Thursday, February 27, 2020

WIZARA YA KATIBA NA SHERIA WAFANYA UCHAGUZI KUPATA WAJUMBE WA BARAZA LA WAFANYAKAZI

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Deogratias Yinza akiongoza kikao cha uchaguzi wa wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo.

Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dodoma Bw. Antelmas Tarimo (aliyesimama) akitoa sifa za wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi kabla ya uchaguzi wa wajumbe wa baraza hilo.

Baadhi ya watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria wakisikiliza maelekezo kabla ya kufanya uchaguzi wa wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi.


Msimamizi wa uchaguzi wa wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Neema Dickson (kulia) akisimamia zoezi la kuhesabu kura.

Msimamizi wa uchaguzi wa wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Neema Dickson akitangaza matokeo ya uchaguzi huo.

XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Wizara ya Katiba na Sheria Ndg. Deogratias Yinza awataka wajumbe waliochaguliwa kuwawakilisha wenzao kwenye baraza la wafanyakazi kuhakikisha wanawakilisha vyema mawazo ya wenzao waliowachagua.

Hayo ameyasema kwenye zoezi la uchaguzi wa wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara hiyo baada ya wajumbe wa awali kumaliza muda wao mwishoni mwa mwaka jana.

“Wawakilishi mliochaguliwa kuwawakilisha wenzenu kwenye baraza la wafanyakazi mhakikishe mnawakilisha vyema mawazo ya waliowachagua” alisema.

Aidha, Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dodoma Bw. Antelmas Tarimo alitaja sifa za mjumbe wa baraza ikiwmo mtu anayejitambua, anayejitoa na mchapakazi, pia awe anajua baadhi ya mambo ya kisheria na utumishi ili kumwezesha kuhoji vizuri mambo muhimu mfano haki za watumishi.

Aliongeza, wajumbe wazuri wanaotoa mawazo ya kusaidia taasisi ni muhimu kwenye baraza na sio kuangalia urafiki ili kuboresha maslahi na utendaji wa taasisi.

“Usichague mtu sababu ni rafiki au mmezoeana”, alisema Tarimo.

Naye Afisa kazi Mkoa wa Dodoma Bi. Neema Dickson ambaye ni msimamizi mkuu wa uchaguzio huo alisema waliochaguliwa washiriki ipasavyo kuwawakilisha wenzao ili kutatua changamoto zinazo wakabili na kuwakilisha mawazo yao vyema kwa viongozi wa baraza.

Katika uchaguzi huo kila Idara na Kitengo ilichagua mjumbe ambaye ana jukumu la kuwasilisha mawazo na maoni yake pamoja na ya wenzake katika kikao cha baraza la wafanyakazi kinachofanyika kila mwaka.


Tuesday, February 25, 2020

TANZANIA NA CHAMA CHA UTAWALA WA SHERIA CHA KIMATAIFA CHA IRELAND KUKOMESHA UNYANYASAJI WA KIJINSIA

Wanachama wa Chama cha Utawala wa Sheria cha Kimataifa cha Ireland wakiwa katika kikao na wataalam kutoka Wizara ya Katiba na sheria kwenye kikao chao kuangalia maeneo ambayo wanaweza kushirikiana ili kuiboresha sekta ya Sheria nchini.

Mkurugenzi wa Idara ya Rasilimali za Asili Bibi neema Mwanga (kulia) kutoka Wizara ya Katiba na Sheria akisisitiza jambo kwenye kikao na wageni kutoka  Chama cha Utawala wa Sheria cha Kimataifa cha Ireland walipokuwa wakijadiliana maeneo ambayo wanaweza kushirikiana ili kuiboresha sekta ya Sheria nchini.
Picha ya pamoja ya Wakurugenzi wa Wizara ya Katiba na sheria na wageni kutoka Chama cha Utawala wa Sheria cha Kimataifa cha Ireland baada ya kumaliza kikao chao.

XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na Chama cha Utawala wa Sheria cha Ireland wajipanga kukomesha unyanyasaji wa kijinsia na watoto nchini.

Katika kikao kilichofanyika Wizarani hapo mapema leo Mtumba, jijini Dodoma, wataalam kutoka Chama cha Utawala wa Sheria cha Ireland wameahidi kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Katiba na Sheria na Taasisi zake ikiwemo Mahakama katika kuzuia unyanyasaji wa kijinsia na watoto kwani ni tatizo linaloonekana kushika kasi kwa sasa.

