Monday, December 16, 2019

NAIBU KATIBU MKUU MPANJU ATOA WITO KWA VIONGOZI WA DINI KUHAMASISHA WANANCHI KUSAJILI WATOTO ILI KUPATIWA VYETI VYA KUZALIWA


xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Ndg. Amon Mpanju awaomba viongozi wa dini na kuwataka watendaji wa Serikali kuhamasisha waumini na wananchi waliopo maeneo yao kupeleka watoto kusajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa.

Mpanju ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa mpango wa usajili wa watoto wa umri chini ya miaka mitano katika mikoa ya Morogoro na Pwani uliofanyika wiki hii katika viwanja vya uwanja wa ndege Mkoani Morogoro.

“Nitoe wito kwa viongozi wa dini zetu popote walipo kwenye mikoa ya Morogoro na Pwani, viongozi wa kijamii, wenyeviti wetu wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji waliochaguliwa hivi karibuni na watendaji kwa ngazi zote kuhakikisha mnahamasisha wananchi wetu kwenye mikoa hii wajitokeze katika kampeni inayoendelea kuwasajili watoto na kupatiwa cheti bure”alisema.

Aidha ndg Mpanju aliwaeleza viongozi hao kwamba zoezi hilo linagusa mtoto aliyezaliwa mwishoni mwa mwaka 2014 mpaka wanaozaliwa sasahivi hivyo, wawahamasishe wazazi na walezi wajitokeze kusajili watoto na kupata vyeti bure.

 Mpanju alisisitiza “Kwa hiyo nitoe rai kwa viongozi wa dini na watendaji wa Serikali kote nchini ambako kampeni hii inaendelea tutumie mimbali za makanisa, misikiti na majukwaa yetu ya kisiasa na kwenye maeneo ya kazi tuhakikishe habaki mtoto mwenye sifa bila kusajiliwa na kupata cheti”

Zoezi hili la uandikishaji linaloendelea katika mikoa 15 ya Tanzania Bara linatarajiwa kuifikia mikoa mingine yote iliyobaki ndani ya kipindi cha miaka mitatu kuanzia sasa.

Friday, December 13, 2019

MKUTANO WA WATAALAM WA SHERIA WA NCHI ZA SADC WAMALIZIKA

Mwenyekiti wa mkutano wa wataalam wa sheria wa nchi za SADC ambaye pia ni Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Prof Sifuni Mchome (wa tatu kushoto) katika picha ya pamoja na wajumbe baada ya kumalizika kwa mkutano huo.

USAJILI WA VIZAZI NA VIFO NI TAKWA LA KISHERIA

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akizindua zoezi la uandikishaji wa watoto wa umri chini ya miaka mitano na ugawaji wa vyeti kwa watoto hao katika mikoa ya Morogoro na Pwani uliofanyika katika viwanja vya uwanja wa Ndege Mkoa wa Morogoro.

 Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akionesha cheti cha kuzaliwa kwa wananchi waliofika kwenye uzinduzi wa uandikishaji wa watoto wa umri chini ya miaka mitano na ugawaji wa vyeti kwa watoto hao katika mikoa ya Morogoro na Pwani.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Ndg. Amon Mpanju akiongea na wananchi kwenye uzinduzi wa uandikishaji wa watoto wa umri chini ya miaka mitano na ugawaji wa vyeti kwa watoto hao katika mikoa ya Morogoro na Pwani.

 Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akiangalia cheti cha kuzaliwa mtoto baada ya kuandikishwa  kwenye uzinduzi wa uandikishaji wa watoto wa umri chini ya miaka mitano na ugawaji wa vyeti kwa watoto hao katika mikoa ya Morogoro na Pwani.

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu RITA Bi. Emmy Hudson akiongea na wananchi kwenye uzinduzi wa uandikishaji wa watoto wa umri chini ya miaka mitano na ugawaji wa vyeti kwa watoto hao katika mikoa ya Morogoro na Pwani.


Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (kushoto) akisalimiana na Mwenyekiti wa Bodi ya RITA Prof. Hamisi Dihenga wakati wa uzinduzi wa uandikishaji wa watoto wa umri chini ya miaka mitano na ugawaji wa vyeti kwa watoto hao katika mikoa ya Morogoro na Pwani.


xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Usajili wa Vizazi na vifo ni jambo la lazima kwa wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani limetamkwa kwenye sheria ya uandikishaji vizazi na vifo, (sura 108 toleo la 2002), hivyo, wananchi wote wanapaswa kuwa waelimishaji na wahamasishaji ili vizazi na vifo viandikishwe kwa maendeleo endelevu ya Taifa la Tanzania kuelekea uchumi wa kati na uchumi wa viwanda.

Haya yamesemwa na Waziri wa Katiba na Sheria Mheshimiwa Balozi Dkt. Augustine Mahiga wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Mpango wa Usajili wa Watoto wa Umri Chini ya Miaka Mitano ulioambatana na utaoji wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto hao katika Mikoa ya Morogoro na Pwani uliofanyika katika viwanja vya uwanja wa Ndege Mkoa wa Morogoro katikati ya wiki hii.

Balozi Mahiga ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo alisema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali zenye lengo la kuboresha mfumo wa uandikishaji wa vizazi, ndoa, talaka na vifo kwa kuzingatia umri wa makundi mbalimbali kupitia mkakati wa kitaifa wa usajili wa matukio muhimu ya binadamu na kuyapa nguvu ya kisheria kupitia Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) ambayo ipo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria.

“Vilevile katika kuhakikisha kwamba maboresho haya yanapata nguvu ya kisheria, mnamo mwezi Septemba 2019, Bunge lilipitisha Sheria mpya ya usajili wa Vizazi na Vifo ambayo tayari Imeshasainiwa na Mheshimiwa Rais na sasa tunaendelea kuandaa kanuni za utekelezaji wa Sheria hiyo”. Alisema Dkt. Mahiga.

Kwa upande wake Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu wa RITA Bi Emmy Hudson wakati akitoa hotuba yake mbele ya mgeni rasmi alisema kuwa licha ya zoezi la uandikishaji vizazi na vifo kuwa na umri usiopungua miaka 100  bado mwitikio na wanachi kuandikisha vizazi na vifo ni hafifu sana hivyo kurudisha nyuma mipango ya maendeleo nchini.

“kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 wananchi waliokuwa wamezaliwa Tanzania Bara na kustahili kupatiwa vyeti walikuwa 13.4%. Upo uwezekano wa hali kuwa mbaya zaidi kutokana na kutokuwa na uwiano sawia kati ya idadi ya ongezeko la idadi ya watu na kiwango cha usajili kwani kila siku tukio la kufa na kuzaliwa linatokea hivyo tusipoweka nguvu ya kusajili vizazi na vifo tutajikuta katika hatari ya kuwa na idadi ndogo ya watu waliosajiliwa hali itakayodhoofisha mipango ya maendeleo nchini”.

Nae Naibu Katibu MKuu wa Wizara ya Katiba na Sheria ndugu Amon Mpanju aliposimama kutoa salamu za Wizara aliipongeza RITA chini ya uongozi Madhubuti wa Mwenyekiti wa Bodi Prof. Hamisi Dihenga na Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu wa RITA Bi Emmy Hudson kwa kutekeleza kikamilifu Mpango Mkakati wa Usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu kama yalivyotamkwa katika kutambua sheria ya RITA ya usajili ya 2002 pamoja na kutekeleza maelekezo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya kutambua watu wake (watanzania) popote walipo ili waweze kufikiwa na huduma za kijamii. 

“Kinachofanyika leo ni ushahidi dhahili wa utekelezaji wa mpango huo na pia kutekeleza maelekezo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya kutambua watu wake (watanzania) popote walipo ili waweze kufikiwa na huduma za kijamii”.

