Thursday, July 30, 2020

WIZARA YA KATIBA YAENDELEA KUIKIJANISHA DODOMAMtumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Dina Njovu akisukuma toroli kupeleka miti kwenye mashimo ili iweze kupandwa. 

Mtumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Ernest Mbuna akimwagilia maji mti aliopanda katika zoezi la upandaji miti lililofanyika leo katika viwanja vya Wizara hiyo.  

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Deogratias Yinza akichimba shimo kwa ajili ya kupanda ua katika eneo linalozunguka ofisi za Wizara hiyo.

Watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria wakiwa katika zoezi la upandaji miti na maua katika eneo llinalozunguka ofisi hizo leo Mtumba jijini Dodoma.

XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Wizara ya Katiba na Sheria yaendelea kuikijanisha Dodoma kwa kupanda miti ya kivuli, matunda na maua katika viwanja  vya Wizara hiyo iliyopo Mtumba Mkoani Dodoma.

Zoezi hilo la upandaji miti limekuwa likifanyika mara kwa mara ili kuwezesha viwanja vya wizara hiyo kuwa na mazingira mazuri ya kuvutia.

Miti hiyo mbali na kuwapatia kivuli, watumishi watapata fursa ya kula matunda mbalimbali wakiwa kazini ikiwemo zabibu ambalo ni zao linalostawi sana mkoani Dodoma.

Aidha Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara hiyo Ndg. Deogratias Yinza amekuwa mstari wa mbele katka kuhamasisha upandaji wa miti  katika maeneo ya viwanja vya Wizara hiyo na hivyo kuwapa mwamko watumishi wa wizara hiyo wa kupanda miti ili kukabiliana na hali ya ukame iliyopo katika Mkoa wa Dodoma.

Zoezi hili la upandaji miti limejumuisha watumishi wote wa Wizara ya Katiba na Sheria.


Thursday, July 23, 2020

KATIBU MKUU KATIBA NA SHERIA AWATAKA POLISI, MAGEREZA KUHAKIKISHA HAKI ZA MTOTO ZINALINDWA NA KUHIFADHIWA

Katibu Mkuu Wizara ya katiba na Sheria, Prof. Sifuni Mchome (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Mafunzo ya siku nne kwa maafisa wa Jeshi la Polisi na Magereza kutoka katika mikoa ya Iringa na Mbeya kuhusu utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria kwa watoto jana katika ukumbi wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Mbeya- jijini


Washiriki wa Mafunzo ya siku nne kuhusu utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria kwa watoto jana katika ukumbi wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Mbeya- jijini
Katibu Mkuu Wizara ya katiba na Sheria, Prof. Sifuni Mchome akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mafunzo ya siku nne kwa maafisa wa Jeshi la Polisi na Magereza kutoka katika mikoa ya Iringa na Mbeya kuhusu utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria kwa watoto jana katika ukumbi wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Mbeya- jijini Mbeya.

XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

SERIKALI imewataka Polisi na Magereza nchini kuhakikisha haki na maslahi ya mtoto anayekinzana na sheria zinalindwa na kuhifadhiwa kwa kuhakikisha kuwa shauri linalomhusu linapewa kipaumbele na linashughulikiwa kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto Na. 21 ya 2009.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome wakati akifungua Mafunzo ya siku nne kwa maafisa wa Jeshi la Polisi na Magereza kutoka katika mikoa ya Iringa na Mbeya kuhusu utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria kwa watoto jana katika ukumbi wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Mbeya- jijini Mbeya.

Prof. Mchome amesema Wizara kwa kushirikiana na wadau, kama vile UNICEF na wengine, imeendelea kuzingatia maslahi ya mtoto anayekinzana na sheria kwa kuhakikisha kuwa shauri linalomhusu linapewa kipaumbele na linashughulikiwa kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto.

“Ni rai yangu kuwa mnapokabiliana na kesi za watoto hakikisheni mtoto anapata msaada wa kisheria mara unapokutana naye au kusikia habari zake. Kwa kuwa mtakutana na watoto wa namna hii, ninaomba mafunzo haya yawakumbushe wajibu wenu katika kumhudumia mtoto huyu ili haki itendeke kwa wakati.”

