USAJILI WA VIZAZI NA VIFO NI TAKWA LA KISHERIA

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akizindua zoezi la uandikishaji wa watoto wa umri chini ya miaka mitano na ugawaji wa vyeti kwa watoto hao katika mikoa ya Morogoro na Pwani uliofanyika katika viwanja vya uwanja wa Ndege Mkoa wa Morogoro.

 Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akionesha cheti cha kuzaliwa kwa wananchi waliofika kwenye uzinduzi wa uandikishaji wa watoto wa umri chini ya miaka mitano na ugawaji wa vyeti kwa watoto hao katika mikoa ya Morogoro na Pwani.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Ndg. Amon Mpanju akiongea na wananchi kwenye uzinduzi wa uandikishaji wa watoto wa umri chini ya miaka mitano na ugawaji wa vyeti kwa watoto hao katika mikoa ya Morogoro na Pwani.

 Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akiangalia cheti cha kuzaliwa mtoto baada ya kuandikishwa  kwenye uzinduzi wa uandikishaji wa watoto wa umri chini ya miaka mitano na ugawaji wa vyeti kwa watoto hao katika mikoa ya Morogoro na Pwani.

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu RITA Bi. Emmy Hudson akiongea na wananchi kwenye uzinduzi wa uandikishaji wa watoto wa umri chini ya miaka mitano na ugawaji wa vyeti kwa watoto hao katika mikoa ya Morogoro na Pwani.


Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (kushoto) akisalimiana na Mwenyekiti wa Bodi ya RITA Prof. Hamisi Dihenga wakati wa uzinduzi wa uandikishaji wa watoto wa umri chini ya miaka mitano na ugawaji wa vyeti kwa watoto hao katika mikoa ya Morogoro na Pwani.


xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

Usajili wa Vizazi na vifo ni jambo la lazima kwa wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani limetamkwa kwenye sheria ya uandikishaji vizazi na vifo, (sura 108 toleo la 2002), hivyo, wananchi wote wanapaswa kuwa waelimishaji na wahamasishaji ili vizazi na vifo viandikishwe kwa maendeleo endelevu ya Taifa la Tanzania kuelekea uchumi wa kati na uchumi wa viwanda.

Haya yamesemwa na Waziri wa Katiba na Sheria Mheshimiwa Balozi Dkt. Augustine Mahiga wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Mpango wa Usajili wa Watoto wa Umri Chini ya Miaka Mitano ulioambatana na utaoji wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto hao katika Mikoa ya Morogoro na Pwani uliofanyika katika viwanja vya uwanja wa Ndege Mkoa wa Morogoro katikati ya wiki hii.

Balozi Mahiga ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo alisema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali zenye lengo la kuboresha mfumo wa uandikishaji wa vizazi, ndoa, talaka na vifo kwa kuzingatia umri wa makundi mbalimbali kupitia mkakati wa kitaifa wa usajili wa matukio muhimu ya binadamu na kuyapa nguvu ya kisheria kupitia Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) ambayo ipo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria.

“Vilevile katika kuhakikisha kwamba maboresho haya yanapata nguvu ya kisheria, mnamo mwezi Septemba 2019, Bunge lilipitisha Sheria mpya ya usajili wa Vizazi na Vifo ambayo tayari Imeshasainiwa na Mheshimiwa Rais na sasa tunaendelea kuandaa kanuni za utekelezaji wa Sheria hiyo”. Alisema Dkt. Mahiga.

Kwa upande wake Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu wa RITA Bi Emmy Hudson wakati akitoa hotuba yake mbele ya mgeni rasmi alisema kuwa licha ya zoezi la uandikishaji vizazi na vifo kuwa na umri usiopungua miaka 100  bado mwitikio na wanachi kuandikisha vizazi na vifo ni hafifu sana hivyo kurudisha nyuma mipango ya maendeleo nchini.

“kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 wananchi waliokuwa wamezaliwa Tanzania Bara na kustahili kupatiwa vyeti walikuwa 13.4%. Upo uwezekano wa hali kuwa mbaya zaidi kutokana na kutokuwa na uwiano sawia kati ya idadi ya ongezeko la idadi ya watu na kiwango cha usajili kwani kila siku tukio la kufa na kuzaliwa linatokea hivyo tusipoweka nguvu ya kusajili vizazi na vifo tutajikuta katika hatari ya kuwa na idadi ndogo ya watu waliosajiliwa hali itakayodhoofisha mipango ya maendeleo nchini”.