Mpanju alimalizia kwa kuupongeza uongozi wa mikoa ya Morogoro na Pwani na watendaji walioenea katika wilaya za mikoa hiyo miwili kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kuandikisha watoto zaidi ya elfu 95 ndani ya muda mfupi.

 “Nipongeze uongozi wa mikoa ya Morogoro na Pwani kwa namna walivyoanza zoezi hili kwa kishindo, zoezi hili limeanza mnamo tarehe sita mwezi huu, leo ni takribani siku ya tano lakini usajili wa watoto ambao wameshasajiliwa na kupewa vyeti ni zaidi ya elfu 95. Hii inaonesha ni namna gani wamejitoa kwa kazi hii na pongezi nyingi ziwafikie watendaji wetu ambao mmeenea katika wilaya zetu zote za mikoa hii miwili kuhakikisha zoezi linafana, endeleeni hivyo kwani mnachokifanya ni kuisaidia serikali yenu katika kuwafikia wanyonge katika kupata huduma za kijamii”

Waziri Mahiga alihitimisha hotuba yake kwa kuwapongeza RITA na wadau wengine wa maendeleo kama UNICEF, Canada na Kampuni ya Mtandao wa Simu za Mkononi, TIGO kwa kuwezesha watoto wa kitanzania zaidi ya milioni 3.6 kupata vyeti vyao vya kuzaliwa ndani ya miaka 13 ambayo mpango huu unatekelezwa na kuagiza kwamba jitihada ziendelee na nguvu kubwa iwekezwe ili idadi ya uandikishaji wa watoto wenye umri chini ya miaka mitano uongezeke zaidi na ataendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa zoezi hilo.

“Naomba nichukue nafasi hii kuwapongeza tena RITA na wadau wengine wote kwa kuwezesha watoto wa kitanzania zaidi ya milioni 3.6 kupata vyeti vyao vya kuzaliwa katika miaka 13 ambayo mpango huu unatekelezwa na ninaamini katika kipindi cha kampeni tukiweza kusajili 90% ya watoto katika mikoa ya Morogoro na Pwani kama tulivyo azimia, idadi basi itaweza kufikia milioni nne (4) na nitaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa zoezi hili, naamini hamtaniangusha”. Alihitimisha Balozi Mahiga.

Takwimu zinaonesha kwamba idadi ya watoto waliozaliwa bila kusajiliwa na wengi wao wakiwa ni watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano inaongezeka kwa haraka sana na hivyo Wakala ya Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma (PO – PSM) pamoja na wadau wengine wa maendeleo wanatekeleza mfumo wa Usajili wa vizazi na vifo uliyoboreshwa (BRS) ambao hutumia teknolojia mpya ya habari na mawasiliano (TEHAMA) ili kusajili watoto wengi nchini Tanzania katika miaka mitano ijayo.

Thursday, December 12, 2019

WATUMISHI WA UMMA WATAKIWA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAO KWA KUZINGATIA WELEDI WA TAALUMA ZAOWaziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika akifungua Kongamano la Kuadhimisha Siku ya Maadili na Haki za Binadamu, katika ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (katikati mstari wa mbele) na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa  (wa tatu kutoka kulia mstari wa mbele), Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Mhe. Jaji Mathew Mwaimu (wa pili kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na Viongozi mbalimbali wa Taasisi za Umma, baada ya ufunguzi wa Kongamano la Kuadhimisha Siku ya Maadili na Haki za Binadamu katika ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa jijini Dodoma.


