SERIKALI YAKABIDHIWA MALI ZENYE THAMANI YA ZAIDI TSH. BILIONI 58




Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Balozi Augustine Mahiga akizungumza katika hafla ya Serikali kukabidhiwa mali zilizotaifishwa zenye thamani ya shilingi Bilioni 58. Wengine pichani , kushoto ni Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango na kulia ni Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko 



Baadhi ya vipande vya dhahabu vikiwa katika begi.


Makasha yaliyohifadhi mali zilizotaifishwa zikiwemo fedha na dhahabu.


Baadhi ya Fedha zilizotaifishwa


Mkurugenzi wa Mashtaka akiwaonesha viongozi baadhi ya magari yaliyotaifishwa.


XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

SERIKALI kupitia Ofisi ya Taifa ya Mashtaka chini ya uongozi wa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) imefanikiwa kupata amri za kutaifisha mali mbalimbali zinazohusiana na uhalifu sambamba na fedha zilizolipwa  kutokana na kesi za madini zilizopo katika akaunti ya AFR katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zenye thamani ya zaidi ya Tsh Bilioni 58.

Akizungumza na waandishi wa vyombo vya habari mapema wiki hii Jijini Dar es Salaam, wakati wa makabidhiano ya mali hizo Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), Biswalo Mganga alisema Ofisi yake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imepata amri ya kutaifisha nyumba 24, magari 65, viwanja 9, mashamba 2, mbao 6894, jahazi  moja (1) lililotokana na uvuvi haramu kwenye ukanda wa bahari kuu ya Tanzania pamoja na boti moja ya Yohanda iliyohusika katika kuingiza nchini vipodozi vyenye sumu.

 ‘’Kwa ufupi ukichukua thamani ya madini na kiasi cha fedha zilizomo kwenye akaunti ya Asset Forfeiture Recovery (AFR) ya BOT unapata Tsh 19,639,782,781.46 ambazo nakabidhi, hivyo ukijumuisha thamani ya madini yote, fedha iliyolipwa kutokana na kesi zinazohusiana na madini pamoja na fedha zilizomo kwenye akaunti ya AFR jumla yake inakuwa Tsh 58,604,375,783.56’’ alisema Biswalo.

Biswalo anasema tangu kuzinduliwa rasmi kwa ofisi hiyo mwezi Agosti mwaka 2018, Ofisi yake imefanikiwa kutaifisha jumla ya kilo 397.937 za dhahabu zenye thamani ya Tsh Bilioni 32.2 zilizokuwa zikitoroshwa nje ya nchi na kuisababishia serikali kukosa mapato, ambapo kati ya hizo, kilo 351.76 za dhahabu zenye thamani ya Tsh Bilioni 29 zimeshakabidhiwa kwa Katibu Mkuu Hazina ambaye ndiye mtunzaji wa mali za Serikali.

‘’Leo hii nakabidhi jumla ya kilo 46.177 za dhahabu zenye thamani ya Tsh Bilioni 3.2, pamoja na hayo tumeendesha kesi na kufanikiwa kupata amri za kutaifisha madini aina ya Almas, Tanzanite, Silver, Amethyst, Rhodolite, Bati, Blue Sapphire, Spinel, Ruby, Tourmaline, Acuamarine, ambapo jumla ya thamani ya madini yote yaliyotaifishwa pamoja na faini zilizolipwa na washitakiwa ni Tsh Bilioni 42.2’’ alisema Biswalo.

Katika hatua nyingine, Biswalo alisema kufuatia marekebisho ya sheria mbalimbali Na. 11 ya mwaka 2019, Ofisi yake imeendesha kesi katika zoezi la washtakiwa kukiri makosa yao ambapo jumla ya Tsh Bilioni 12.36 zimeshalipwa kama kodi iliyokwepwa, faini na  fidia katika akaunti maalum iliyopo Benki Kuu ya Tanzania.

Akifafanua zaidi Biswalo alisema zoezi la urejeshaji wa fedha kwa washitakiwa 341 ambao hawajamaliza kutimiza makubalino linaendelea na makubaliano hayo yanapaswa kutekelezwa kama yalivyosajiliwa kwa amri ya mahakama, ambapo katika madai hayo Serikali inawadai washitakiwa wote kiasi cha Tsh Bilioni 32.

Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Augustine Mahiga alisema wakati umefika kwa Watanzania kunufaika kikamilifu na uwepo na rasilimali katika nchi yao ikiwemo madini ambayo katika miaka ya nyuma hayakuwa na usimamizi madhubuti, hivyo Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa rasilimali za nchi zinaleta manufaa endelevu kwa Taifa na wananchi wake.

Aidha Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango alisema zoezi la utaifishaji wa mali za uhalifu, ni dalili tosha kuwa Tanzania sio nchi maskini na hivyo hakuna sababu ya Serikali kwenda kukopa nje ya nchi na badala yake itaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha kuwa raslimali zake zitalindwa kwa nguvu zote hivyo kumtaka DPP na Waziri Biteko kutoogopa vitisho badala yake wawe tayari kufa kwaajili ya kulipigania Taifa. “kufa kwasababu ya kulipigania taifa ni heshima itakayokumbukwa siku zote kuliko kufa kwa aibu” alimaliza Waziri Mpango.


Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YAIPONGEZA WIZARA KWA UTEKELEZAJI WA MAMA SAMIA LEGAL AID CAMPAIGN

TUFANYE KAZI KWA UADILIFU NA USHIRIKIANO - MHE CHANA