ya mipira wa Miguu kati ya Wakulima na wafugaji,  mbinu hii imeonesha kuwa na tija katika ujenzi wa amani katika Wilaya hiyo kwasababu michezo imewaleta wakulima na wafugaji pamoja na kuishi kwa upendo.

 

"Nimeanzisha na kuhamisisha michezo mbalimbali hasa mpira wa Miguu kati ya wakulima na wafugaji, na nimekuwa nikishiriki nao katika michezo husika. Kwakweli njia hii pia imeonesha mafanikio makubwa katika jitihada za Serikali katika ujenzi wa amani na kuzuia migogoro katika jamii." Amemaliza Mhe. Mgonya.

 

Kamati hii imehitimisha ziara yake ya utekelezaji wa majukumu muhimu ya Ujenzi wa Amani na Kuzuia Mauaji ya Kimbari katika Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro baada ya kufanya kazi kama hiyo katika Mikoa ya Arusha, Manyara na Rukwa.