Baadhi ya viongozi wa Taasisi mbalimbali za Umma wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika  wakati akifungua Kongamano la Kuadhimisha Siku ya Maadili na Haki za Binadamu, katika ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa jijini Dodoma


XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX


Watumishi wa Umma wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia weledi wa taaluma zao.
kauli hiyo imetolewa   na Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kepteni Mstaafu George Mkuchika wakati akifungua maadhimisho ya siku ya maadili na haki za bianadamu kitaifa jijini Dodoma ambapo amewataka watumishi wa Umma kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maadili.
“Tunaona Maadili ndio neno la Msingi Miongoni mwa jitihada za serikali ni kutunga sheria na kanuni mbalimbali zinazozingatia Maadili na Kanuni za utumishi wa umma, hivyo niwaase watumishi wa umma kuzingatia katika kufuata na kusimamia sheria  na Miongozo ya utumishi kwa lengo la kuboresha utawala bora” amesema.
Aidha, Waziri Mkuchika amesema suala la mfumo wa Mtandao limekuwa na mchango mkubwa katika kuhakiki watumishi feki pamoja na uadilifu wa matumizi ya fedha za umma.
Awali  akizungumza katika maadhimisho hayo, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora  Mhe. Mary Mwanjelwa amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imejikita katika masuala ya uadilifu na uzalendo hivyo kila mmoja anapaswa kuepuke kufanya mambo yasiyofaa katika taifa.
Sisi tunatakiwa kuwa mfano bora katika kusimamia uadilifu na utawala bora hivyo niwaase watumishi wa umma kuwa jambo la uadilifu ni jambo la muhimu sana”
Kwa upande wake Kamishina wa Sekretarieti ya Maadili ya viongozi wa Umma Jaji Mstaafu Harold Nsekela ameelezea chimbuko la siku hiyo kuwa ni siku ya kimataifa ya kuzuia na kupambana na Rushwa ambayo huadhimishwa Desemba 09 ya kila mwaka
Tangu mwaka 2017 maadhimisho ya siku ya maadili na haki za bianadamu kitaifa yamekuwa yakifanyika Jijini Dodoma kufuatia maamuzi ya Serikali kuhamishia makao makuu jijini hapa na kauli mbiu kwa mwaka huu ni “Maadili katika Utumishi wa Umma ni Nguzo Muhimu katika Kuimarisha Utawala Bora na Haki za Binadamu”

KATIBU MKUU WIZARA YA KATIBA NA SHERIA AONGOZA MKUTANO WA WATAALAM WA SHERIA WA NCHI ZA SADC

Mwenyekiti wa mkutano wa wataalam wa Sheria wa nchi za SADC ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome (kulia) akiongea na wataalam hao (hawapo pichani). Tanzania ni Mwenyekiti wa mkutano huo hivyo kumwezesha Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria kuwa Mwenyekiti wa mkutano huo.

Mwenyekiti wa mkutano wa wataalam wa Sheria wa nchi za SADC ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome (wa pili kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa mkutano huo.

Friday, December 6, 2019

SIKU YA MAADILI NA HAKI ZA BINADAMU KUADHIMISHWA KITAIFA DESEMBA 11 MWAKA HUU.

Waziri wa Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Mkuchika akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuwafahamisha kuhusu maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu yanayotarajiwa kufanyika Desemba 11, Jijini Dodoma. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Amon Mpanju na Kulia ni Kamishna wa Maadili na Viongozi wa Umma Mhe. Jaji mstaafu Harold Nsekela.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Amon Mpanju akiongea waandishi wa habari (hawapo pichani) kuwafahamisha kuhusu maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu yanayotarajiwa kufanyika Desemba 11 Jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora  Mhe. Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu akiongea waandishi wa habari (hawapo pichani) kuwafahamisha kuhusu maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu.

Viongozi mbalimbali wakimsikiliza Waziri wa Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Mkuchika wakati akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuwafahamisha kuhusu maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu yanayotarajiwa kufanyika Desemba 11, Jijini Dodoma.

Sehemu ya waandishi wa habari waliohudhuria kikao na viongozi mbalimbali kufahamishwa kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Desemba 11, 2019.

xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
WAZIRI MKUCHIKA ATAKA WANANCHI WATEKELEZE WAJIBU WAO ILI KUPATA HAKI ZAO

Wananchi wametakiwa kufahamu wajibu wao katika kila eneo pale wanapodai haki zao ili kuwezesha haki hizo kupatikana kwa wakati.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Uawala Bora Mhe. George Mkuchika wakati akiongea na waandishi wa habari na kuufahamisha Umma kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu yanayotarajiwa kufanyika Disemba 11, 2019 Jijini Dodoma.

