WIZARA YA KATIBA KUSHIRIKIANA NA UNDP KUJENGA UELEWA KWA WANANCHI JUU YA UTAJIRI WA ASILI NA RASILIMALI ASILIA
Wataalam kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) wakifuatilia majadiliano wakati wa kikao chao na Menejimenti ya Wizara ya Katiba na Sheria.
Mkurugenzi wa kitengo cha Uangalizi wa Utajiri wa Asili na Rasilimali Asilia cha Wizara ya Katiba na Sheria Bi Neema Mwanga akielezea jambo wakati wa kikao kati ya Menejimenti ya Wizara ya Katiba na Sheria na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).
Picha ya pamoja ya Menejimenti ya Wizara ya Katiba na Sheria na wataalam kutoka Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) baada ya kumaliza kikao chao.
Serikali kupitia Wizara ya
Katiba na Sheria yakubaliana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kujenga uelewa kwa wananchi juu
ya kulinda Utajiri wa Asili na Rasilimali Asilia za nchi.
Makubaliano hayo yamefikiwa katika kikao kati ya Menejimenti ya Wizara
ya Katiba na Sheria na Maafisa kutoka UNDP kilichofanyika wizarani hapo Mtumba,
jijini Dodoma.
Katika kikao hicho UNDP waliahidi kuandaa andiko ambalo ndilo
litakalokuwa muongozo wa namna ya kutoa elimu kwa wananchi waweze kulewa dhana
nzima ya utajiri wa asili na rasilimali asilia na namna ambavyo zinaweza
kuwaletea maendeleo kwa wao binafsi na nchi pia.
Bw. Godfrey Mulisa ambaye ni mtaalam kutoka UNDP alisema Shirika lao litasaidia
kuangalia ni namna gani watashirikiana kuongeza usimamizi wa utajiri wa asili
na rasilimali asilia na kuhakikisha faida inapatikana kwa watanzania.
“Kubwa la kuangalia ni kuongeza usimamizi na kuhakikisha faida
inapatikana kwa watanzania” alisema Bw. Godfrey
Naye Bi. Getrude kutoka kitengo cha mazingira kwenye shirika hilo
alisema UNDP itashirikiana na kitengo cha Uangalizi wa Utajiri wa Asili na
Rasilimali Asilia kilichopo wizarani hapo ili kukijengea uwezo kitengo hicho
kiweze kufuatilia rasilimali na utajiri uliopo Tanzania ili kuweza kuinua
uchumi wa nchi na wananchi kwani shirika hilo linaangalia sana maendeleo ya
watu.
Awali akielezea kuhusu jukumu ililonalo Wizara ya Katiba na Sheria la
kusimamia utajiri wa asili na rasilimali asilia Mkurugenzi wa Kitengo cha
Uangalizi wa Utajiri wa Asili na Rasilimali Asilia Bi. Neema Mwanga alisema
jukumu kubwa lililonalo ni kuangalia mifumo au mikataba iliyopo inahakikisha
inalinda rasilimali za Taifa.
Aliongeza kuwa kitengo hicho kilianzishwa mwaka 2018 ili kuratibu na
kuangalia maendeleo endelevu ya uvunaji na matumizi ya utajiri wa asili na
rasilimali, pia kusajili na kuangalia mikataba inayohusu rasilimali asilia, na kupitia
sheria, sera na miongozo ili zisiathiri matakwa ya Katiba.
Aidha, Mkurugenzi huyo alisisitiza
Katiba inahitaji wananchi walinde rasilimali hivyo ni vyema wakapata elimu ya
namna ya kulinda kwani uelewa mdogo wa jamii kuhusu sheria ni kikwazo katika
kulinda rasilimali asilia.
Comments
Post a Comment