Dkt Mahiga Awataka Wakuu wa Magereza Nchini Kutumia Ujuzi wa Wafungwa Kujiendesha na Kutoa Mchango wa Gawio kwa Serikali

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akisaini kitabu cha wageni alipotembelea gereza la Mahabusu Wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya wakati akiendelea na ziara yake.

Viongozi mbalimbali walioambatana na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga wakiingia kwenye gereza la  Mahabusu Wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya .




XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Waziri wa Katiba na Sheria Mheshimiwa Balozi Dkt Augustine Mahiga amewataka Wakuu wa Magereza nchini kutumia nguvu kazi na ujuzi wa wafungwa walioko magerezani kubuni miradi mbalimbali ili kuwazalishia fedha zitakazowawezesha kujiendesha bila kutegemea ruzuku kutoka serikalini.

Balozi Mahiga ameyasema hayo leo alipotembelea gereza la Kyela kujionea jinsi Taasisi za Haki Jinai zinavyotekeleza majukumu yake katika mahakama na magereza ikiwemo kutatua changamoto ya mrundikano wa mahabusu katika magereza pamoja na kuboresha mfumo wa utoaji haki na hali ya magereza kote nchini.

“Nguvu kazi za hawa wafungwa ni nyingi na wana ujuzi mbalimbali mnaoweza kuutumia kuanzisha miradi ambayo itawasaidia kupata fedha na mkaweza kujiendesha bila kutegemea ruzuku kutoka serikalini, watumieni. Pale Dar es Salaam natazama yale majengo ya magereza mnajengewa na jeshi wakati mngeweza kujenga wenyewe.”

Kwa upande wake Mkuu wa Gereza la Kyela ASP. Nelson.M. Mwaifani amesema kwamba wao wamejitahidi kuhakikisha kwamba gereza hilo halina msongamano wa mahabusu na kwamba mazingira ya wafungwa na mahabusu ni mazuri salama kwa afya za watu hao kwani wana mabweni na magodoro yanayowatosha wafungwa na mahabusu wote waliopo katika gereza hilo. Pamoja na hayo ASP. Mwaifani amemwambia Waziri Mahiga aliyeambatana na Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka Biswalo Mganga kwamba wameingia mkataba na Halmashauri ya Wilaya ya Kyela ya kuzoa taka ngumu, kuzibua mifereji na kufanya usafi katika hospitali ya Wilaya kwa makubalino ya kulipwa shilingi 6,700,000/-.

Hata hivyo, Dkt. Mahiga alifurahishwa na uongozi wa gereza la Kyela chini ya ASP. Nelson.M. Mwaifani kwa kuwa wabunifu na kushirikiana vizuri na Halmashauri ya Kyela kiasi cha kufanikiwa kupata tenda ya kufanya usafi katika Halmashauri hiyo jambo linalowaingizia wastani wa cha shilingi milioni sita kwa mwezi. Aidha aliwataka wakuu wote wa Magereza nchini kuiga mfano huo na kwamba siku moja wawe sehemu ya taasisi za serikali zitakazotoa gawio mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt John Joseph Pombe Magufuli.

“Nataka siku moja gereza hili lichangie kwenye mgao wa pesa za Taasisi ya Mahakama kwaajili ya gawio la kwenda serikalini mbele ya Rais, nikisikia, nitafurahi sana. Nina uhakika hivi karibuni tutaulizwa mchango wenu ni nini kwenye gawio la serikali. Najua mnaweza kuwa vyanzo vingi vya kupata pesa hivyo ni matumaini yangu kuwa gawio lijalo Wizara yetu au Taasisi ndani ya wizara yetu itatoa kitu (‘very signficant’) kikubwa, na magereza nina uhakika. Kule sabasaba kila mwaka mnapata zawadi tena nzuri tu, mnaongoza, sasa hapa onesheni mfano mzuri.” Amesema Dkt. Mahiga.

Hivi Karibuni Mheshimiwa Rais Dkt. John Joseph Pombe Magufuli azitaka Taasisi za Umma zinazozalisha na kupata faida zitoe gawio kwa serikali na kuzipa siku 60 Taasisi,Mashirika na Makampuni ya serikali ambayo hajatoa yafanye hivyo ndani ya muda huo. Waziri Mahiga ameamua kutumia ziara yake ya siku saba pamoja na mambo mengine kuzipa changamoto Taasisi za utoaji haki jinai kuanza kufikiria namna ya kuweka mikakati madhubuti ili nazo zianze kutoa gawio kwa serikali. Ziara hii iliyoendelea leo katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kyela na Gereza la Kyela, itaendelea tena kesho katika Wilaya ya Mbarali jijini Mbeya.

Comments

Popular posts from this blog

USAJILI WA VIZAZI NA VIFO NI TAKWA LA KISHERIA

BODI YA KITAIFA YA USHAURI YA MSAADA WA KISHERIA YATEMBELEA WASAIDIZI WA KISHERIA IRINGA