“Wanahabari, matarajio yangu ni kwamba katika kuuhabarisha Umma, mtachambua haya ilimkila upande na hasa mwananchi ambaye pamoja na kudai haki zake, afahamu pia wajibu wake katika kila eneo” alisema.

Aliongeza ““Uadilifu unaanzia ngazi ya familia ndipo Serikali itapata watumishi waadilifu wanaozingatia misingi na kanuni za utumishi wa Umma”.

Waziri Mkuchika amesema tunapoadhimisha Siku ya Maadili na Haki za Binadamu nchi inajitathmini namna inavyozingatia maadili, kudhibiti rushwa na kufuata taratibu katika manunuzi na nidhamu za watumishi zinavyosimamiwa.

Aidha, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Amon Mpanju alisema sheria za Utekelezwaji wa Maadili na Haki za Binadamu zipo na zinafuatwa ipasavyo hivyo hali ya upatikanaji wa haki za binadamu kwa sasa unaendelea vizuri.

Naye, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Mhe. Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu alisema Hali ya utekelezwaji wa Haki za Binadamu nchini uko vizuri kwa sasa kwani haki hizo zimekuwa zikitekelezwa kikamilifu katika sehemu mbalimbali ikiwemo Afya, Elimu na Miundombinu.

Kauli Mbiu kwa mwaka huu ni “Utumishi wa Umma ni Nguzo Muhimu katika Kuimarisha Utawala Bora na Haki za Binadamu”

Kongamano la kuhitimisha Maadhimisho hayo linatarajiwa kufanyika Disemba 11 ma litahusisha watumishi waandamizi wa Serrikali wakiwemo Makatibu Wakuu, Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Serikali.Thursday, December 5, 2019

WAZIRI MAHIGA ASHUHUDIA UANDIKISHAJI VIZAZI, VIFO NA WATOTO CHINI YA MIAKA MITANO MKOANI IRINGA

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akimkabidhi mzazi cheti cha kuzaliwa mtoto baada ya kuandikishwa.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akionesha cheti cha kuzaliwa kilichoandikishwa.
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) Bi Emmy Hudson (kushoto) akiwa na Mkurugenzi wa Huduma za Sheria Bi. Lina Msanga katika zoezi la uandikishaji wa vizazi na vifo Mkoani Iringa.

Wednesday, December 4, 2019

DKT MAHIGA AWATAKA WATENDAJI WA SERIKALI KUSIMAMIA KIKAMILIFU ZOEZI LA USAJILI WA VIFO NCHINI

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akiwa katika picha ya pamoja Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA na viongozi wa Mkoa wa Njombe baada ya kikao cha tathmini cha viongozi kuhusu mpango wa maboresho na usajili wa vifo katika Mkoa huo.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akiongea na viongozi wa Mkoa wa Njombe kuhusu mpango wa Maboresho na usajili wa vifo katika Mkoa huo.
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini Bi. Emmy Hudson akiongea kwenye kikao cha tathmini cha viongozi wa Mkoa wa Njombe kuhusu mpango wa maboresho na usajili wa vifo Mkoani humo.


xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Dkt Mahiga awataka watendaji wa Serikali kusimamia kikamilifu usajili wa vifo nchini

Licha ya kuwepo kwa faida nyingi za usajili wa vifo nchini, lakini kumekuwepo na mwamko mdogo wa wananchi kuona umuhimu wa zoezi hilo mara baada ya kifo.

Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi yao, idadi ya vifo nchini  vilivyosajiliwa inaonesha ni asilimia 17.5% tu hii inamaanisha vifo vingi haviandikishwi nchini.

