RAIA WA ETHIOPIA WALIOMALIZA VIFUNGO WARUDI NCHINI KWAO – WAZIRI MAHIGA
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.
Balozi Dkt. Augustine Mahiga Ataka raia wa Ethiopia waliomaliza vifungo vyao
warudishwe nchini kwao.
Waziri Mahiga ameyasema hayo
katika ziara yake ya kikazi ya siku saba katika Mikoa ya Iringa, Njombe na
Mbeya ambapo anatembelea magereza ili kuona Haki Jinai inavyotekelezwa katika
mikoa hiyo.
“Hakuna sababu kwa nini raia hawa
waendelee kutumia gharama kubwa ya Serikali yetu wakati wameshamaliza vifungo
vyao, naahidi kuwa tutatumia kila njia kuhakikisha Serikali inatua mzigo huu”,
alisema Balozi Mahiga.
Akiwa ameambatana na Mkurugenzi
wa Mashtaka nchini Ndg. Biswalo Mganga, Waziri Mahiga alianza ziara yake kwa
kutembelea gereza la Wilaya ya Iringa mjini na kujionea namna Haki Jinai
inavyotekelezwa katika gereza hilo.
Waziri Mahiga alizipongeza
taasisi za Haki Jinai Mkoani humo kwa kuendelea kushirikiana katika kuhakikisha
haki jinai inatekelezwa ipasavyo na kuepuka vitendo vya rushwa, unyanyasaji na
ubambikizaji wa kesi kwa watuhumiwa.
Naye Mkurugenzi wa Mashtaka nchini
Ndg. Biswalo Mganga katika ziara hiyo ametumia mamlaka yake kisheria kufuta
kesi 45 ambazo ziko mahakama za mwanzo na Wilaya na ameahidi kuendelea kufanya
hivyo kwa kesi nyingine. Mkurugenzi Mganga alifikia uamuzi wa kufuta kesi hizo baada
ya kupitia mafaili na kujiridhisha kuwa hakuna haja ya kuendelea na kesi hizo
lengo ikiwa ni kuhakikisha haki inapatikana kwa wakati.
Comments
Post a Comment