Thursday, June 25, 2020

MPANJU ATAKA VIPAUMBELE VYA MSINGI VIIBULIWE KATIKA MPANGO KAZI WA PILI WA HAKI ZA BINADAMU

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Ndg. Amon Mpanju akifungua kikao cha siku mbili cha wataalam wa Kikosi kazi cha kupitia rasimu ya mpango kazi wa pili wa haki za binadamu kinachofanyika jijini Dodoma.Wengine pichani kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Haki za Binadamu Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Nkasori Sarakikya na kushoto ni  Afisa Mchunguzi Mkuu na Mratibu wa Mpango kazi wa kwanza wa haki za binadamu Bw. Laurent Buliro kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

Wataalam wa kikosi kazi cha kupitia rasimu ya mpango kazi wa pili wa haki za binadamu wakimsikiliza mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Ndg. Amon Mpanju (hayupo pichani) wakati akifungua kikao cha kupitia rasimu hiyo.

Mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Ndg. Amon Mpanju akiwa katika picha ya pamoja na Wataalam wa kikosi kazi cha kupitia rasimu ya mpango kazi wa pili wa haki za binadamu baada ya kufungua kikao chao.

XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Ndg. Amon Mpanju akitaka kikosi kazi cha wataalam kutoka Wizara na Taasisi za Serikali zinazopitia rasimu ya Mpango kazi wa pili wa haki za binadamu kuibua vipaumbele vya msingi ambavyo vimekosekana katika mpango kazi wa kwanza ulioishia 2017.

“Mpango kazi wa kwanza ulioanza 2013 na kuishia 2017 haukuzingatia vipaumbele hivyo mpango kazi huu wa pili ulete vipaumbele vya msingi”.

Naibu Katibu Mkuu  aliyasema hayo wakati akifungua kikao kazi hicho cha siku mbili kinachofanyika jijini Dodoma.

Aliongeza, kazi hii ya kupitia rasimu ya mpango kazi wa pili wa haki za binadamu ni muhimu kuifanya kwa umakini kwani inatoa muongozo wa kisera katika kusimamia masuala ya haki za binadamu na pia hauji kuwa mbadala wa mambo mengine ya haki za binadamu.

Mpanju aliwasisitiza wataalam hao kuwa mpango kazi huu uzingatie haki za kiraia, kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni, kijamii, kimaendeleo na makundi maalum mfano wakulima na walemavu.

Aliongeza, mpango kazi wa pili wa haki za binadamu ni kipaumbele cha Serikali na utakuwa mwongozo wa kisera wa kukuza na kulinda haki za binadamu nchini na hivyo alisisitiza kuwa kila taasisi ihakikishe kwamba vipaumbele katika sekta zao zimo katika mpango kazi huu ili kuufanya uwe bora zaidi kwani mpango kazi wa haki za binadamu wa kwanza japokuwa ulipata mafanikio kadhaa lakini haukuzingatia vipaumbele.

Aliwasihi wataalam hao kufanya kazi kwa weledi na kwa kujituma na kutambua kwamba zoezi hili ni nyeti na ni la muhimu alisema, “nawasihi kutoa ushirikiano, kufanya kazi kwa weledi, kwa kujituma na kutambua kwamba zoezi hili ni nyeti na ni la umuhimu kwa kuwa ni mfumo wakuhakikisha Serikali inatimiza wajibu wake wa kukuza na kulinda haki za binadamu kwa wananchi wake.

Aidha, alizitaka asasi zisizo za Serikali kuweka mfumo mzuri wa kufuatilia masuala ya haki za binadamu katika Halmashauri hadi Serikali kuu na kutatua changamoto zilizokuwepo kwenye mpango kazi wa kwanza wa haki za binadamu. Kabla ya kuandaliwa kwa rasimu hii ya mpango kazi wa pili wa haki za binadamu maoni mbalimbali yalikusanywa kutoka kwa wadau katika mikoa mbalimbali Tanzania Bara na Visiwani na hivyo Naibu Katibu Mkuu alikitaka kikosi kazi hicho kuweka vizuri mawazo hayo kutoka kwa wananchi ili kupata mpango kazi ulio mzuri kwa Taifa.

Kikosi kazi hiki cha wataalam kimeundwa ili kupitia muongozo wa kisera unaolenga kutatua changamoto mbalimbali zilizojitokeza kwenye mpango kazi wa kwanza ambao ulikosa vipaumbele vya msingi.Tuesday, June 23, 2020

WIZARA YA KATIBA NA SHERIA YAADHIMISHA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Deogratias Yinza akiongea na watumishi wa Wizara hiyo katika kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoadhimishwa kila mwaka kuanzia tarehe 16 hadi 23, Juni. Katika maadhimisho hayo watumishi hao walikumbushwa kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali inayopaswa kufuatwa na watumishi wa Umma. Kauli mbiu ya mwaka huu ni " Jukumu la utumishi wa Umma katika kujenga na kudumisha amani iliyopo miongoni mwa jamii".

