MAFUNZO YA SHERIA NCHINI YAENDANE NA KASI YA UCHUMI WA VIWANDA

Waziri wa Katiba na Sheria Mh Balozi Dkt Augustine Mahiga (pili kulia) akisalimiana na Makamu Mkuu (Taaluma)  wa chuo kikuu cha Tumaini Makumira Prof. Mbise katika ziara ya kutembelea vyuo vya sheria nchini.

Waziri wa Katiba na Sheria Mh Balozi Dkt Augustine Mahiga (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa chuo kikuu cha Mzumbe katika ziara ya kutembelea vyuo vya sheria nchini.
Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Prof Sifuni Mchome (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa chuo kikuu cha Iringa katika ziara ya kutembelea vyuo vinavyofundisha sheria nchini.


XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Vyuo vinavyotoa elimu ya Sheria nchini vimeshauriwa kutengeneza mitaala ya mafunzo ya sheria inayoendana na kasi ya maendeleo ya kiuchumi na viwanda yanayofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sasa ili kuongeza tija kiusimamizi na ulinzi wa miundombinu na maendeleo hayo kwa ustawi wa taifa na wananchi wake.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome katika ziara ya siku tatu ya kutembelea vyuo vya elimu ya juu vinavyofundisha Sheria inchini ambapo alitembelea Chuo Kikuu cha Iringa na Chuo Kikuu Katoliki cha Ruaha (Iringa), Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira (Arusha) pamoja na Chuo Kikuu Mzumbe, Chuo Kikuu Kishiriki cha Jordani na Chuo Kikuu cha Waislam vyote vya Morogoro.

Katika ziara hiyo Prof. Mchome alisema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi shupavu wa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, imefanya mageuzi ya kimaendeleo kwa kutekeleza miradi mikubwa inayochochea ukuaji wa uchumi nchini na yenye manufaa kwa wananchi akitolea mfano wa ujenzi unaoendelea wa Reli ya Kisasa (SGR) na Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JNHPP). Ni lazima elimu ya Sheria nchini ilenge kuwajenga wanasheria nchini katika muktadha wa kushiriki kulinda na kusimamia miundombinu inayojengwa na itakayojengwa ili kuleta tija maridhawa katika kuelekea uchumi wa kati na uchumi wa viwanda kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

“Hatuwezi kuendelea kufundisha sheria za makosa ya jinai (criminal law) pekee kana kwamba nchi hii ni ya wahalifu tu wakati ukweli uko wazi kuwa Serikali inatekeleza miradi mikubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, nishati, usafilishaji na uchukuzi kwa lengo la kuipeleka nchi kwenye chumi wa kati na wa viwanda. Lazima tubadilike sasa kwa kuwapika wataalamu wetu wa Sheria ili kushiriki katika kulinda na kusimamia miundombinu hii kisheria ikiwemo uandishi wa mikataba.”

Nae Kaimu Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Sheria kwa vitendo maarufu kama ‘Law School’ Dkt. Zakayo Lukumayi baada ya kuwasilisha mada iliyohusu maendeleo ya taaluma ya sheria nchini amesema kwamba wameamua kushiriki katika ziara ya kuvitembelea vyuo vinavyofundisha sheria kwaajili ya kutoa mrejesho wa hali ya taaluma ya sheria nchini kutokana na uzoefu wa kuwafundisha wanasheria wanaopita katika chuo hicho ili kwa pamoja waimarishe mfumo wa kufundisha wanasheria kwa lengo la kupata wataalamu bora wa sheria nchini kwa maslahi ya Taifa.

“Tumeona tutoe mrejesho wa hali halisi ya maendeleo ya taaluma ya sheria nchini kwa sasa ili tujue wapi tulipotoka, na tulipo ili tushauriane namna ya kuboresha mitaala yetu kwa lengo la kuendana na hali halisi ya mwelekeo wa nchi yetu kiuchumi. Tunataka tuwe washindani katika sekta zote za kimkakati ili kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais wetu wa Awamu ya Tano, Dkt. Magufuli”. Alisisitiza Dkt. Lukumay.

Kwa upande wake Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga aliyeambatana Katibu Mkuu Prof. Mchome, Naibu Katibu Mkuu, Bw. Amon Mpanju, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Sheria ‘Law School’ Dkt. Zakayo Lukumay pamoja na Mjumbe wa Baraza la Sheria nchini Dkt. Erasmo Nyika pamoja na pongezi aliwaeleza viongozi na wanafunzi wa vyuo hivyo kuwa nchi yoyote duniani haiwezi kupiga hatua kimaendeleo bila kuwa na sheria madhubuti zinazotungwa na kusimamiwa na wanasheria waliopikwa vizuri kuendana na wakati na mwelekeo wa taifa husika kiuchumi na kutenda haki kwa wakati, hivyo kuna haja kwa Taifa la Tanzania kuzalisha wanasheria watakaokidhi mahitaji ya sheria nchini sambamba na kasi ya maendeleo inayofanywa na Mhe Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.


Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YAIPONGEZA WIZARA KWA UTEKELEZAJI WA MAMA SAMIA LEGAL AID CAMPAIGN

TUFANYE KAZI KWA UADILIFU NA USHIRIKIANO - MHE CHANA