SERIKALI KUFUTA ADA YA USAJILI KWA WATOA HUDUMA YA MSAADA WA KISHERIA


Serikali inafanyia kazi wazo la kufuta ada ya usajili kwa watoa huduma ya  msaada wa kisheria ili kuhakikisha huduma hiyo inawafikia  wananchi wanyonge na kwa wakati mahali katika maeneo wanayoishi.

Kauli hiyo imetolewa jana Mkoani Tabora na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Amon Mpanju wakati akizindua Kamati ya Uratibu wa Huduma ya Msaada wa Kisheria kwa ngazi ya Mkoa.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha huduma ya msaada wa kisheria inawafikia wananchi wanyonge kwa wakati ili muda mwingi ambao wangeutumia kuhangaika na kesi wautumie katika shughuli za uzalishaji mali na kukuza uchumi wao na wa taifa kwa ujumla.

Pamoja na wazo hilo ni  lazima watoa huduma hao  wakaendelea kuzingatia taratibu nyingine zilizoanishwa katika Sheria na kanuni ili waweze kuwafikia wananchi wanyonge; alisisitiza Mpanju.
“Ni vema watoa Huduma ya Msaada wa Kisheria wakasaidia kutatua kwa haraka migogoro ya wananchi wanyonge ili watumie muda mwingi katika uzalishaji badala ya kuwa Mahakamani.”

Alisisitiza kuwa Watoa huduma za Msaada wa Kisheria na Wasaidizi wa Msaada wa Kisheria ni sawa na viongozi wa dini ambao hutoa huduma kwa wananchi wanyonge bila malipo; hivyo, watoa huduma hawa wawasaidie watanzania ambao hawana uwezo kulipa gharama za Mawakili katika kuifikia haki.

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Tabora (Utumishi na Utawala) Hamis Mkunga alisema kuzinduliwa kwa Kamati hiyo kutasaidia kutatua migogoro ambayo wakazi wa Mkoa huo wenye kipato duni wamekuwa wakikabiliana nayo.

Aliongeza kuwa wananchi wengi walikuwa wakipoteza haki zao katika mambo mbalimbali na kudhulumiwa mali zao kwasababu ya ukosefu wa fedha za kulipa Mawakili na wengine kwa sababu ya kuishi mbali na vyombo vya utoaji haki.

Msajiri Msaidizi (LAPS) Mkoa wa Tabora Panin Kerika alisema katika wiki ya Sheria ya Mwaka 2018/19 , Mkoa ulikuwa na jumla ya mashauri 358 ambayo yaliweza kusikilizwa.

Alisema kati ya hayo 181 yalihusu migogoro ya ardhi, 62 matunzo ya watoto, 58 masuala ya mirathi, ukatili wa kijinsia matatu, migogoro katika ndoa yalikuwa 21, madai 15, migogoro katika masuala ya kazi 8 na jinai 10.
Mwisho



Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YAIPONGEZA WIZARA KWA UTEKELEZAJI WA MAMA SAMIA LEGAL AID CAMPAIGN

TUFANYE KAZI KWA UADILIFU NA USHIRIKIANO - MHE CHANA