Baadhi ya Watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria wakimsikiliza Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara hiyo Bw. Deogratias Yinza (hayupo pichani) katika kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma.

Afisa Rasilimali Watu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Hilda Makwinya (mwenye kilemba) akiongea na watumishi wa Wizara hiyo katika kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma.

Wednesday, June 17, 2020

RAIS MAGUFULI AIPONGEZA SEKTA YA SHERIA
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Magufuli aipongeza sekta ya sheria kwa mafanikio iliyoyapata katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Pongezi hizo amezitoa katika hotuba yake ya kufunga Bunge la 11, alisema katika kipindi hicho sekta ya sheria imejitahidi kupunguza vitendo vya rushwa, ucheleweshaji na ubambikaji wa kesi pamoja na mlundikano wa wafungwa . Alisema “ Ili kukabiliana na tatizo la ucheleweshaji wa kesi Serikali iliteua Majaji wapya 17 wa Mahakama ya Rufani, Majaji 52 wa Mahakama Kuu na kuajiri watumishi wa mahakama 859, wakiwemo mahakimu 396”.

Aidha, Katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya awamu ya tano Mahakama kadhaa zilijengwa na nyingine kukarabatiwa na mahakama inayotembea ilianzishwa katika mikoa ya Dar es salaam na Mwanza, hadi kufikia mwezi wa tatu 2020 ilikuwa imeshasajili mashauri 337 na kusikiliza mashauri 274 hizi zote zikiwa ni jitihada za kupunguza  mlundikano wa kesi.

Rais Magufuli aliongeza kuwa katika kukabiliana na tatizo la ucheleweshwaji wa kesi alitia saii hati ya kuimarisha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na kuanzishwa kwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, alisema “uwekaji saini hati hiyo umeongeza tija na kuleta ufanisi mkubwa katika usimamizi na uendeshaji wa mashauri Mahakamani na pia kwenye Mabaraza ya usuluhishi ndani na nje ya nchi.”

Vilevile alisema, Wafungwa 42,774 waliokuwa wakitumikia vifungo mbalimbali walisamehewa na mahabusu 2812 walifutiwa kesi ili kupunguza mlundikano magerezani.

Wakati huohuo, Rais Magufuli alisema mageuzi makubwa yamefanyika kwenye sekta ya madini ambapo Mwezi Julai 2017 sheria ya kulinda Rasilimali za Taifa ikiwemo madini ilipitishwa alisema, “Nashukuru kupitisha sheria hii muhimu sana kwa taifa letu. Kwa hakika mmeingia kwenye vitabu vya historia ya nchi yetu na vizazi vitawakumbuka”

Aliongeza, Kupitishwa kwa sheria hiyo kumewezesha kwa mara ya kwanza Watanzania kumiliki rasilimali zao kwa nguvu za kisheria. Na sheria hiyo pia ndiyo imefanikisha kuanzishwa kwa kampuni ya Twiga Minerals Company ambayo Serikali inamiliki hisa 16% na Barrick 84%. Kadhalika imesaidia kutolewa kwa malipo ya fidia ya dola milioni 100 kati ya dola million 300 ambazo kampuni ya Barrick ilikubali kulipa.

Katika hotuba yake Rais Magufuli alimshukuru Mh. Spika kwa kuunda Kamati maalum ya Bunge ya kuchunguza utoroshaji wa madini ya Tanzanite ambapo Kamati hiyo ilitoa ushauri wa kujenga ukuta wa Km 25 katika mgodi wa Mererani na  Serikali iliujenga kwa haraka sana.

Sekta ya Madini imeanza kukua kwa kasi ambapo 2019 iliongoza kwa ukuaji kwa 17.7% ikifuatiwa na ujenzi 14.1%.

Aliongeza, Mapato yatokanayo na madini nayo yameongezeka, mwaka 2018/2019  zilikusanywa bilioni 346 kutoka bilioni 194 mwaka 2016/17. Mwaka huu 2019/20 bilioni 470 zinatarajiwa kukusanywa ambapo mwezi Aprili 2020 pekee licha ya kuwepo kwa ugonjwa wa corona bilioni 58 zimekusanywa.

Alisema, haijawahi kutokea kabisa, kiwango cha juu kilichowahi kukusanywa kwa mwezi kilikuwa bilioni 43. Haya yametokana na kupitishwa kwa sheria hii.

Rais Magufuli alisema mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano ni matokeo ya ushirikiano miongoni mwa watanzania wote hivyo hakuna budi kuendelea kushirtikiana kwa lengo la kuiletea nchi maendeleo.