WAZIRI DKT. MWIGULU NCHEMBA AWASILISHA TAARIFA KATIKA KIKAO CHA 66 CHA TUME YA AFRIKA YA HAKI ZA BINADAMU NA WATU
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba amewasilisha
taarifa juu ya Haki za Binadamu na za Watu Barani Afrika na ugonjwa wa covid-
19 katika Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu.
Taarifa hii imewasilishwa kwa njia ya njia ya kikao cha
mtandao (video conference) kwa washiriki waliopo Banjul, Gambia Julai 13, 2020.
Katika taarifa hiyo Waziri Nchemba amesema ugonjwa wa covid
-19 sio tu ni janga la kiafya bali pia ni la kiuchumi na kijamii.
Katika kukabiliana na ugonjwa huu nchi ya Tanzania inakabiliana
nao kwa kutofunga mipaka ya nchi na kuendelea na shughuli za uzalishaji mali
huku wananchi wakipewa elimu na kusisitizwa kufuata njia za kujikinga na
maambukizi ya virusi hivyo.
Njia zinazotumika
kukabiliana na covid-19 ni pamoja na kutumia dawa za asili katika kuimarisha
kinga ya mwili na pia kujifukiza kwa kutumia
majani ya miti mbalimbali maarufu kama nyungu ili kupambana na ugonjwa
huo.
Vilevile, Wananchi wameelimishwa kuondoa hofu mara wapatapo
maambukizi ya virusi hivyo na badala yake kukabiliana navyo kwa kutumia dawa
wanazoelekezwa na wataalam wa afya, na pia kuepuka misongamano, kuosha mikono
mara kwa mara, na kuvaa barakoa bila kusahau kumuomba Mungu kwa imani zao.
Serikali ina uelewa wa kutosha juu ya hatari ya virusi vya
covid-19 na umuhimu wa kuchukua tahadhari na tumejiridhisha na njia
tulizochukua katika kukabiliana nao.
Ugonjwa huo ulipogundulika Tanzania kwa mara ya kwanza
tarehe 16 Machi, 2020 Serikali ilichukua hatua za haraka kuwaelimisha wananchi
kutotembelea nchi zilizoathirika, kujiweka karantini kwa siku 14 kwa wasafiri
wote waingiapo nchini, kusitisha sherehe za kitaifa ikiwemo maadhimisho ya siku
ya Muungano, kufunga shule na vyuo na kisitisha michezo mbalimbali ilim
kupunguza maambukizi zaidi.
Aidha, Wizara ya afya imekuwa ikitoa elimu ya kujikinga na
ugonjwa huo kwa taasisi mbalimbali za Serikali na elimu zaidi iliendelea
kutolewa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na
vipeperushi.
Waziri Nchemba alisema sekta ya afya imepanga mikakati
mbalimbali katika kukabiliana na ugonjwa wa covid-19 ikiwemo kupeleka mahitaji ya muhimu kwa watoa huduma za afya, kuongeza
idadi ya madaktari na watoa huduma za afya, ushauri ulitolewa kwa wananchi
kuhusu kutumia dawa za asili na sio kutegemea dawa za kisasa pekee na pia
taasisi za utafiti wa dawa asilia zimeimarishwa.
Vilevile aliongeza kuwa Serikali imefungua maabara mpya
yenye mashine 5 zenye uwezo wa kupima sampuli 1,800 kwa siku ambapo wahudumu
1,000 wa afya walipata ajira katika maabara hizo.
Aidha, Serikali imemuagiza Wakala wa Ugavi wa maji na usafi
wa mazingira kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuhakikisha maji
yanapatikana na kuweka vifaa vya kunawia mikono maeneo mbalimbali.
Mbali na hayo,upatikanaji wa haki umeendelea kuzingatiwa katika
kipindi cha mlipuko wa ugonjwa wa covid-19. Wafungwa na mahabusu kadhaa
waliachiwa ili kupunguza msongamano magarezani na kamati za afya za mikoa na
wilaya zilianzishwa ili kukabiliana na ugonjwa
huo magerezani.
Katika taarifa hiyo Waziri Nchemba amesema Kwa sasa Tanzania
imeanza kurudi katika maisha ya kawaida ambapo shule, vyuo, shughuli za utalii
na michezo imefunguliwa huku wananchi wakiendelea kusisitizwa kuchukua
tahadhari za kujikinga na covid-19.
Comments
Post a Comment