Monday, March 30, 2020

OFISI ZA KATA KUTUMIKA KUSAJILI WATOTO CHINI YA UMRI WA MIAKA MITANO

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Amon Mpanju akitoa elimu ya namna ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa Korona kwa wananchi waliofika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma kusajili wa watoto walio chini ya Miaka Mitano unaofanywa na RITA.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Amon Mpanju akishuhudia zoezi la usajili wa watoto chini ya umri wa miaka mitano katika kituo cha usajili kilichopo katika Hospitali ya Misheni Peramiho Mkoa wa Ruvuma.

Baadhi ya Wazazi wakionesha vyeti vya kuzaliwa vya watoto wao walivyokabidhiwa na Naibu Katibu MKuu wa Katiba na Sheria Bw. Amon Mpanju baada ya kufanikiwa kuwasajili watoto wao.


XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini RITA umefanya maboresho ya mfumo wa usajili kuwezesha Vituo vya Afya pamoja ofisi za kata vitumike kuwasajili watoto na kupatiwa cheti cha kuzaliwa.

Hayo yameelezwa jana na Msajili wa Vizazi na Vifo na Mratibu wa zoezi la Usajili wa Watoto walio chini ya umri wa miaka mitano Mkoa wa Ruvuma Bwn Jonathan Magoti wakati akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya zoezi hilo mbele ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bwana Amon Mpanju aliyetembelea Mkoa wa Ruvuma kujionea maendeleo ya usajili wa watoto hao.

Bwn. Magoti alieleza kuwa wameshapeleka maboresho hayo katika mikoa 16 ukiwemo mkoa wa Ruvuma baada ya kupitishwa na Bunge na kurasmisha kuwa usajili unaweza kufanyika katika Ofisi za Kata na Vituo vya Afya kwa lengo la kuhakikisha huduma hizi zinafikika kiurahisi na wananchi.

“Hapo awali maboresho haya yalikuwa yakifanyika kwa kutumia Hati ya makubalinao baina ya Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Rais Tamisemi na Wizara ya Afya lakini sasa Bunge limeshapitisha na kurasimisha kuwa usajili unaweza kufanyika katika Ofisi za Kata na Vituo vya Afya baada ya kupitia marekebisho ya sheria mbambali Na.4 ya mwaka 2019” alisema Magoti.

Kwa upande wake Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu wa RITA Bi Emmy Hudson alisema kuwa maboresho ya ughatuaji wa mamlaka kutoka Serikali kuu kwenda Serikali za mitaa umerahisisha hatua za usajili kutoka hatua mbili hadi moja kwani hapo awali mtoto alipatiwa uthibitisho wa kizazi yaani tangazo na baadae kwenda ofisi ya mkuu wa wilaya kupata cheti lakini sasa mtoto hupatiwa cheti papo hapo na bila ya malipo.

“Uboreshwaji huu wa usajili wa watoto umesaidia Serikali na wadau mbalimbali kupata takwimu sahihi na kwa wakati ambazo zimekuwa zikitumika katika mipango ya maendeleo katika sekta mbalimbali nchini kama vile afya na elimu” alisisitiza Emmy Hudson.

Nae Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Amon Mpanju pamoja na kuupongeza uongozi wa RITA chini Mtenaji Mkuu wake Bi Emmy Hudson kwa kazi nzuri wanayofanya ya kupanua huduma ya usajili wa watoto chini ya umri wa miaka mitano kufikia mikoa 16 sasa, amewaasa kuendelea kuchukua tahadhari na kujikinga na ugonjwa wa Korona unaoitesa dunia kwa sasa.

“Ili tusikinzane na maelekezo ya serikali ya kujikinga na kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa Korona, lazima muhakikishe kwamba watu wanakuja kujisajili kwa awamu na kwa kupeana muda maalumu ili kuzuia milundikano ya watu, wazazi wafike kwenye vituo kwa kutofautiana muda na wakae mbali mbali muda wote wawapo katik vituo vya usjili”. Alisema Mpanju.

Aidha, Amon Mpanju aliongea na wazazi waliojitokeza katika vituo vyote alivyotembelea na kuwasisitiza kufuata maelekezo yote yanayotolewa na serikali juu ya namna ya kujikinga na kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa Korona popote watakapokuwa, ikiwa ni pamoja na kunawa mikono na sabuni kwa kutumia maji yanayotiririka, kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima pamoja na kuzingatia yote yanayoelezwa na serikali kupitia vyombo vya habari.