Katika tathmini ya zoezi la usajili wa vifo mkoa wa Njombe lililofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya mji wa Njombe, Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Dkt. Augustine Mahiga amesema takwimu hizo haziridhishi na kuwataka watendaji kufanya jitihada za ziada ili kufikia malengo ya zoezi.

“Takwimu hizi haziridhishi kwa hiyo tufanye jitihada za maksudi ili tuweze kufikia asilimia kubwa zaidi na ninaomba mikoa mingine iige mfano wa Njombe kwasababu katika asilimia Njombe bado mnaongoza ukilinganisha na mikoa mingine” amesema Waziri Mahiga

Dkt. Mahiga aliongeza kuwa ni muhimu kuandikisha na kupata cheti cha kifo mara inapotokea ili kuweza kupata stahiki zinazomuhusu marehemu.

“Ni muhimu sana kuhakikisha tunaandikisha vifo ili kupata vyeti vya kifo ambavyo vinatumika kama uthibitisho wa kisheria na hutumiwa na familia na ndugu kupata stahiki mbali mbali zinazomuhusu marehemu. Ni muhimu kusajili vifo mara tu vinapotokea hata kama ni vya watoto waliozaliwa na kuishi kwa dakika chache” ameongeza Mahiga.

Kwa upande wake Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu/Afisa Mtendaji Mkuu Bi Emmy Hudson amesema Utekelezaji wa mpango wa usajili wa matukio ya vifo katika Mkoa wa Njombe ninsehemu ya mageuzi makubwa yanayofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wa maendeleo katika kuhakikisha kwamba kiwango cha usajili wa matukio muhimu ya binadamu (Civil Registration and Vital Statistics - CVRS) kinakuwa Bora zaidi kwani hali kwa sasa siyo nzuri.

Hii ni programu ya pili ya mkakati huu kutekelezwa katika Mkoa wa Njombe unaounganisha utekelezaji wa usajili wa watoto chini ya miaka mitano.

"Usajili wa kifo siyo jambo geni kwani umekuwa ukifanyika tangu wakati wa ukoloni japokuwa mpaka sasa mwitikio bado ni mdogo kutokana na sababu mbalimbali ikiwa pamoja na wananchi kutokuona umuhimu wake." Amesema Emmy Hudson.

"Kama wakala tunaendelea kuhamasisha wananchi na kusisitiza kwamba ni muhimu sana vifo vyote visajiliwe mara tu vinaootokea" ameongeza Emmy Hudson.

Viongozi wa Mkoa wa Njombe wamekutana leo tarehe 4 Desemba kufanya tathmini ya Mpango wa Maboresho ya Usajili wa Vifo katika Mkoa huo na kumhusisha Waziri wa Katiba na Sheria ambaye alikuwa katika ziara ya siku mbili kujionea utendaji kazi wa RITA.

Monday, December 2, 2019

Dkt Mahiga Awataka Wakuu wa Magereza Nchini Kutumia Ujuzi wa Wafungwa Kujiendesha na Kutoa Mchango wa Gawio kwa Serikali

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akisaini kitabu cha wageni alipotembelea gereza la Mahabusu Wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya wakati akiendelea na ziara yake.

Viongozi mbalimbali walioambatana na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga wakiingia kwenye gereza la  Mahabusu Wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya .
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Waziri wa Katiba na Sheria Mheshimiwa Balozi Dkt Augustine Mahiga amewataka Wakuu wa Magereza nchini kutumia nguvu kazi na ujuzi wa wafungwa walioko magerezani kubuni miradi mbalimbali ili kuwazalishia fedha zitakazowawezesha kujiendesha bila kutegemea ruzuku kutoka serikalini.

Balozi Mahiga ameyasema hayo leo alipotembelea gereza la Kyela kujionea jinsi Taasisi za Haki Jinai zinavyotekeleza majukumu yake katika mahakama na magereza ikiwemo kutatua changamoto ya mrundikano wa mahabusu katika magereza pamoja na kuboresha mfumo wa utoaji haki na hali ya magereza kote nchini.

