WANYONGE NI LAZIMA WALINDWE NA SHERIA-DKT MWIGULU
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba akiongea na kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Shinyanga alipofanya ziara ya kikazi mkoani humo.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba akiongea na kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Shinyanga (hawapo pichani) alipofanya ziara ya kikazi mkoani humo.
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Serikali ya awamu ya tano
inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. John Pombe
Magufuli imejipambanua kuwalinda wanyonge hivyo anapojitokeza mtu yeyote kutaka
kuwaumiza ni lazima ashughulikiwe kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu
Lameck Nchemba ametoa angalizo hilo tarehe 15 Disemba 2020 wakati akizungumza
kwenye kikao kazi na kamati ya ulinzi na usalama ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya
ya Kahama Mhe Anamringi Macha akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja Mkoani
Shinyanga.
Nchemba amekemea vikali wananchi wanaotaka
kuijaribu serikali inayoongozwa na Mhe Rais Dkt Magufuli kwa kupora haki za
watu hivyo ameeleza kuwa lazima watu hao waonyeshwe kwamba serikali haijaribiwi
na haki za wananchi haziwezi kuchezewa.
"Msihangaike na jambo limetokea wapi badala
yake uhalisia utumike kufanikisha utoaji wa maamuzi, ndugu zangu Rais wetu ana
maono ya kutetea haki hivyo sisi wasaidizi wake tunapaswa kuhakikisha
kuwa wananchi wanatendewa haki pasina kuonewa" Alikaririwa Mhe Mwigulu
Nchemba
Awali akisikiliza malalamiko ya mkazi wa Mtaa wa
Nyakato Kata ya Nyasubi katika Halmashauri ya Mji wa Kahama Bi Specious
Silvester anayemlalamikia aliyekuwa mume wake Ndg Richard Majenga kwa kumfanyia
jaribio la kumuua kwa kummwagia Tindikali pamoja na kumzulumu mali zake, Mhe
Mwigulu amesema kuwa Sheria na mahakama imechezewa vya kutosha hivyo ni lazima
sasa jambo hilo lifike kikomo na hatua kali kuchukuliwa.
Katika kikao kazi hicho Waziri Nchemba
amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga kuandaa na kusimamia
utaratibu wa kisheria kuhakikisha kuwa hakuna jambo lolote litakalofanyika
ikiwemo mauziano bubu ya mali za mlalamikaji huyo hadi pale shauri lililoko
mahakamani litakapokamilika.
Pia ameagiza kuwa Wataalamu wa sheria katika
Hamashauri ya Wilaya ya Kahama waandikishe kisheria kuzuia mpango ovu
unaoendeshwa wa uuzaji mali huku kesi ipo mahakamani ambapo mpango huo ameutaja
kuwa ni dharau kwa mahakama kadhalika ameagiza ufanyike uchunguzi wa haraka
kuhusu mali zote za wawili hao.
Akizungumzia Mali zingine ambazo tayari
zimeshauzwa na zingine zimesalia, Waziri huyo ameagiza zifuatiliwe zote na
endapo itabainika umiliki wake ulikuwa wa watu wawili huku mmoja akiuza kinyume
na utaratibu basi uchunguzi ukibaini mtu huyo akamatwe na kuchukuliwa hatua za
kisheria haraka iwezekanavyo.
Kuhusu jaribio la kuua kwa mama huyo kumwagiwa
tindikali, Mhe Dkt Mwigulu amesema kuwa halipaswi kuishia hewani lazima lipewe
ukubwa namba moja na uchunguzi ufanyike upya ili sheria iweze kuchukua mkondo
wake kwani jambo hilo limepelekea ulemavu wa kudumu kwa mama huyo.
Kadhalika Waziri Mwigulu ametoa angalizo kwa
watendaji wote kutekeleza wajibu wao kwa wakati kwani amesema kuwa Sheria
isipochukua mkondo wake kwa wakati wananchi huchukua sheria mkononi
katika kutafuta haki zao.
Kwa upande wake Silvester Model ambaye ni baba
mzazi wa Specious Silvester ameipongeza serikali kupitia Waziri wa Katiba na
Sheria kutembelea eneo lenye mgogoro pamoja na kufanya maamuzi ambayo yametoa
taswira ya utendaji uliotukuka wa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe
Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Comments
Post a Comment