Monday, April 20, 2020

UTEKELEZWAJI WA RIPOTI YA MFUMO WA UTATUZI WA MIGOGORO YA ARDHI WATAKIWA KUKAMILIKA MAPEMA

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (katikati) akipokea ripoti ya mfumo wa utatuzi wa migogoro ya ardhi kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Mhe. Jaji Mstaafu Januari Msoffe (kulia) wakati wa makabidhiano hayo katika ofisi za Wizara hiyo, Mtumba, jijini Dodoma. Mwingine pichani ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Ndg. Casmir Kyuki.

 Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Mhe. Jaji Mstaafu Januari Msoffe (aliyesimama) akifafanua jambo mbele ya Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga wakati wa makabidhiano ya ripoti ya mfumo wa utatuzi wa migogoro ya ardhi.

 Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania baada ya makabidhiano ya ripoti ya mfumo wa utatuzi wa migogoro ya ardhi.


XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX


Utekelezwaji wa ripoti ya mfumo wa utatuzi wa migogoro ya ardhi watakiwa kukamilika mapema kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga wakati akipokea ripoti ya mfumo wa utatuzi wa migogoro ya ardhi kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, ofisini kwake Mtumba jijini Dodoma.
Waziri Mahiga amewataka wasaidizi wake waliopo Wizarani wahakikishe ripoti hiyo inafanyiwa kazi haraka na kupitia hatua zote stahiki na kukamilika kabla ya Serikali ya awamu ya tano haijamaliza muda wake.
Aidha, Waziri Mahiga aliwaahidi viongozi wa Tume kuwasaidia pale watakapohitaji msaada wowote kutoka wizarani, alisema “Tume ikihitaji msaada kutoka Wizarani ili kuboresha kazi zao wasisite kuwasiliana na Wizara”
Aliongeza, wananchi wamekuwa wakilalamikia sheria mbalimbali kupitwa na wakati hivyo Tume izitazame sheria hizo na kuzifanyia utafiti. Pia aliwapongeza watendaji wote wa Tume ya Kurekebisha sheria kwa kazi nzuri wanayofanya ya kuhakikisha sheria zilizopitwa na wakati zinafanyiwa utafiti.
Kwa upande wake wakati akikabidhi ripoti hiyo Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Jaji Mstaafu Januari Msoffe alisema kabla ya kuandaa ripoti hiyo Tume ilikusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali katika mikoa kadhaa nchini ikiwemo Mwanza, Shinyanga, Songwe, Dodoma, Kilimanjaro, Dar Es Salaam, Tanga, Mbeya na Iringa.
Alisema baada ya utafiti wao waligundua changamoto kadhaa katika kutatua migogoro ya ardhi ikiwemo idadi ndogo ya mabaraza ya ardhi, Mahakama kukosa rasilimali watu na vifaa, ugumu katika kufikika kwenye mabaraza ya ardhi na nyumba ya Wilaya, na kutokuwepo kwa muongozo katika utozaji ada kwenye mabaraza ya vijiji na kata kunakosababisha utozwaji wa ada kubwa kwa wananchi. Kutokana na changamoto hizo, Tume imependekeza Mabaraza ya ardhi na nyumba ya wilaya yafutwe na shughuli zake zihamishiwe Mahakama na Mabaraza ya vijiji na kata yabaki na jukumu la usuluhishi.Friday, April 3, 2020

WIZARA YA KATIBA YAENDELEA KUIKIJANISHA DODOMA

Mkurugenzi Msaidizi sehemu ya Utawala wa Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Edith Simtengu akipanda mti katika zoezi la upandaji miti katika viwanja vya Wizara hiyo Mtumba, Jijini Dodoma..

Watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria wakiendelea na zoezi la kukijanisha Dodoma kwa kupanda miti katika viwanja vya wizara hiyo.
Bi Joyce Mtuma (kushoto) na Bi. Agnes Mkawe ambao ni watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria wakiwa wamebeba mti kuupeleka kwenye shimo la kuupanda katika zoezi la upandaji miti lililofanyika leo (3/4/2020) katika viwanja vya wizara hiyo.

WATUMISHI WIZARA YA KATIBA WAPATA ELIMU YA KUJIKINGA NA VIRUSI VYA COVID19

Waziri wa Katiba na Sheria Mh. Dkt. Balozi Augustine Mahiga akifafanua jambo wakati watumishi wa Wizara hiyo wakipatiwa mafunzo ya kujikinga na virusi vya Covid19 kutoka kwa wataalam wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto katika ofisi za Wizara hiyo Mtumba Jijini Dodoma.

Mtaalam wa Afya kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto akiwaonyesha namna sahihi ya kunawa mikono watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria wakati akiwapatia mafunzo ya kujikinga na virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Corona.