“Nguvu kazi za hawa wafungwa ni nyingi na wana ujuzi mbalimbali mnaoweza kuutumia kuanzisha miradi ambayo itawasaidia kupata fedha na mkaweza kujiendesha bila kutegemea ruzuku kutoka serikalini, watumieni. Pale Dar es Salaam natazama yale majengo ya magereza mnajengewa na jeshi wakati mngeweza kujenga wenyewe.”

Kwa upande wake Mkuu wa Gereza la Kyela ASP. Nelson.M. Mwaifani amesema kwamba wao wamejitahidi kuhakikisha kwamba gereza hilo halina msongamano wa mahabusu na kwamba mazingira ya wafungwa na mahabusu ni mazuri salama kwa afya za watu hao kwani wana mabweni na magodoro yanayowatosha wafungwa na mahabusu wote waliopo katika gereza hilo. Pamoja na hayo ASP. Mwaifani amemwambia Waziri Mahiga aliyeambatana na Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka Biswalo Mganga kwamba wameingia mkataba na Halmashauri ya Wilaya ya Kyela ya kuzoa taka ngumu, kuzibua mifereji na kufanya usafi katika hospitali ya Wilaya kwa makubalino ya kulipwa shilingi 6,700,000/-.

Hata hivyo, Dkt. Mahiga alifurahishwa na uongozi wa gereza la Kyela chini ya ASP. Nelson.M. Mwaifani kwa kuwa wabunifu na kushirikiana vizuri na Halmashauri ya Kyela kiasi cha kufanikiwa kupata tenda ya kufanya usafi katika Halmashauri hiyo jambo linalowaingizia wastani wa cha shilingi milioni sita kwa mwezi. Aidha aliwataka wakuu wote wa Magereza nchini kuiga mfano huo na kwamba siku moja wawe sehemu ya taasisi za serikali zitakazotoa gawio mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt John Joseph Pombe Magufuli.

“Nataka siku moja gereza hili lichangie kwenye mgao wa pesa za Taasisi ya Mahakama kwaajili ya gawio la kwenda serikalini mbele ya Rais, nikisikia, nitafurahi sana. Nina uhakika hivi karibuni tutaulizwa mchango wenu ni nini kwenye gawio la serikali. Najua mnaweza kuwa vyanzo vingi vya kupata pesa hivyo ni matumaini yangu kuwa gawio lijalo Wizara yetu au Taasisi ndani ya wizara yetu itatoa kitu (‘very signficant’) kikubwa, na magereza nina uhakika. Kule sabasaba kila mwaka mnapata zawadi tena nzuri tu, mnaongoza, sasa hapa onesheni mfano mzuri.” Amesema Dkt. Mahiga.

Hivi Karibuni Mheshimiwa Rais Dkt. John Joseph Pombe Magufuli azitaka Taasisi za Umma zinazozalisha na kupata faida zitoe gawio kwa serikali na kuzipa siku 60 Taasisi,Mashirika na Makampuni ya serikali ambayo hajatoa yafanye hivyo ndani ya muda huo. Waziri Mahiga ameamua kutumia ziara yake ya siku saba pamoja na mambo mengine kuzipa changamoto Taasisi za utoaji haki jinai kuanza kufikiria namna ya kuweka mikakati madhubuti ili nazo zianze kutoa gawio kwa serikali. Ziara hii iliyoendelea leo katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kyela na Gereza la Kyela, itaendelea tena kesho katika Wilaya ya Mbarali jijini Mbeya.

SERIKALI YATAIFISHA MAGARI MANNE NA PIKIPIKI 16 KWA KOSA LA KUJIHUSISHA NA UHALIFU JIJINI MBEYA

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akiangalia magari yaliyotaifishwa na Serikali kwa kosa la kujihusisha na uhalifu mbalimbali wakati akiendelea na ziara yake jijini Mbeya.