OFISI ZA KATA KUTUMIKA KUSAJILI WATOTO CHINI YA UMRI WA MIAKA MITANO
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bw.
Amon Mpanju akitoa elimu ya namna ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa
Korona kwa wananchi waliofika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma kusajili
wa watoto walio chini ya Miaka Mitano unaofanywa na RITA.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Amon
Mpanju akishuhudia zoezi la usajili wa watoto chini ya umri wa miaka mitano
katika kituo cha usajili kilichopo katika Hospitali ya Misheni Peramiho Mkoa wa
Ruvuma.
Baadhi ya Wazazi wakionesha vyeti vya kuzaliwa vya watoto
wao walivyokabidhiwa na Naibu Katibu MKuu wa Katiba na Sheria Bw. Amon Mpanju
baada ya kufanikiwa kuwasajili watoto wao.
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Wakala wa Usajili Ufilisi
na Udhamini RITA umefanya maboresho ya mfumo wa usajili kuwezesha Vituo vya Afya
pamoja ofisi za kata vitumike kuwasajili watoto na kupatiwa cheti cha kuzaliwa.
Hayo yameelezwa jana na Msajili
wa Vizazi na Vifo na Mratibu wa zoezi la Usajili wa Watoto walio chini ya umri
wa miaka mitano Mkoa wa Ruvuma Bwn Jonathan Magoti wakati akiwasilisha taarifa
ya maendeleo ya zoezi hilo mbele ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na
Sheria Bwana Amon Mpanju aliyetembelea Mkoa wa Ruvuma kujionea maendeleo ya
usajili wa watoto hao.
Bwn. Magoti alieleza kuwa
wameshapeleka maboresho hayo katika mikoa 16 ukiwemo mkoa wa Ruvuma baada ya
kupitishwa na Bunge na kurasmisha kuwa usajili unaweza kufanyika katika Ofisi
za Kata na Vituo vya Afya kwa lengo la kuhakikisha huduma hizi zinafikika
kiurahisi na wananchi.
“Hapo awali maboresho haya
yalikuwa yakifanyika kwa kutumia Hati ya makubalinao baina ya Wizara ya Katiba
na Sheria, Ofisi ya Rais Tamisemi na Wizara ya Afya lakini sasa Bunge
limeshapitisha na kurasimisha kuwa usajili unaweza kufanyika katika Ofisi za
Kata na Vituo vya Afya baada ya kupitia marekebisho ya sheria mbambali Na.4
ya mwaka 2019” alisema Magoti.
Kwa upande wake Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu wa RITA Bi
Emmy Hudson alisema kuwa maboresho ya ughatuaji wa mamlaka kutoka
Serikali kuu kwenda Serikali za mitaa umerahisisha hatua za usajili kutoka
hatua mbili hadi moja kwani hapo awali mtoto alipatiwa uthibitisho wa kizazi yaani
tangazo na baadae kwenda ofisi ya mkuu wa wilaya kupata cheti lakini sasa mtoto
hupatiwa cheti papo hapo na bila ya malipo.
“Uboreshwaji huu wa usajili
wa watoto umesaidia Serikali na wadau mbalimbali kupata takwimu sahihi na kwa
wakati ambazo zimekuwa zikitumika katika mipango ya maendeleo katika sekta
mbalimbali nchini kama vile afya na elimu” alisisitiza Emmy Hudson.
Nae Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Amon Mpanju pamoja na kuupongeza uongozi wa RITA
chini Mtenaji Mkuu wake Bi Emmy Hudson kwa kazi nzuri wanayofanya ya kupanua
huduma ya usajili wa watoto chini ya umri wa miaka mitano kufikia mikoa 16
sasa, amewaasa kuendelea kuchukua tahadhari na kujikinga na ugonjwa wa Korona
unaoitesa dunia kwa sasa.
“Ili tusikinzane na
maelekezo ya serikali ya kujikinga na kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa Korona,
lazima muhakikishe kwamba watu wanakuja kujisajili kwa awamu na kwa kupeana
muda maalumu ili kuzuia milundikano ya watu, wazazi wafike kwenye vituo kwa
kutofautiana muda na wakae mbali mbali muda wote wawapo katik vituo vya
usjili”. Alisema Mpanju.
Aidha, Amon Mpanju aliongea
na wazazi waliojitokeza katika vituo vyote alivyotembelea na kuwasisitiza
kufuata maelekezo yote yanayotolewa na serikali juu ya namna ya kujikinga na
kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa Korona popote watakapokuwa, ikiwa ni pamoja na
kunawa mikono na sabuni kwa kutumia maji yanayotiririka, kuepuka mikusanyiko
isiyo ya lazima pamoja na kuzingatia yote yanayoelezwa na serikali kupitia
vyombo vya habari.
Usajili katika mkoa wa
Ruvuma ulianza rasmi tarehe 20/03/2020 baada ya jumla ya watoa huduma 102
kupatiwa mafunzo ya ngazi ya taifa na mkoa na kula viapo vya uadilifu kuwa
wanaenda kufanya kazi kwa nguvu na umakini wa hali ya juu kama walivyofundishwa.
Mafunzo hayo yaliyoanza 09/03/2020 na kuhitimishwa tarehe 14/03/2020 mkoani
Ruvuma yalilenga kuwaongezea uwezo maafisa hao ili waweze kutekeleza jukumu la
usajili wa watoto kwa ufanisi ambapo kwa siku nne pekee wameweza kusajli watoto
37,544 kati ya watoto 242,000 sawa na asilimia 19.
Comments
Post a Comment