Hivi karibuni, Mhe. Jaji Mkuu alitoa Kanuni za ushughulikiaji wa mashauri yanayohusu watu wenye mahitaji maalum, wakiwamo watoto. Kanuni hizo zinaweka masharti ya kuhakikisha upelelezi, uendeshaji na utoaji wa hukumu kwa mashauri ya watoto unafanyika kwa wakati kutokana na changamoto zilizopo katika mashauri hayo amesisitiza Prof. Mchome.

Aidha, Prof. Sifuni Mchome ametaja hatua za zilizochukuliwa na Serikali katika kuboresha mfumo wa haki jinai kuwa ni marekebisho ya sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20 kwa kuweka utaratibu wa kufifisha makosa na kuimarisha mfumo wa upatanishi katika makosa ya jinai kwa lengo la kupunguza mrundikano wa mashauri Mahakamani na kuondoa msongamano wa mahabusu na wafungwa katika vituo vya polisi na magereza, hivyo kuwataka mafisa wa polisi na Magereza kuzitumia njia hizo.

“Ninyi mnaopatiwa mafunzo haya mnapaswa kuwa mabalozi kuonesha mfano kwa kuzitumia njia hizi kwani zipo kwa mujibu wa sheria kuwezesha mfumo huo kufanya kazi kwa mujibu wa Sheria. Kutokana na Wizara yangu kusimamia masuala ya utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria na mfumo wa haki jinai, ni imani yetu kuwa, kama wadau wakubwa, mtaitumia fursa hii kujitathimini na kushiriki kujenga mfumo wa utoaji haki wenye tija usio na malalamiko kwa wananchi.”

Akiwashukuru UNICEF kwa jitihada kubwa wanazofanya katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha haki za mtoto zinalindwa na kuhifadhiwa Prof. Mchome amesema Serikali imejipanga kuhakikisha inatatua changamoto zinazomkabili mtoto anayekinzana na sheria katika maeneo mbalimbali nchini. Aidha, Wizara ya Katiba na Sheria, kwa kushirikiana na UNICEF pamoja na wadau wa haki mtoto,  imeandaa Mkakati wa Haki Mtoto ambao hivi karibuni utazinduliwa. Mkakati huu unalenga kuhakikisha kuwa wadau wa masuala ya mtoto wanafanya kazi kwa pamoja katika kusimamia masuala ya haki mtoto.

“Moja ya wadau wakubwa katika mkakati huu ni Jeshi la Polisi na Magereza ambapo jukumu lenu ni kubwa mno katika masuala ya haki mtoto. Mkakati huu unawalenga watoto wote walioathirika na ukatili wa kijinsia, waliotenda makosa au kujikuta kizuizini kutokana na mzazi kutenda kosa.”
Ni wazi kwamba Mkakati huu kitakuwa chombo kinachoaminika na sehemu salama kwa mtoto tofauti na ilivyo sasa ambapo kumekuwa na malalamiko ya watoto kupewa umri mkubwa tofauti na uhalisia, amesisitiza Prof. Mchome.

“Ni rai yangu kwamba Wadau wote tutashirikiana katika kuhakikisha ulinzi na ustawi wa mtoto linakuwa ni jukumu letu la msingi. Hivyo, nawahimiza kwa mara nyingine kujaribu kutumia njia mbadala za kushughulikia masuala yanayohusu haki za mtoto badala ya kujielekeza katika kuwaweka vituoni au magereza jambo linalosababisha msongamano.”

Mwaka 2017 Wizara ya Katiba na Sheria ilisimamia mchakato wa kutunga na kupatikana kwa sheria ya Msaada wa Kisheria Na 1 ya 2017. Pamoja na mambo mengine, Sheria hiyo ina lengo la kutoa huduma ya msaada wa kisheria kwa watu wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za Mawakili. Aidha, sheria hii imeweka masharti ya kutoa msaada wa kisheria katika mashauri ya jinai. Ni kwa muktadha huo, Wizara ya Katiba na Sheria iliingia makubaliano na Wizara ya Mambo ya Ndani mwaka 2018 kuhusu utekelezaji wa masuala ya msaada wa kisheria katika vituo vya Polisi na magereza nchini.

Tuesday, July 14, 2020

WAZIRI DKT. MWIGULU NCHEMBA AWASILISHA TAARIFA KATIKA KIKAO CHA 66 CHA TUME YA AFRIKA YA HAKI ZA BINADAMU NA WATU


XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba amewasilisha taarifa juu ya Haki za Binadamu na za Watu Barani Afrika na ugonjwa wa covid- 19 katika Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu.

