UTEKELEZWAJI WA RIPOTI YA MFUMO WA UTATUZI WA MIGOGORO YA ARDHI WATAKIWA KUKAMILIKA MAPEMA
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (katikati) akipokea ripoti ya mfumo wa utatuzi wa migogoro ya ardhi kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Mhe. Jaji Mstaafu Januari Msoffe (kulia) wakati wa makabidhiano hayo katika ofisi za Wizara hiyo, Mtumba, jijini Dodoma. Mwingine pichani ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Ndg. Casmir Kyuki.
Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Mhe. Jaji Mstaafu Januari Msoffe (aliyesimama) akifafanua jambo mbele ya Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga wakati wa makabidhiano ya ripoti ya mfumo wa utatuzi wa migogoro ya ardhi.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania baada ya makabidhiano ya ripoti ya mfumo wa utatuzi wa migogoro ya ardhi.
Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Mhe. Jaji Mstaafu Januari Msoffe (aliyesimama) akifafanua jambo mbele ya Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga wakati wa makabidhiano ya ripoti ya mfumo wa utatuzi wa migogoro ya ardhi.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania baada ya makabidhiano ya ripoti ya mfumo wa utatuzi wa migogoro ya ardhi.
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Utekelezwaji wa ripoti ya mfumo wa utatuzi wa
migogoro ya ardhi watakiwa kukamilika mapema kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Rais na
Wabunge.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.
Balozi Dkt. Augustine Mahiga wakati akipokea ripoti ya mfumo wa utatuzi wa
migogoro ya ardhi kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, ofisini kwake Mtumba
jijini Dodoma.
Waziri Mahiga amewataka wasaidizi wake waliopo
Wizarani wahakikishe ripoti hiyo inafanyiwa kazi haraka na kupitia hatua zote
stahiki na kukamilika kabla ya Serikali ya awamu ya tano haijamaliza muda wake.
Aidha, Waziri Mahiga aliwaahidi viongozi wa Tume
kuwasaidia pale watakapohitaji msaada wowote kutoka wizarani, alisema “Tume
ikihitaji msaada kutoka Wizarani ili kuboresha kazi zao wasisite kuwasiliana na
Wizara”
Aliongeza, wananchi wamekuwa wakilalamikia sheria mbalimbali
kupitwa na wakati hivyo Tume izitazame sheria hizo na kuzifanyia utafiti. Pia aliwapongeza
watendaji wote wa Tume ya Kurekebisha sheria kwa kazi nzuri wanayofanya ya
kuhakikisha sheria zilizopitwa na wakati zinafanyiwa utafiti.
Kwa upande wake wakati akikabidhi ripoti hiyo Mwenyekiti
wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Jaji Mstaafu Januari Msoffe alisema
kabla ya kuandaa ripoti hiyo Tume ilikusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali
katika mikoa kadhaa nchini ikiwemo Mwanza, Shinyanga, Songwe, Dodoma,
Kilimanjaro, Dar Es Salaam, Tanga, Mbeya na Iringa.
Alisema baada ya utafiti wao waligundua changamoto
kadhaa katika kutatua migogoro ya ardhi ikiwemo idadi ndogo ya mabaraza ya
ardhi, Mahakama kukosa rasilimali watu na vifaa, ugumu katika kufikika kwenye
mabaraza ya ardhi na nyumba ya Wilaya, na kutokuwepo kwa muongozo katika
utozaji ada kwenye mabaraza ya vijiji na kata kunakosababisha utozwaji wa ada
kubwa kwa wananchi. Kutokana na changamoto hizo, Tume imependekeza Mabaraza ya
ardhi na nyumba ya wilaya yafutwe na shughuli zake zihamishiwe Mahakama na
Mabaraza ya vijiji na kata yabaki na jukumu la usuluhishi.
Comments
Post a Comment