DKT. MWIGULU NCHEMBA ATEMBELEA OFISI YA WAKILI MKUU WA SERIKALI

 

Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Mwigulu Nchemba akifafanua jambo wakati akizungumza na Menejimenti ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, jijini Dar es Salaam.

Wakili Mkuu wa Serikali Bw. Gabriel Malata (kulia) akimkabidhi taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya ofisi yake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Ndg. Amon Mpanju (kushoto), jijini Dar es Salaam.


XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka watendaji wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kutekeleza majukumu yao kwa weledi ili kuhakikisha haki inapatikana kwa ajili ya maslahi ya Taifa.

Akizungumza na menejimenti ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali jijini Dar es Salaam alipofanya ziara ya kikazi katika ofisi hiyo Dkt. Nchemba amesema, hatapenda kuona uzembe unafanywa na mawakili wasomi wa serikali katika kusimamia haki.

“Mtendaji yoyote akifanya kosa ambalo litaleta madhara kwa taifa kupitia utendaji wake, atachukuliwa hatua za kisheria kwa kuwa atakuwa amehujumu uchumi” amesema Dkt. Nchemba.

Amesema, ni vizuri mawakili kuacha kufanya kazi kwa mazoea, badala yake kuendelea kulinda rasilimali za taifa kwa wivu mkubwa ili kuokoa mali za watanzania katika kutafuta haki.

 “Sitapenda kusikia jambo kubwa lenye maslahi kwa taifa linashindwa kufanikiwa katika kuhakikisha haki inapatikana kwani baadhi ya watu wamekuwa na tabia ya kuiba na kwenda kujificha katika kichaka cha sheria” amesema Dkt. Nchemba.

Hata hivyo, ameeleza kuwa anaamini watendaji wote wa Ofisi hiyo wataendelea kufanya kazi kwa uaminifu ikiwemo kutowaficha wahalifu.

Aidha, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Ndg. Amon Mpanju ameeleza kuwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa serikali ina umuhimu mkubwa katika kuhakikisha taifa linasonga mbele.

Ndg. Mpanju ameeleza kuwa baada ya matokeo ya uchaguzi mkuu, baadhi ya wagombea wamekuwa na tabia ya kupinga matokeo mahakamani kwa kuweka pingamizi, hivyo anatarajia kuona mawakili wasomi wanasimama kidete kuhakikisha haki inapatikana.

Kwa upande wake, Wakili Mkuu wa Serikali Bw. Gabriel Malata amesema kuwa ofisi yake ambayo imeanzishwa miaka miwili iliyopita imeweza kuokoa kiasi cha shilingi trilioni 11.4 katika uendeshaji wa mashauri ya madai ambayo yaliendeshwa ndani na nje ya nchi.

Amesema, ofisi yake inahakikisha inapata idadi ya mashauri yote ya madai yanayohusu serikali na mashirika ya umma ili kutambua mashauri yasiokuwa na tija pamoja na yenye maslahi kwa taifa.

Wakili Malata amesema Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali itaendelea kufanya kazi kwa weledi ili kuhakikisha taifa linasonga mbele.

 


Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YAIPONGEZA WIZARA KWA UTEKELEZAJI WA MAMA SAMIA LEGAL AID CAMPAIGN

TUFANYE KAZI KWA UADILIFU NA USHIRIKIANO - MHE CHANA