Wednesday, December 16, 2020

WANYONGE NI LAZIMA WALINDWE NA SHERIA-DKT MWIGULU


 Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba akiongea na kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Shinyanga alipofanya ziara ya kikazi mkoani humo.


Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba akiongea na kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Shinyanga (hawapo pichani)  alipofanya ziara ya kikazi mkoani humo.


XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. John Pombe Magufuli imejipambanua kuwalinda wanyonge hivyo anapojitokeza mtu yeyote kutaka kuwaumiza ni lazima ashughulikiwe kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.
 
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba ametoa angalizo hilo tarehe 15 Disemba 2020 wakati akizungumza kwenye kikao kazi na kamati ya ulinzi na usalama ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mhe Anamringi Macha akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja Mkoani Shinyanga.
 
Nchemba amekemea vikali wananchi wanaotaka kuijaribu serikali inayoongozwa na Mhe Rais Dkt Magufuli kwa kupora haki za watu hivyo ameeleza kuwa lazima watu hao waonyeshwe kwamba serikali haijaribiwi na haki za wananchi haziwezi kuchezewa.
 
"Msihangaike na jambo limetokea wapi badala yake uhalisia utumike kufanikisha utoaji wa maamuzi, ndugu zangu Rais wetu ana maono ya kutetea haki hivyo sisi  wasaidizi wake tunapaswa kuhakikisha kuwa wananchi wanatendewa haki pasina kuonewa" Alikaririwa Mhe Mwigulu Nchemba
 
Awali akisikiliza malalamiko ya mkazi wa Mtaa wa Nyakato Kata ya Nyasubi katika Halmashauri ya Mji wa Kahama Bi Specious Silvester anayemlalamikia aliyekuwa mume wake Ndg Richard Majenga kwa kumfanyia jaribio la kumuua kwa kummwagia Tindikali pamoja na kumzulumu mali zake, Mhe Mwigulu amesema kuwa Sheria na mahakama imechezewa vya kutosha hivyo ni lazima sasa jambo hilo lifike kikomo na hatua kali kuchukuliwa.
 
Katika kikao kazi hicho Waziri Nchemba amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga kuandaa na kusimamia utaratibu wa kisheria kuhakikisha kuwa hakuna jambo lolote litakalofanyika ikiwemo mauziano bubu ya mali za mlalamikaji huyo hadi pale shauri lililoko mahakamani litakapokamilika.
 
Pia ameagiza kuwa Wataalamu wa sheria katika Hamashauri ya Wilaya ya Kahama waandikishe kisheria kuzuia mpango ovu unaoendeshwa wa uuzaji mali huku kesi ipo mahakamani ambapo mpango huo ameutaja kuwa ni dharau kwa mahakama kadhalika ameagiza ufanyike uchunguzi wa haraka kuhusu mali zote za wawili hao.
 
Akizungumzia Mali zingine ambazo tayari zimeshauzwa na zingine zimesalia, Waziri huyo ameagiza zifuatiliwe zote na endapo itabainika umiliki wake ulikuwa wa watu wawili huku mmoja akiuza kinyume na utaratibu basi uchunguzi ukibaini mtu huyo akamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria haraka iwezekanavyo.
 
Kuhusu jaribio la kuua kwa mama huyo kumwagiwa tindikali, Mhe Dkt Mwigulu amesema kuwa halipaswi kuishia hewani lazima lipewe ukubwa namba moja na uchunguzi ufanyike upya ili sheria iweze kuchukua mkondo wake kwani jambo hilo limepelekea ulemavu wa kudumu kwa mama huyo.
 
Kadhalika Waziri Mwigulu ametoa angalizo kwa watendaji wote kutekeleza wajibu wao kwa wakati kwani amesema kuwa Sheria isipochukua mkondo wake  kwa wakati wananchi huchukua sheria mkononi katika kutafuta haki zao.
 
Kwa upande wake Silvester Model ambaye ni baba mzazi wa Specious Silvester ameipongeza serikali kupitia Waziri wa Katiba na Sheria kutembelea eneo lenye mgogoro pamoja na kufanya maamuzi ambayo yametoa taswira ya utendaji uliotukuka wa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
 


Friday, December 11, 2020

ONGEZENI NGUVU KATIKA KUSIMAMIA HAKI ZA WANANCHI - MHE. NCHEMBA


 Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Mwigulu Nchemba akiongea na watumishi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (hawapo pichani) alipofanya ziara katika ofisi ya Tume hiyo. Wengine pichani ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo  Mhe. Geoffrey Mizengo Pinda (kulia) na mwingine ni Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo Ndg. Amon Mpanju.


Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Mhe. Mathew Maimu (aliyesimama) akitoa taarifa ya utekelezaji kwa Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Mwigulu Nchemba alipotembelea ofisi za Tume hiyo.


Baadhi ya watumishi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora wakimsikiliza Waziri wa Katiba na Sheria alipofanya ziara katika ofisi za Tume hiyo.


XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Mwigulu Nchemba aitaka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kuongeza nguvu katika kusimamia na kusikiliza malalamiko ya wananchi.

Mhe. Nchemba ameyasema hayo alipofanya ziara ya kwanza ya kikazi katika Tume hiyo tangu alipoapishwa kushika wadhifa huo katika awamu ya pili ya serikali ya awamu ya tano.

Mhe. Nchemba alisema “changamoto kwa wananchi zinaendelea kukua hivyo ongezeni nguvu katika kazi yenu ya kusikiliza malalamiko yao”

Aliongeza, Tume inatakiwa iwafikie wananchi kule waliko   na waangalie maeneo ambayo wananchi wanakosa haki zao ili waweze kuwatembelea na kutatua changamoto zinazowakabili na kuwawzesha kupata haki hizo kwani maeneo mengi kuna uonevu mwingi na wanyonge kuporwa haki zao.

Alisisitiza kuwa eneo la haki za watu likifanyiwa kazi ipasavyo litasaidia wananchi kuzipata haki hizo kwani Tanzania ni taifa huru hivyo Tume inapaswa kujali wananchi na kuwahudumia wote kwa usawa.

Waziri aliongeza kuwa masuala ya haki za binadamu ni kipaumbele cha Serikali ya awamu ya tano hivyo wasitumie vichaka vya haki kutikisa haki za wananchi ni lazima maslahi ya nchi na wananchi yatangulizwe mbele.

Aidha, nae Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Geoffrey Mizengo Pinda alisema Tume ni taasisi iliyoundwa kusaidia jamii lakini kuna watu wanaotaka kupotosha uwepo wake hivyo Tume ya Haki za Binadamu iende kwa jamii ili waweze kuitambua na iwe rahisi kwao kuweza kuisaidia jamii hiyo.

Awali wakati akitoa taarifa ya utekelezaji kwa Mawaziri hao Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Mhe. Mathew Maimu alisema Tume imekuwa ikifanya kazi mbalimbali za kusaidia upatikanaji wa haki kwa jamii japokuwa imekuwa ikikabiliwa na uhaba mkubwa wa majengo ya ofisi na vitendea kazi.