MAZUNGUMZO YA AMANI YATAJWA KUWA NJIA BORA NA SALAMA YA UTATUZI WA MIGOGORO NCHINI.
Mazungumzo ya amani ni muarobaini
uliothibitika kutumika kama tiba ya migogoro ya ardhi Mvomero Mkoani Morogoro.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero
Mhe. Albinus Mgonya wakati akitoa taarifa ya hali ya amani wilayani humo kwa
Kamati ya Kitaifa ya Ujenzi wa Amani na Kuzuia Mauaji ya Kimbari iliyofika
walayani kwake hivi karibuni.
Wakulima na wafugaji ni watanzania wanaoishi
pamoja na kushirikiana katika shughuli mbalimbali za kijamii, kisiasa na
kiuchumi katika maeneo wanaoishi na zaidi, wengi wao ni wakulima na ni wafugaji
kwa wakati mmoja hivyo njia ya mazungumzo ya amani imejipambanua kuwa tiba ya
utatuzi wa migogoro inayowakabili.
"Unajua, hawa wakulima na wafugaji
wanafahamiana kwasababu wanaishi pamoja, matumizi ya nguvu hususani vyombo vya
ulinzi na usalama isingekuwa muarobaini, badala yake kwa kuwakutanisha na
kuzungumza nao kumeonesha kuwa ni suluhisho la migogoro na ujenzi wa amani na
utulivu baina yao."
Kwa niaba ya wakulima na wafugaji ndugu
Moringe Kwinasei ameungana na Mkuu huyo wa Wilaya kwa kuthibitisha hali ya
uwepo wa utulivu na amani uliotokana na utatuzi wa migogoro kwa njia ya
mazungumzo ya amani na kuwataka wakulima na wafugaji kuacha tabia ya uchochezi
kwa kisingizio cha migogoro baina yao.
"Unajua sisi ni ndugu na wote
tunahitajiana katika mambo mengi ikiwemo mazao ya mifugo na mimea ambayo ndiyo
yanatugombanisha, tunagombana shambani baadae tunakaa hotelini tunakula
wali-nyama! sasa kwanini tuendelee kugombania mambo ambayo ni sehemu ya
mahitaji yetu muhimu? Ameongeza kwa kuuliza Martine Matingise.
Aidha, Mhe. Mgonya amesema Wilaya yake
imeanzisha programu ya michezo mbalimbali hasa mashindano ya mipira wa Miguu
kati ya Wakulima na wafugaji, mbinu hii imeonesha kuwa na tija katika
ujenzi wa amani katika Wilaya hiyo kwasababu michezo imewaleta wakulima na
wafugaji pamoja na kuishi kwa upendo.
"Nimeanzisha na kuhamisisha michezo mbalimbali
hasa mpira wa Miguu kati ya wakulima na wafugaji, na nimekuwa nikishiriki nao
katika michezo husika. Kwakweli njia hii pia imeonesha mafanikio makubwa katika
jitihada za Serikali katika ujenzi wa amani na kuzuia migogoro katika
jamii." Amemaliza Mhe. Mgonya.
Kamati hii imehitimisha ziara yake ya
utekelezaji wa majukumu muhimu ya Ujenzi wa Amani na Kuzuia Mauaji ya Kimbari
katika Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro baada ya kufanya kazi kama hiyo katika
Mikoa ya Arusha, Manyara na Rukwa.
Comments
Post a Comment