Usajili katika mkoa wa Ruvuma ulianza rasmi tarehe 20/03/2020 baada ya jumla ya watoa huduma 102 kupatiwa mafunzo ya ngazi ya taifa na mkoa na kula viapo vya uadilifu kuwa wanaenda kufanya kazi kwa nguvu na umakini wa hali ya juu kama walivyofundishwa. Mafunzo hayo yaliyoanza 09/03/2020 na kuhitimishwa tarehe 14/03/2020 mkoani Ruvuma yalilenga kuwaongezea uwezo maafisa hao ili waweze kutekeleza jukumu la usajili wa watoto kwa ufanisi ambapo kwa siku nne pekee wameweza kusajli watoto 37,544 kati ya watoto 242,000 sawa na asilimia 19.
Thursday, March 19, 2020

WATUMISHI WIZARA YA KATIBA NA SHERIA WAPATA ELIMU NAMNA YA KUJIKINGA NA VIRUSI VYA CORONA

Baadhi ya watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria wakiwasikiliza wataalam wa afya kutoka General hospital Mkoani Dodoma (hawapo pichani), walipofika kuwapa elimu kuhusu ugonjwa wa Corona. Wataalam hao waliwaeleza namna ugonjwa huo unavyoenezwa, jinsi ya kujikinga na hatua za kuchukua pale wanapomhisi mtu ameambukizwa virusi vya Corona.

Daktari Elam Lazaru Yango kutoka General Hospital Mkoani Dodoma (aliyesimama) akitoa elimu kuhusu virusi vya Corona kwa watumishi wa Wizara ya Katiba na sheria. 

Waziri wa Katiba na Sheria Mh. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akiuliza swali kwa wataalam wa afya kutoka General Hospital Mkoani Dodoma wakati wakitoa elimu kuhusu virusi vya Corona kwa watumishi wa Wizara ya Katiba na sheria.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Ndg. Amon Mpanju (mwenye miwani nyeusi) akiuliza swali kwa wataalam wa afya kutoka General Hospital Mkoani Dodoma wakati wakitoa elimu kuhusu virusi vya Corona kwa watumishi wa Wizara ya Katiba na sheria.

MAFUNZO YA SHERIA NCHINI YAENDANE NA KASI YA UCHUMI WA VIWANDA

Waziri wa Katiba na Sheria Mh Balozi Dkt Augustine Mahiga (pili kulia) akisalimiana na Makamu Mkuu (Taaluma)  wa chuo kikuu cha Tumaini Makumira Prof. Mbise katika ziara ya kutembelea vyuo vya sheria nchini.

Waziri wa Katiba na Sheria Mh Balozi Dkt Augustine Mahiga (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa chuo kikuu cha Mzumbe katika ziara ya kutembelea vyuo vya sheria nchini.
Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Prof Sifuni Mchome (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa chuo kikuu cha Iringa katika ziara ya kutembelea vyuo vinavyofundisha sheria nchini.


XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Vyuo vinavyotoa elimu ya Sheria nchini vimeshauriwa kutengeneza mitaala ya mafunzo ya sheria inayoendana na kasi ya maendeleo ya kiuchumi na viwanda yanayofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sasa ili kuongeza tija kiusimamizi na ulinzi wa miundombinu na maendeleo hayo kwa ustawi wa taifa na wananchi wake.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome katika ziara ya siku tatu ya kutembelea vyuo vya elimu ya juu vinavyofundisha Sheria inchini ambapo alitembelea Chuo Kikuu cha Iringa na Chuo Kikuu Katoliki cha Ruaha (Iringa), Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira (Arusha) pamoja na Chuo Kikuu Mzumbe, Chuo Kikuu Kishiriki cha Jordani na Chuo Kikuu cha Waislam vyote vya Morogoro.

Katika ziara hiyo Prof. Mchome alisema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi shupavu wa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, imefanya mageuzi ya kimaendeleo kwa kutekeleza miradi mikubwa inayochochea ukuaji wa uchumi nchini na yenye manufaa kwa wananchi akitolea mfano wa ujenzi unaoendelea wa Reli ya Kisasa (SGR) na Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JNHPP). Ni lazima elimu ya Sheria nchini ilenge kuwajenga wanasheria nchini katika muktadha wa kushiriki kulinda na kusimamia miundombinu inayojengwa na itakayojengwa ili kuleta tija maridhawa katika kuelekea uchumi wa kati na uchumi wa viwanda kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

“Hatuwezi kuendelea kufundisha sheria za makosa ya jinai (criminal law) pekee kana kwamba nchi hii ni ya wahalifu tu wakati ukweli uko wazi kuwa Serikali inatekeleza miradi mikubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, nishati, usafilishaji na uchukuzi kwa lengo la kuipeleka nchi kwenye chumi wa kati na wa viwanda. Lazima tubadilike sasa kwa kuwapika wataalamu wetu wa Sheria ili kushiriki katika kulinda na kusimamia miundombinu hii kisheria ikiwemo uandishi wa mikataba.”

Nae Kaimu Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Sheria kwa vitendo maarufu kama ‘Law School’ Dkt. Zakayo Lukumayi baada ya kuwasilisha mada iliyohusu maendeleo ya taaluma ya sheria nchini amesema kwamba wameamua kushiriki katika ziara ya kuvitembelea vyuo vinavyofundisha sheria kwaajili ya kutoa mrejesho wa hali ya taaluma ya sheria nchini kutokana na uzoefu wa kuwafundisha wanasheria wanaopita katika chuo hicho ili kwa pamoja waimarishe mfumo wa kufundisha wanasheria kwa lengo la kupata wataalamu bora wa sheria nchini kwa maslahi ya Taifa.

