NAIBU KATIBU MKUU MPANJU ATOA WITO KWA VIONGOZI WA DINI KUHAMASISHA WANANCHI KUSAJILI WATOTO ILI KUPATIWA VYETI VYA KUZALIWA
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya
Katiba na Sheria Ndg. Amon Mpanju awaomba viongozi wa dini na kuwataka
watendaji wa Serikali kuhamasisha waumini na wananchi waliopo maeneo yao
kupeleka watoto kusajiliwa na kupatiwa vyeti vya kuzaliwa.
Mpanju ameyasema hayo wakati wa
uzinduzi wa mpango wa usajili wa watoto wa umri chini ya miaka mitano katika
mikoa ya Morogoro na Pwani uliofanyika wiki hii katika viwanja vya uwanja wa
ndege Mkoani Morogoro.
“Nitoe wito kwa viongozi wa dini
zetu popote walipo kwenye mikoa ya Morogoro na Pwani, viongozi wa kijamii,
wenyeviti wetu wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji waliochaguliwa hivi
karibuni na watendaji kwa ngazi zote kuhakikisha mnahamasisha wananchi wetu
kwenye mikoa hii wajitokeze katika kampeni inayoendelea kuwasajili watoto na
kupatiwa cheti bure”alisema.
Aidha ndg Mpanju aliwaeleza
viongozi hao kwamba zoezi hilo linagusa mtoto aliyezaliwa mwishoni mwa mwaka
2014 mpaka wanaozaliwa sasahivi hivyo, wawahamasishe wazazi na walezi
wajitokeze kusajili watoto na kupata vyeti bure.
Mpanju alisisitiza “Kwa hiyo nitoe rai kwa viongozi wa dini na
watendaji wa Serikali kote nchini ambako kampeni hii inaendelea tutumie mimbali
za makanisa, misikiti na majukwaa yetu ya kisiasa na kwenye maeneo ya kazi
tuhakikishe habaki mtoto mwenye sifa bila kusajiliwa na kupata cheti”
Zoezi hili la uandikishaji linaloendelea
katika mikoa 15 ya Tanzania Bara linatarajiwa kuifikia mikoa mingine yote
iliyobaki ndani ya kipindi cha miaka mitatu kuanzia sasa.
Comments
Post a Comment