Akizungumza katika kikao kutazama maeneo ya ushirikiano baina ya Taasisi hizi mbili Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Kisheria kwa Umma Bw. Griffin Mwakapeje alisema ili kuleta matokeo chanya katika sekta ya sheria kwa sasa Tanzania inahitaji kushirikiana na wadau mbalimbali katika maeneo muhimu ikiwemo kuzuia unyanyasaji wa aina mbalimbali na kuwajengea uwezo watumishi kama Mawakili, Makarani na Mahakimu ili kuwawezesha kusimamia haki nchini.

Aidha, Bw. Griffin aliongeza kuwa wanawake wanaofanya shughuli za uchimbaji wa madini wanakumbana na changamoto nyingi kwani huko kuna unyanyasaji wa aina mbalimbali ikiwepo wa kijinsia hivyo ni muhimu jamii ielimishwe namna ya kulinda na kutetea haki zao ili waweze kufaidika na rasilimali za asili.

Chama cha Utawala wa Sheria cha Ireland kimekuwa kikitoa mchango mkubwa katika upatikanaji wa haki kwenye nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo Tanzania.

Friday, February 21, 2020

NAIBU KATIBU MKUU MPANJU ATAKA WALEMAVU KUFUATA SHERIA ZA NCHIXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Watu wenye ulemavu watakiwa kufuata sheria na taratibu ili kuepuka migongano na vyombo vya sheria nchini Tanzania.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na kituo cha Televisheni cha TBC 1 ofisini kwake Mtumba, jijini Dododma Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Ndg. Amon Mpanju ambaye pia ni mlemavu wa macho aliwataka wananchi wenye ulemavu watii sheria za nchi ili kuepukana na mkono wa sheria kwani ulemavu haumpi mtu yeyote uhalali wa kuvunja sheria.

“Taratibu na sheria za nchi lazima zifuatwe bila kujali ulemavu wa mwananchi na niwaombe wenzangu watambue kwamba ulemavu siyo tiketi ya kuvunja sheria” amesema  Mpanju. 

Naibu Katibu Mkuu huyo alisisitiza kwamba kila mwananchi bila kujali hali yake ana wajibu wa kufuata na kutii sheria zilizowekwa na nchi, vinginevyo ataadhibiwa kama sheria invyoelekeza. “Kukiwa na tataizo ni vema wawafuate viongozi na kuzungumza nao ili waweze kutatua changamoto walizonazo na sio kufanya vurugu kwa mwanvuli wa ulemavu au hali zao.”  Alisisitiza Mpanju.

Aidha, ndugu Mpanju aliwataka watu wenye ulemavu kutobweteka na badala yake wafanye kazi halali na kwa bidii ili kujipatia kipato kwani ulemavu haumpi mtu hela wala kutatua changamoto zozote za kimaisha.

“Ulemavu haukupi hela au maisha, hivyo ulemavu sio sababu ya kubweteka, watu wenye ulemavu wajielewe na kufanya kazi halali ili kujiongezea kipato” Alisema.

Vilevile alisisitiza kuwa watu wenye ulemavu ni jukumu lao kusimamia mambo yao wenyewe ikiwemo ujenzi wa majengo yanayofaa, kwa mfano, Sheria namba 9 ya mwaka 2010 ya watu wenye ulemavu imeelekeza majengo yote mapya yanayojengwa yazingatie miundombinu rafiki kwa walemavu. Hivyo, watu wenye ulemavu wajitahidi kutafuta elimu, ajira, matibabu na mahitaji mengine muhimu wanayohitaji na sio kubakia wanyonge kwa kuona wananyanyaswa na kwamba hawapewi haki zao.

Wizara ya Katiba na Sheria inasimamia mfumo wa haki kupitia taasisi zilizo chini yake zinazochangia uwepo wa utawala wa sheria nchini. Wananchi wote wakiwemo watu wenye ulemavu watumie taasisi zote zilizo chini ya Wizara kuhakikisha wanapata haki zao.Friday, February 14, 2020

BALOZI MAHIGA AONGOZA KIKAO CHA WAKUU WA HAKI JINAI KUANGALIA HALI HALISI YA MABARAZA YA ARDHI

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akiwa katika picha ya pamoja na Wakuu wa Taasisi za Haki Jinai nchini (Collegium) baada ya kumaliza kikao chao cha kuangalia hali halisi ya Mabaraza ya Ardhi nchini.