Taarifa hii imewasilishwa kwa njia ya njia ya kikao cha mtandao (video conference) kwa washiriki waliopo Banjul, Gambia Julai 13, 2020.

Katika taarifa hiyo Waziri Nchemba amesema ugonjwa wa covid -19 sio tu ni janga la kiafya bali pia ni la kiuchumi na kijamii.

Katika kukabiliana na ugonjwa huu nchi ya Tanzania inakabiliana nao kwa kutofunga mipaka ya nchi na kuendelea na shughuli za uzalishaji mali huku wananchi wakipewa elimu na kusisitizwa kufuata njia za kujikinga na maambukizi ya virusi hivyo.

 Njia zinazotumika kukabiliana na covid-19 ni pamoja na kutumia dawa za asili katika kuimarisha kinga ya mwili na pia kujifukiza kwa kutumia  majani ya miti mbalimbali maarufu kama nyungu ili kupambana na ugonjwa huo.

Vilevile, Wananchi wameelimishwa kuondoa hofu mara wapatapo maambukizi ya virusi hivyo na badala yake kukabiliana navyo kwa kutumia dawa wanazoelekezwa na wataalam wa afya, na pia kuepuka misongamano, kuosha mikono mara kwa mara, na kuvaa barakoa bila kusahau kumuomba Mungu kwa imani zao.

Serikali ina uelewa wa kutosha juu ya hatari ya virusi vya covid-19 na umuhimu wa kuchukua tahadhari na tumejiridhisha na njia tulizochukua katika kukabiliana nao.

Ugonjwa huo ulipogundulika Tanzania kwa mara ya kwanza tarehe 16 Machi, 2020 Serikali ilichukua hatua za haraka kuwaelimisha wananchi kutotembelea nchi zilizoathirika, kujiweka karantini kwa siku 14 kwa wasafiri wote waingiapo nchini, kusitisha sherehe za kitaifa ikiwemo maadhimisho ya siku ya Muungano, kufunga shule na vyuo na kisitisha michezo mbalimbali ilim kupunguza maambukizi zaidi.

Aidha, Wizara ya afya imekuwa ikitoa elimu ya kujikinga na ugonjwa huo kwa taasisi mbalimbali za Serikali na elimu zaidi iliendelea kutolewa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na vipeperushi.

Waziri Nchemba alisema sekta ya afya imepanga mikakati mbalimbali katika kukabiliana na ugonjwa wa covid-19 ikiwemo kupeleka mahitaji  ya muhimu kwa watoa huduma za afya, kuongeza idadi ya madaktari na watoa huduma za afya, ushauri ulitolewa kwa wananchi kuhusu kutumia dawa za asili na sio kutegemea dawa za kisasa pekee na pia taasisi za utafiti wa dawa asilia zimeimarishwa.

Vilevile aliongeza kuwa Serikali imefungua maabara mpya yenye mashine 5 zenye uwezo wa kupima sampuli 1,800 kwa siku ambapo wahudumu 1,000 wa afya walipata ajira katika maabara hizo.

Aidha, Serikali imemuagiza Wakala wa Ugavi wa maji na usafi wa mazingira kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuhakikisha maji yanapatikana na kuweka vifaa vya kunawia mikono maeneo mbalimbali.

Mbali na hayo,upatikanaji wa haki umeendelea kuzingatiwa katika kipindi cha mlipuko wa ugonjwa wa covid-19. Wafungwa na mahabusu kadhaa waliachiwa ili kupunguza msongamano magarezani na kamati za afya za mikoa na wilaya  zilianzishwa ili kukabiliana na ugonjwa huo magerezani.

Katika taarifa hiyo Waziri Nchemba amesema Kwa sasa Tanzania imeanza kurudi katika maisha ya kawaida ambapo shule, vyuo, shughuli za utalii na michezo imefunguliwa huku wananchi wakiendelea kusisitizwa kuchukua tahadhari za kujikinga na covid-19.

