DPP afuta Kesi 59 zaidi jijini Mbeya
Waziri wa Katiba na Sheria Mh. Balozi Dkt Augustine Mahiga
(Mb) katikati akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Mh.
Chalya J. Nyangidu (wa pili kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Mashitaka Biswalo
Mganga (wa pili kulia), walipotembelea Ofisi ya Mkuu huyo wa Wilaya leo tarehe 28
Nov. 2019 wakati wa ziara ya kikazi wilayani humo.
Waziri wa Katiba na Sheria Mh. Balozi Dkt Augustine Mahiga (Mb) akisalimiana na afisa wa magereza wakati wa ziara ya kikazi katika gereza la Tukuyu Wilaya ya Rungwe Jijini Mbeya. Kushoto ni Mkuu wa Gereza la Tukuyu ASP. Samwel J. Kaluwa akiwatambulisha Staff wa gereza hilo mbele ya Waziri.
Waziri wa Katiba na Sheria Mh. Balozi Dkt Augustine Mahiga
(Mb) kulia akiwa na mwenyeji wake Kamishna Msaidizi wa Magereza Mkoa wa Mbeya
Mathias Mkama (ACP) katikati,
alipotembelea Gereza Kuu la Ruanda Mbeya 27 Nov. 2019. Kushoto ni Kamishna
Msaidizi wa Magereza na Mkuu wa Gereza
la Ruanda Mbeya Vendeline Tesha wakati wa ziara ya kikazi jijini humo.
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Katika mwendelezo wa ziara ya
kikazi ya Waziri wa Katiba na Sheria Mh. Balozi Dkt Augustine Mahiga (Mb) kwenye
Mikoa ya kusini, Mkurugenzi Mkuu wa Mashitaka Tanzania (DPP) Biswalo Mganga
amefuta jumla ya kesi 59 katika mahakama za Mkoa wa Mbeya.
Mkurugenzi Biswalo ameyafanya
hayo katika gereza la Ruanda mjini Mbeya na gereza la Tukuyu Wilaya ya Rungwe
alipoambatana na Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Mahiga ili kujionea hali
halisi ya mazingira ya utoaji haki jinai katika magereza hayo na taasisi
mbalimbali za haki jinai ikiwemo Ofisi ya Taifa ya Mashitaka, Polisi, Mahakama
na Magereza yenyewe.
“Niliowafutia Kesi nendeni mkawe
raia wema, msirudie makosa, badala yake mkawe mabalozi wema mtakaofanya kazi
kwa bidii ili kumuunga mkono Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli
katika kauli yake ya hapa kazi tu.”
Kwa upande wake Waziri mwenye
dhamana ya Katiba na Sheria Balozi Dkt Augustine Mahiga (Mb) aliwataka wote
waliofutiwa mashitaka kwenda kufurahi na familia zao huku wakimshukuru Mungu na
kujutia makosa yaliyosababisha kushitakiwa kwao. Aidha, aliwaonya kutokurudia
makosa hayo badala yake watumie nguvu na akili walizonazo kuzalisha mali kwa
maendeleo yao na familia zao pamoja na kukuza uchumi wa Taifa.
“Mliosamehewa leo nendeni
mkafurahi na familia zenu sambamba na kuwa watu wema katika jamii
inayowazunguka kwani ni matumaini yangu kuwa mmejifunza mengi na mmebadilika.
Kuna watu hapa nikiwatizama misuli yao, walipaswa wakaitumie kufanya kazi na
kuzalisha mali kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla badala ya kuitumia kufanya
uhalifu.”
Kwa mujibu wa kifungu cha 91(1)
cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, sura ya 20 kama ilivyofanyiwa
marejeo 2002, Mkurugenzi Mkuu wa Mashitaka anayo mamlaka ya kuwafutia mashitaka
watuhumiwa wa makosa ya jinai katika magereza mbalimbali nchini. Mpaka sasa
katika ziara hii ya kikazi ya Waziri wa Katiba na Sheria katika Mikoa mitatu DPP
Biswalo ameshafuta jumla ya kesi 120 na
bado ziara inaendelea katika Wilaya ya Kyela na baadae Mkoa wa Njombe.
Comments
Post a Comment