Mjumbe wa kikao cha kuangalia hali halisi ya Mabaraza ya Ardhi nchini ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi kutoka TAMISEMI Bw. Stanley Kamana akifafanua jambo katika kikao hicho.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akiongoza kikao cha Wakuu wa Taasisi za Haki Jinai nchini (Collegium) cha kuangalia hali halisi ya Mabaraza ya Ardhi nchini.Wednesday, February 12, 2020

SERIKALI YAKABIDHIWA MALI ZENYE THAMANI YA ZAIDI TSH. BILIONI 58
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Balozi Augustine Mahiga akizungumza katika hafla ya Serikali kukabidhiwa mali zilizotaifishwa zenye thamani ya shilingi Bilioni 58. Wengine pichani , kushoto ni Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango na kulia ni Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko Baadhi ya vipande vya dhahabu vikiwa katika begi.


Makasha yaliyohifadhi mali zilizotaifishwa zikiwemo fedha na dhahabu.


Baadhi ya Fedha zilizotaifishwa


Mkurugenzi wa Mashtaka akiwaonesha viongozi baadhi ya magari yaliyotaifishwa.


XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

SERIKALI kupitia Ofisi ya Taifa ya Mashtaka chini ya uongozi wa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) imefanikiwa kupata amri za kutaifisha mali mbalimbali zinazohusiana na uhalifu sambamba na fedha zilizolipwa  kutokana na kesi za madini zilizopo katika akaunti ya AFR katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zenye thamani ya zaidi ya Tsh Bilioni 58.

Akizungumza na waandishi wa vyombo vya habari mapema wiki hii Jijini Dar es Salaam, wakati wa makabidhiano ya mali hizo Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), Biswalo Mganga alisema Ofisi yake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imepata amri ya kutaifisha nyumba 24, magari 65, viwanja 9, mashamba 2, mbao 6894, jahazi  moja (1) lililotokana na uvuvi haramu kwenye ukanda wa bahari kuu ya Tanzania pamoja na boti moja ya Yohanda iliyohusika katika kuingiza nchini vipodozi vyenye sumu.

 ‘’Kwa ufupi ukichukua thamani ya madini na kiasi cha fedha zilizomo kwenye akaunti ya Asset Forfeiture Recovery (AFR) ya BOT unapata Tsh 19,639,782,781.46 ambazo nakabidhi, hivyo ukijumuisha thamani ya madini yote, fedha iliyolipwa kutokana na kesi zinazohusiana na madini pamoja na fedha zilizomo kwenye akaunti ya AFR jumla yake inakuwa Tsh 58,604,375,783.56’’ alisema Biswalo.

Biswalo anasema tangu kuzinduliwa rasmi kwa ofisi hiyo mwezi Agosti mwaka 2018, Ofisi yake imefanikiwa kutaifisha jumla ya kilo 397.937 za dhahabu zenye thamani ya Tsh Bilioni 32.2 zilizokuwa zikitoroshwa nje ya nchi na kuisababishia serikali kukosa mapato, ambapo kati ya hizo, kilo 351.76 za dhahabu zenye thamani ya Tsh Bilioni 29 zimeshakabidhiwa kwa Katibu Mkuu Hazina ambaye ndiye mtunzaji wa mali za Serikali.

‘’Leo hii nakabidhi jumla ya kilo 46.177 za dhahabu zenye thamani ya Tsh Bilioni 3.2, pamoja na hayo tumeendesha kesi na kufanikiwa kupata amri za kutaifisha madini aina ya Almas, Tanzanite, Silver, Amethyst, Rhodolite, Bati, Blue Sapphire, Spinel, Ruby, Tourmaline, Acuamarine, ambapo jumla ya thamani ya madini yote yaliyotaifishwa pamoja na faini zilizolipwa na washitakiwa ni Tsh Bilioni 42.2’’ alisema Biswalo.

