NAIBU KATIBU MKUU MPANJU ATAKA WALEMAVU KUFUATA SHERIA ZA NCHI
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Watu wenye ulemavu watakiwa kufuata sheria na taratibu ili
kuepuka migongano na vyombo vya sheria nchini Tanzania.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na kituo cha Televisheni
cha TBC 1 ofisini kwake Mtumba, jijini Dododma Naibu Katibu Mkuu Wizara ya
Katiba na Sheria Ndg. Amon Mpanju ambaye pia ni mlemavu wa macho aliwataka wananchi
wenye ulemavu watii sheria za nchi ili kuepukana na mkono wa sheria kwani
ulemavu haumpi mtu yeyote uhalali wa kuvunja sheria.
“Taratibu na sheria za nchi lazima zifuatwe bila kujali
ulemavu wa mwananchi na niwaombe wenzangu watambue kwamba ulemavu siyo tiketi
ya kuvunja sheria” amesema Mpanju.
Naibu Katibu Mkuu huyo alisisitiza kwamba kila mwananchi bila
kujali hali yake ana wajibu wa kufuata na kutii sheria zilizowekwa na nchi, vinginevyo
ataadhibiwa kama sheria invyoelekeza. “Kukiwa na tataizo ni vema wawafuate
viongozi na kuzungumza nao ili waweze kutatua changamoto walizonazo na sio
kufanya vurugu kwa mwanvuli wa ulemavu au hali zao.” Alisisitiza Mpanju.
Aidha, ndugu Mpanju aliwataka watu wenye ulemavu kutobweteka
na badala yake wafanye kazi halali na kwa bidii ili kujipatia kipato kwani ulemavu
haumpi mtu hela wala kutatua changamoto zozote za kimaisha.
“Ulemavu haukupi hela au maisha, hivyo ulemavu sio sababu ya
kubweteka, watu wenye ulemavu wajielewe na kufanya kazi halali ili kujiongezea
kipato” Alisema.
Vilevile alisisitiza kuwa watu wenye ulemavu ni jukumu lao
kusimamia mambo yao wenyewe ikiwemo ujenzi wa majengo yanayofaa, kwa mfano, Sheria
namba 9 ya mwaka 2010 ya watu wenye ulemavu imeelekeza majengo yote mapya
yanayojengwa yazingatie miundombinu rafiki kwa walemavu. Hivyo, watu wenye
ulemavu wajitahidi kutafuta elimu, ajira, matibabu na mahitaji mengine muhimu
wanayohitaji na sio kubakia wanyonge kwa kuona wananyanyaswa na kwamba hawapewi
haki zao.
Wizara ya Katiba
na Sheria inasimamia mfumo wa haki kupitia taasisi zilizo chini yake zinazochangia
uwepo wa utawala wa sheria nchini. Wananchi wote wakiwemo watu wenye ulemavu watumie taasisi zote zilizo chini ya Wizara kuhakikisha wanapata haki zao.
Comments
Post a Comment