Wednesday, January 29, 2020

KATIBU MKUU KATIBA NA SHERIA APOKEA UGENI WA MWAKILISHI MKAZI WA UNDP BI. CHRISTINE MUSISI

Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome (kulia) akiongea na Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa Bi. Christine Musisi alipomtembelea ofisini kwake, Mji wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma kwa ajili ya kujitambulisha. Mwingine pichani ni  Bw. Godfrey Mulisa Mtaalam wa masuala ya utawala wa Umoja wa Mataiafa.

Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome (kushoto) akiongea na Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa Bi. Christine Musisi (kulia) alipomtembelea ofisini kwake, Mji wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma kwa ajili ya kujitambulisha. Wengine pichani ni Wakurugenzi kutoka Wizarani hapo.

Tuesday, January 21, 2020

Habari Picha: Baraza la wafanyakazi Tume ya Kurekebisha Sheria

 Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la TUMESHERIA na viongozi wao katika picha ya pamoja muda mchache kabla ya Uzinduzi wa Baraza hilo uliofanyika Ngorongoro


Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome akiwahutubia Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la TUMESHERIA wakati wa  Uzinduzi wa Baraza hilo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome (katikati) akufuatilia mada katika Hafla ya Uzinduzi wa Baraza la Wafanyakazi la TUMESHERIA

Afisa kutoka Ofisi ya Rais UTUMISHI Bi. Mwanvita Shamte (katikati) akitoa mada wakati wa Uzinduzi wa Baraza la Wafanyakazi TUMESHERIA
Katibu wa TUGHE wa Mkoa wa Manyara Bw. Yakubu salim akifafanua jambo wakati wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania.

Katibu MKuu Katiba na Sheria Awataka TUMESHERIA Kuendeleza Watumishi Kitaaluma
Uongozi wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania yatakiwa kuwaendeleza watumishi wake kitaaluma ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao na kuweka mpango maalum wa kutambua mchango wa watumishi wao katika maendeleo ya Tume na Taifa kwa ujumla.

Maelekezo hayo yametolewa na Katibu Mkuu wa Katiba na Sheria Profesa Sifuni Mchome wakati akizindua Baraza jipya la Wafanyakazi wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania katika Mkutano wa 14 wa Baraza hilo uliofanyika jana katika ukumbi wa Mikutano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

“Watumishi ni rasilimali muhimu kuliko zote kwani ndiyo inayowezesha rasilimali nyingine ziwe na thamani, kwa maana hiyo kuna umuhimu mkubwa sana kwa Menejimenti ya Tume kuwawezesha  na kuwaendeleza watumishi wake kitaaluma kulingana na kada zao” alisema Prof. Mchome.

Aidha, Prof. Mchome aliliasa Baraza la Wafanyakazi la TUMESHERIA kuweka mzingira mazuri yanayomruhusu mwajiri kuwajengea uwezo watumishi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kunakuwa na Mpango wa Mafunzo ambao utafuatwa na kutekelezwa vizuri na kwamba, watumishi watakaotekeleza majukumu yao vizuri, kuwepo na mpango maalumu wa kutambua mchango wao kwa kipindi kinachokubalika ndani ya Taasisi. Kwa kujali maslahi ya watumishi, ni dhahiri shahiri kwamba Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania itapata matokeo chanya kutokana na kuboreka kwa utendaji na ufanisi wa watumishi wake.
“Baraza la Wafanyakazi ni ushahidi wa uwepo wa demokrasia mahala pa kazi kwakuwa ni chombo kinachowashirikisha wafanyakazi kupanga, kusimamia na kutekeleza mipango mbalimabili ikiwemo mafunzo ya watumishi hivyo ni lazima muweke mzingira mazuri yanayomruhusu mwajiri kuwajengea uwezo watumishi wake ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kunakuwa na Mpango wa Mafunzo ambao utafuatwa na kutekelezwa vizuri. Watumishi watakaotekeleza majukumu yao vizuri, hakikisheni kunakuwepo na mpango maalumu wa kutambua mchango wao kwa kipindi kinachokubalika ndani ya Taasisi” alisisitiza Prof. Mchome.

Aidha, Prof. Mchome amewaasa Baraza la Wafanyakazi la TUMESHERIA kuwa mshiriki na mdau mkubwa katika kubuni mbinu mpya za uendeshaji na kukabiliana na changamoto mbalimbali ili kuisaidia Taasisi na Serikali kwa ujumla kuboresha maslahi wafanyakazi na uhusiano wa kiutendaji baina ya Watumishi na Menejimenti badala ya kuwa chombo cha kupokea malalamiko ya wafanyakazi pekee. “Mabaraza yanapaswa kusaidia kutoa suluhisho na fursa kwa wafanyakazi kushiriki katika maamuzi mbalimbali na kuboresha uhusiano baina ya Wafanyakazi na viongozi (menejimenti) pamoja na mazingira ya utendaji kazi mahala pa kazi” alimalizia Katibu Mkuu huyo.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria Bw. Casmir Kyuki alisema kwamba TUMESHERIA imefanya tathmini ya mahitaji ya mafunzo na kuandaa Mpango wa Mafunzo pamoja na Urithishwaji wa Madaraka (Succession Plan) kwa lengo la kuwaongezea uwezo watumishi wake na kumuunga mkono Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika kuipeleka Tanzania katika maendeleo ya uchumi wa kati na wa viwanda.

Bwana Kyuki alifafanua kwamba katika kipindi cha Julai hadi Desemba, 2019, watumishi saba wa kada tofautitofauti walihudhuria mafunzo yaliyohusu kufanya manunuzi kwa njia ya mtandao (TANEPS) na Uandaaji wa wa Mipango na Bajeti pamoja na mafunzo ya Uandaaji wa Mfumo Mpya wa Neno Kuu (Key Word Filling Classification System) wa utunzaji wa kumbukumbu lengo likiwa ni kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ndani ya Tume na serikali kwa ujumla.

“katika kipindi cha Julai hadi Desemba, 2019, watumishi saba katika kada tofautitofauti walihudhuria mafunzo ikiwa ni matokeo ya kufanya tathmini ya mahitaji ya mafunzo na kuandaa Mpango wa Mafunzo pamoja na Urithishwaji wa Madaraka (Succession Plan) kwa lengo la kuwaongezea uwezo watumishi wetu na kumuunga mkono Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika kuiletea Tanzania maendeleo ya uchumi wa kati na wa viwanda”. Alisema Bw. Kyuki.

Mkutano wa 14 wa Baraza la Wafanyakazi la TUMESHERIA unaofanyika kwa siku mbili katika Ukumbi wa Mikutano wa Makao Mkuu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro pamoja na mambo mengine, mada kuu nne zimewasilishwa na kuwapa fursa wajumbe kuzijadili na kujiongezea uwezo na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao kwa mujibu wa sheria na kwa kuzingatia agizo la Rais Na. 1 la mwaka 1970. Mada hizo ni: Umuhimu wa Maadili katika Utumishi wa Umma; Mabadiliko yaliyotokana na Kuunganishwa kwa Mifuko ya Pensheni; nyingine ni: Utekelezaji wa Bajeti ya Tume kwa mwaka 2019/20 na Mwelekeo wa Bajeti ya Tume kwa mwaka wa Fedha 2020/2012 na Mwongozo wa Kuandaa Ikama na Bajeti ya Mishahara kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 na Mabadiliko Mbalimbali ya Miundo ya Kiutumishi.