“Tumeona tutoe mrejesho wa hali halisi ya maendeleo ya taaluma ya sheria nchini kwa sasa ili tujue wapi tulipotoka, na tulipo ili tushauriane namna ya kuboresha mitaala yetu kwa lengo la kuendana na hali halisi ya mwelekeo wa nchi yetu kiuchumi. Tunataka tuwe washindani katika sekta zote za kimkakati ili kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais wetu wa Awamu ya Tano, Dkt. Magufuli”. Alisisitiza Dkt. Lukumay.

Kwa upande wake Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga aliyeambatana Katibu Mkuu Prof. Mchome, Naibu Katibu Mkuu, Bw. Amon Mpanju, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Sheria ‘Law School’ Dkt. Zakayo Lukumay pamoja na Mjumbe wa Baraza la Sheria nchini Dkt. Erasmo Nyika pamoja na pongezi aliwaeleza viongozi na wanafunzi wa vyuo hivyo kuwa nchi yoyote duniani haiwezi kupiga hatua kimaendeleo bila kuwa na sheria madhubuti zinazotungwa na kusimamiwa na wanasheria waliopikwa vizuri kuendana na wakati na mwelekeo wa taifa husika kiuchumi na kutenda haki kwa wakati, hivyo kuna haja kwa Taifa la Tanzania kuzalisha wanasheria watakaokidhi mahitaji ya sheria nchini sambamba na kasi ya maendeleo inayofanywa na Mhe Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.


Monday, March 16, 2020

KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA KAZI YA UJENZI WA MAHAKAMA NCHINI

Baadhi ya Mafundi wakiendelea na ujenzi wa jengo la ghorofa nne la Mahakama Kuu Kanda ya Arusha ambalo pia litatumika kama kituo jumuishi cha utoaji haki.


Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria wakipokea maelezo kuhusu kukamilika kwa ujenzi wa jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi-Manyara.


 Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (kulia) akizungumza jambo na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe. Emmanuel Mwakasaka wakati wa ziara ya Kamati hiyo ya kukagua ujenzi wa jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.


Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria wakikagua samani katika moja ya chumba cha Mahakama ya Wilaya ya Longido jijini Arusha.


XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria iliyoshirikisha viongozi wa juu wa Wizara ya Katiba na Sheria na Mahakama wamefanya ziara ya ukaguzi wa majengo yanayojengwa na Mahakama ya Tanzania katika Wilaya za Kondoa mkoani Dodoma, Babati mkoani Manyara, na Longido mkoani Arusha. Aidha, ukaguzi huo pia umefanyika katika majengo ya Mahakama Kuu ya jiji la Arusha na wiki kesho utaedelea katika Mkoa wa Morogoro.

Katika ziara hiyo, Kamati imeonesha kuridhishwa na kazi nzuri inayofanywa na Mahakama ya Tanzania katika maeneo yaliyotembelewa.

Akizungumza na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini wakati wa ziara hiyo Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Tabora mjini Mhe. Emmanuel Mwakasaka amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa uongozi wake mahili ambao ndiyo chachu ya ujenzi wa Mahakama nyingi nchini kwa sasa. Kondoa, Manyara, Longido ambazo zimekamilika ni mfano wa mahakama nyingi zilizojengwa na zinazoendelea kujengwa kwa kasi hapa Tanzania.

“Kwanza tumpongeze Mhe. Rais Dkt. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa uongozi wake madhubuti katika kuhakikisha kwamba haki inapatikana kwa haraka na kwa wakati. Kasi ya ujenzi wa majengo haya ya Mahakama ni wakupigiwa mfano, niwapongeze sana watendaji wote wa Mahakama”, amesema Mwakasaka.

Kwa upande wake, Mheshimiwa Balozi Dkt. Augustine Mahiga pamoja na kupongeza uzuri na ubora wa majengo ya Mahakama zote walizotembelea, alionesha kufurahishwa na uimara wa samani zilizowekwa katika Jengo la Mahakama ya Longido hivyo, kutoa rai kwa uongozi wa Mahakama kuzingatia utunzaji wa samani na majengo ya mahakama zote nchini hususani zilizojengwa  na zinazoendelea kujengwa.

“Hizi samani zilizowekwa katika Mahakama hii ni za kiwango cha juu na zimetengenezwa kwa mbao zilizozalishwa hapa nchini na waliotengeneza ni mafundi wazawa, hongereni sana watendaji wote mliohusika kutekeleza jambo hili,” amesema Balozi Mahiga.

Ziara hii ya Kamati ya Kudumu ya Bunge katika mikoa ya Dodoma, Manyara na Arusha imeendelea leo kwa kukagua ujenzi wa Jengo la ghorofa nne la Mahakama Kuu ya Kanda ya Arusha ambalo imeelezwa pia litatumika kama kituo jumuishi cha utoaji haki. Aidha, imethibitika kwamba majengo kama hili la Mahakama Kuu ya Kanda ya Arusha yatajengwa katika mikoa ya Dodoma, Mwanza, Dar es Salaam, Morogoro na Arusha yenyewe.