ONGEZENI NGUVU KATIKA KUSIMAMIA HAKI ZA WANANCHI - MHE. NCHEMBA
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Mwigulu Nchemba akiongea na watumishi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (hawapo pichani) alipofanya ziara katika ofisi ya Tume hiyo. Wengine pichani ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Geoffrey Mizengo Pinda (kulia) na mwingine ni Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo Ndg. Amon Mpanju.
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Mhe. Mathew Maimu (aliyesimama) akitoa taarifa ya utekelezaji kwa Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Mwigulu Nchemba alipotembelea ofisi za Tume hiyo.
Baadhi ya watumishi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora wakimsikiliza Waziri wa Katiba na Sheria alipofanya ziara katika ofisi za Tume hiyo.
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Mwigulu Nchemba aitaka Tume
ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kuongeza nguvu katika kusimamia na
kusikiliza malalamiko ya wananchi.
Mhe. Nchemba ameyasema hayo alipofanya ziara ya kwanza ya
kikazi katika Tume hiyo tangu alipoapishwa kushika wadhifa huo katika awamu ya
pili ya serikali ya awamu ya tano.
Mhe. Nchemba alisema “changamoto kwa wananchi zinaendelea kukua
hivyo ongezeni nguvu katika kazi yenu ya kusikiliza malalamiko yao”
Aliongeza, Tume inatakiwa iwafikie wananchi kule
waliko na waangalie maeneo ambayo wananchi wanakosa
haki zao ili waweze kuwatembelea na kutatua changamoto zinazowakabili na
kuwawzesha kupata haki hizo kwani maeneo mengi kuna uonevu mwingi na wanyonge
kuporwa haki zao.
Alisisitiza kuwa eneo la haki za watu likifanyiwa kazi
ipasavyo litasaidia wananchi kuzipata haki hizo kwani Tanzania ni taifa huru
hivyo Tume inapaswa kujali wananchi na kuwahudumia wote kwa usawa.
Waziri aliongeza kuwa masuala ya haki za binadamu ni
kipaumbele cha Serikali ya awamu ya tano hivyo wasitumie vichaka vya haki
kutikisa haki za wananchi ni lazima maslahi ya nchi na wananchi yatangulizwe
mbele.
Aidha, nae Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Geoffrey
Mizengo Pinda alisema Tume ni taasisi iliyoundwa kusaidia jamii lakini kuna
watu wanaotaka kupotosha uwepo wake hivyo Tume ya Haki za Binadamu iende kwa
jamii ili waweze kuitambua na iwe rahisi kwao kuweza kuisaidia jamii hiyo.
Awali wakati akitoa taarifa ya utekelezaji kwa Mawaziri hao
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Mhe. Mathew Maimu
alisema Tume imekuwa ikifanya kazi mbalimbali za kusaidia upatikanaji wa haki
kwa jamii japokuwa imekuwa ikikabiliwa na uhaba mkubwa wa majengo ya ofisi na
vitendea kazi.
Comments
Post a Comment