Thursday, July 9, 2020

NAIBU KATIBU MKUU AKAGUA HUDUMA ZA ZA UTOAJI MSAADA WA KISHERIA MKOANI TABORA


Viongozi mbalimbali wakimpokea Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Sheria na Katiba Amon Mpanju (katikati)  kwa ajili ya kuhudhuria hafla fupi ya uzinduzi wa Kamati ya Uratibu wa Huduma ya Msaada wa Kisheria kwa ngazi ya Mkoa wa Tabora jana
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Sheria na Katiba Amon Mpanju (kushoto) akibadilishana mawazo na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Tabora (Utumishi na Utawala) Hamis Mkunga (kulia)  wakati wa  hafla fupi ya uzinduzi Kamati ya Uratibu wa Huduma ya Msaada wa Kisheria kwa ngazi ya Mkoa wa Tabora jana.Msajili Msaidizi wa Kamati ya Uratibu wa Huduma ya Msaada wa Kisheria kwa ngazi ya Mkoa (LAPS) Mkoa wa Tabora Panin Kerika akiwasilisha taarifa fupi ya hali ya utoaji wa msaada wa kisheria wakati wa  hafla fupi ya uzinduzi Kamati ya Uratibu wa Huduma ya Msaada wa Kisheria kwa ngazi ya Mkoa wa Tabora jana


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Sheria na Katiba Amon Mpanju (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Uratibu wa Huduma ya Msaada wa Kisheria kwa ngazi ya Mkoa wa Tabora mara baada  ya uzinduzi wa Kamati hiyo jana

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Sheria na Katiba Amon Mpanju akitoa nahasa zake wakati wa uzinduzi wa Kamati ya Uratibu wa Huduma ya Msaada wa Kisheria kwa ngazi ya Mkoa wa Tabora jana

SERIKALI KUFUTA ADA YA USAJILI KWA WATOA HUDUMA YA MSAADA WA KISHERIA


Serikali inafanyia kazi wazo la kufuta ada ya usajili kwa watoa huduma ya  msaada wa kisheria ili kuhakikisha huduma hiyo inawafikia  wananchi wanyonge na kwa wakati mahali katika maeneo wanayoishi.

Kauli hiyo imetolewa jana Mkoani Tabora na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Amon Mpanju wakati akizindua Kamati ya Uratibu wa Huduma ya Msaada wa Kisheria kwa ngazi ya Mkoa.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha huduma ya msaada wa kisheria inawafikia wananchi wanyonge kwa wakati ili muda mwingi ambao wangeutumia kuhangaika na kesi wautumie katika shughuli za uzalishaji mali na kukuza uchumi wao na wa taifa kwa ujumla.

Pamoja na wazo hilo ni  lazima watoa huduma hao  wakaendelea kuzingatia taratibu nyingine zilizoanishwa katika Sheria na kanuni ili waweze kuwafikia wananchi wanyonge; alisisitiza Mpanju.
“Ni vema watoa Huduma ya Msaada wa Kisheria wakasaidia kutatua kwa haraka migogoro ya wananchi wanyonge ili watumie muda mwingi katika uzalishaji badala ya kuwa Mahakamani.”

Alisisitiza kuwa Watoa huduma za Msaada wa Kisheria na Wasaidizi wa Msaada wa Kisheria ni sawa na viongozi wa dini ambao hutoa huduma kwa wananchi wanyonge bila malipo; hivyo, watoa huduma hawa wawasaidie watanzania ambao hawana uwezo kulipa gharama za Mawakili katika kuifikia haki.

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Tabora (Utumishi na Utawala) Hamis Mkunga alisema kuzinduliwa kwa Kamati hiyo kutasaidia kutatua migogoro ambayo wakazi wa Mkoa huo wenye kipato duni wamekuwa wakikabiliana nayo.

Aliongeza kuwa wananchi wengi walikuwa wakipoteza haki zao katika mambo mbalimbali na kudhulumiwa mali zao kwasababu ya ukosefu wa fedha za kulipa Mawakili na wengine kwa sababu ya kuishi mbali na vyombo vya utoaji haki.

Msajiri Msaidizi (LAPS) Mkoa wa Tabora Panin Kerika alisema katika wiki ya Sheria ya Mwaka 2018/19 , Mkoa ulikuwa na jumla ya mashauri 358 ambayo yaliweza kusikilizwa.

Alisema kati ya hayo 181 yalihusu migogoro ya ardhi, 62 matunzo ya watoto, 58 masuala ya mirathi, ukatili wa kijinsia matatu, migogoro katika ndoa yalikuwa 21, madai 15, migogoro katika masuala ya kazi 8 na jinai 10.
Mwisho