Nae Naibu Katibu MKuu wa Wizara ya Katiba na Sheria ndugu Amon Mpanju aliposimama kutoa salamu za Wizara aliipongeza RITA chini ya uongozi Madhubuti wa Mwenyekiti wa Bodi Prof. Hamisi Dihenga na Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu wa RITA Bi Emmy Hudson kwa kutekeleza kikamilifu Mpango Mkakati wa Usajili wa Matukio Muhimu ya Binadamu kama yalivyotamkwa katika kutambua sheria ya RITA ya usajili ya 2002 pamoja na kutekeleza maelekezo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya kutambua watu wake (watanzania) popote walipo ili waweze kufikiwa na huduma za kijamii. 

“Kinachofanyika leo ni ushahidi dhahili wa utekelezaji wa mpango huo na pia kutekeleza maelekezo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya kutambua watu wake (watanzania) popote walipo ili waweze kufikiwa na huduma za kijamii”.

Mpanju alimalizia kwa kuupongeza uongozi wa mikoa ya Morogoro na Pwani na watendaji walioenea katika wilaya za mikoa hiyo miwili kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kuandikisha watoto zaidi ya elfu 95 ndani ya muda mfupi.

 “Nipongeze uongozi wa mikoa ya Morogoro na Pwani kwa namna walivyoanza zoezi hili kwa kishindo, zoezi hili limeanza mnamo tarehe sita mwezi huu, leo ni takribani siku ya tano lakini usajili wa watoto ambao wameshasajiliwa na kupewa vyeti ni zaidi ya elfu 95. Hii inaonesha ni namna gani wamejitoa kwa kazi hii na pongezi nyingi ziwafikie watendaji wetu ambao mmeenea katika wilaya zetu zote za mikoa hii miwili kuhakikisha zoezi linafana, endeleeni hivyo kwani mnachokifanya ni kuisaidia serikali yenu katika kuwafikia wanyonge katika kupata huduma za kijamii”

Waziri Mahiga alihitimisha hotuba yake kwa kuwapongeza RITA na wadau wengine wa maendeleo kama UNICEF, Canada na Kampuni ya Mtandao wa Simu za Mkononi, TIGO kwa kuwezesha watoto wa kitanzania zaidi ya milioni 3.6 kupata vyeti vyao vya kuzaliwa ndani ya miaka 13 ambayo mpango huu unatekelezwa na kuagiza kwamba jitihada ziendelee na nguvu kubwa iwekezwe ili idadi ya uandikishaji wa watoto wenye umri chini ya miaka mitano uongezeke zaidi na ataendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa zoezi hilo.

“Naomba nichukue nafasi hii kuwapongeza tena RITA na wadau wengine wote kwa kuwezesha watoto wa kitanzania zaidi ya milioni 3.6 kupata vyeti vyao vya kuzaliwa katika miaka 13 ambayo mpango huu unatekelezwa na ninaamini katika kipindi cha kampeni tukiweza kusajili 90% ya watoto katika mikoa ya Morogoro na Pwani kama tulivyo azimia, idadi basi itaweza kufikia milioni nne (4) na nitaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa zoezi hili, naamini hamtaniangusha”. Alihitimisha Balozi Mahiga.

Takwimu zinaonesha kwamba idadi ya watoto waliozaliwa bila kusajiliwa na wengi wao wakiwa ni watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano inaongezeka kwa haraka sana na hivyo Wakala ya Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma (PO – PSM) pamoja na wadau wengine wa maendeleo wanatekeleza mfumo wa Usajili wa vizazi na vifo uliyoboreshwa (BRS) ambao hutumia teknolojia mpya ya habari na mawasiliano (TEHAMA) ili kusajili watoto wengi nchini Tanzania katika miaka mitano ijayo.

Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YAIPONGEZA WIZARA KWA UTEKELEZAJI WA MAMA SAMIA LEGAL AID CAMPAIGN

TUFANYE KAZI KWA UADILIFU NA USHIRIKIANO - MHE CHANA