Katika hatua nyingine, Biswalo alisema kufuatia marekebisho ya sheria mbalimbali Na. 11 ya mwaka 2019, Ofisi yake imeendesha kesi katika zoezi la washtakiwa kukiri makosa yao ambapo jumla ya Tsh Bilioni 12.36 zimeshalipwa kama kodi iliyokwepwa, faini na  fidia katika akaunti maalum iliyopo Benki Kuu ya Tanzania.

Akifafanua zaidi Biswalo alisema zoezi la urejeshaji wa fedha kwa washitakiwa 341 ambao hawajamaliza kutimiza makubalino linaendelea na makubaliano hayo yanapaswa kutekelezwa kama yalivyosajiliwa kwa amri ya mahakama, ambapo katika madai hayo Serikali inawadai washitakiwa wote kiasi cha Tsh Bilioni 32.

Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Augustine Mahiga alisema wakati umefika kwa Watanzania kunufaika kikamilifu na uwepo na rasilimali katika nchi yao ikiwemo madini ambayo katika miaka ya nyuma hayakuwa na usimamizi madhubuti, hivyo Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa rasilimali za nchi zinaleta manufaa endelevu kwa Taifa na wananchi wake.

Aidha Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango alisema zoezi la utaifishaji wa mali za uhalifu, ni dalili tosha kuwa Tanzania sio nchi maskini na hivyo hakuna sababu ya Serikali kwenda kukopa nje ya nchi na badala yake itaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha kuwa raslimali zake zitalindwa kwa nguvu zote hivyo kumtaka DPP na Waziri Biteko kutoogopa vitisho badala yake wawe tayari kufa kwaajili ya kulipigania Taifa. “kufa kwasababu ya kulipigania taifa ni heshima itakayokumbukwa siku zote kuliko kufa kwa aibu” alimaliza Waziri Mpango.


Thursday, February 6, 2020

MAKAMU MWENYEKITI TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWLA BORA ATEMBELEA BANDA LA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA KATIKA MAADHIMISHO YA WIKI YA SHERIA

Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Mohamed Hamad akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Idara ya Uangalizi wa Utajiri na Rasilimali Asilia kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Neema Mwanga alipotembelea banda hilo kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Sheria.

Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Mohamed Hamad akipokea Katiba ya mwaka 1977 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoka kwa Mkurugenzi wa Idara ya Uangalizi wa Utajiri na Rasilimali Asilia kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Neema Mwanga alipotembelea banda hilo kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Sheria.

Sunday, February 2, 2020

NAIBU MWANASHERIA MKUU ATEMBELEA BANDA LA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA

Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt. Evaristo Longopa akiangalia baadhi ya vipeperushi vinavyogawiwa kwa wananchi wanaotembelea banda la Wizara ya Katiba na Sheria katika maadhimisho ya Wiki ya sheria yanayoendelea katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.

NAIBU WAKILI MKUU WA SERIKALI ATEMBELEA BANDA LA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA

Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Mhe. Gabriel Malata akifafanua jambo alipotembelea banda la Wizara ya Katiba na Sheria katika Maadhimisho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma. Anayemsikiliza ni Mkurugenzi wa Idara ya Uangalizi wa utajiri na Rasilimali asilia wizarani hapo.
Mkurugenzi wa Idara ya Uangalizi wa Utajiri na Rasilimali Asilia waWizara ya Katiba na Sheria Kamishna Neema Mwanga akifafanua jambo kwa Naibu Wakili wa Serikali Mhe. Gabriel Malata alipotembelea banda hilo katika maadimisho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.

Saturday, February 1, 2020

SPIKA NDUGAI ATEMBELEA BANDA LA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA KWENYE MAADHIMISHO YA WIKI YA SHERIA

Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Job Ndugai akipata maelezo kuhusu shughuli zinazofanywa na Wizara ya Katiba na Sheria alipotembelea banda la Wizara hiyo katika Maadhimisho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.
Maafisa kutoka Wizara ya Katiba na Sheria wakimsikiliza Mhe. Ndugai alipotembelea banda la Wizara hiyo kutoka kulia ni Kamishna Neema Mwanga Mkurugenzi wa Idara ya Uangalizi wa utajiri wa asili na rasilimali asilia  katikati ni Bi. Ester Msambazi Wakili wa Serikali na mwingine ni Hussein Mandali Wakili.
Vipeperushi mbalimbali kwa ajili ya kutoa elimu kwa Umma kwenye maadhimisho hayo.