Wednesday, January 20, 2021

WATUMISHI WIZARA YA KATIBA WAJENGEWA UWEZO KUHUSU UANGALIZI WA UTAJIRI WA ASILI NA MALIASILIA


 Mkurugenzi Idara ya Huduma za Kisheria Bw. Griffin Mwakapeje akifungua mafunzo ya siku mbili ya kujengea uwezo watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria katika eneo la Uangalizi wa Utajiri wa Asili na Maliasilia za nchi katika ukumbi wa VETA jijini Dodoma.


Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo.


Mtoa mada kutoka shirika la Petroli la Taifa (TPDC) Dkt. Elias akitoa mada kwa washiriki wa mafunzo.

Picha ya pamoja baada ya ufunguzi wa mafunzo.

XXXXXXXXXXXXXXX

Kitengo cha Uangalizi wa Utajiri  wa Asili na Maliasilia kimeandaa mafunzo ya siku mbili kwa watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria ili kuwajengea uwezo kuhusu masuala ya Uangalizi wa Utajiri na Maliasilia.

Mafunzo hayo yaliyofunguliwa na mwakilishi wa Katibu Mkuu ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Kisheria Bw. Griffin Mwakapeje ambapo alisema mwaka 2017 Serikali iliwasilisha Bungeni miswada ya kutunga sheria mbili za usimamizi wa maliasilia za nchi.

Alisema, hatua za kutunga sheria hizi mbili zilipelekea kujenga uelewa wa pamoja juu ya maliasilia pasipo kuingilia majukumu ya wizara au taasisi nyingine.

Aliongeza kuwa baada ya kutunga sheria wizara iliunda kitengo kwa ajili ya kuratibu ili kuhakikisha watu wote wanajumuika kulinda maliasilia ambapo matokeo baada ya kutungwa kwa sheria hizo ni kujengwa kwa ukuta wa Mererani ili kudhibiti utoroshwaji wa madini, kuanzishwa soko la madini ili wananchi wanufaike na masoko, kuibuka kwa watanzania ambao ni mabilionea na kuanzishwa viwanda vya uchenjuaji.

Mafunzo hayo yalitolewa na Shirika la Petroli la Taifa (TPDC), Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya madini. 


Friday, January 8, 2021

WAZIRI MWIGULU APONGEZA UONGOZI WA MAHAKAMA KWA KUTOA USHIRIKIANO NA KUWAPA NGUVU TAWJA KUFANIKISHA KAZI ZAO


 

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba akisisitiza jambo wakati akimuwakilisha Mhe Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  akifungua Mkutano Mkuu wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA) uliofanyika tarehe 7 Januari 2021 katika ukumbi wa Benki Kuu (BOT) Jijini Mwanza.


Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Geofrey Pinda akisisitiza jambo wakati wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA) uliofanyika tarehe 7 Januari 2021 katika ukumbi wa Benki Kuu (BOT) Jijini Mwanza.


Mgeni rasmi-Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA) uliofanyika tarehe 7 Januari 2021 katika ukumbi wa Benki Kuu (BOT) Jijini Mwanza.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba akikabidhiwa Tuzo na Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu wanawake (TAWJA) Mhe Jaji Joaquuine De-Mello kwa kutambua mchango wake kwa majaji na mahakimu wanawake mara baada ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA) uliofanyika tarehe 7 Januari 2021 katika ukumbi wa Benki Kuu (BOT) Jijini Mwanza.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe Prof. Ibrahim Hamis Juma akikabidhiwa Tuzo na Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu wanawake (TAWJA) Mhe Jaji Joaquuine De-Mello ya kutambua mchango wake kwa Majaji na Mahakimu wananwake wakati wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA) uliofanyika tarehe 7 Januari 2021 katika ukumbi wa Benki Kuu (BOT) Jijini Mwanza.


XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Serikali imefurahishwa kwa kazi zinazofanywa na Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake TAWJA katika kupigania haki za wananchi.

 

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba akimuwakilisha Mhe Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA) uliofanyika tarehe 7 Januari 2021 katika ukumbi wa Benki Kuu (BOT) Jijini Mwanza.

 

Amewataka majaji hao kuendelea kuongeza na kuimarisha Haki za Wanawake katika suala la Haki Sawa kwa wote; Kukuza Upatikanaji wa Haki kwa Wanawake, Kukuza/Kuendeleza Uongozi wa Mahakama; Kufanya tafiti za kisheria katika Usawa wa Kijinsia na Haki za Binadamu; Kubadilishana taarifa katika masuala tata yanayowahusu Wanawake na kuondoa Upendeleo wa Kijinsia na Ubaguzi wa aina yeyote.

 

Amesema kuwa mtazamo mkubwa wa TAWJA ni kuhakikisha Majaji Wanawake na Mahakimu pamoja na Maafisa wengine wa Mahakama na Washirika wanaandaliwa kwa kuwapatia nyenzo sahihi na muhimu zinazohitajika katika kukuza Haki Sawa kwa Wote (‘Equal Justice for All’)

 

“Ninafahamu kuwa mmekuwa mkifanya hivyo bila kuchoka kwa kipindi cha miaka ishirini (20) mfululizo tokea TAWJA kuanzishwa kwake mwaka 2000. Kwa hili niwapongeze sana Wanachama wote, mnatakiwa kujivunia na kutembea kifua mbele kwa kazi nzuri mnazofanya. Naamini kuwa hili lisingewezekana bila msaada mkubwa kutoka kwa Mahakama ya Tanzania Bara na Zanzibar” Alikaririwa Dkt Mwigulu

 

Dkt Mwigulu amesema ni wazi kuwa sauti zao Majaji na Mahakimu Wanawake ikijumuisha na zile za Wadau wengine nchini zimepelekea utayari, uwazi na hamasa katika kulaani ubaguzi na ukiukwaji wa Haki za Binadamu unaofanywa na wanajamii katika maeneo yetu.

 

Waziri Mwigulu amesema kuwa kaulimbiu ya Mkutano huo ni; “Weledi na Ustawi wa Majaji Na Mahakimu Wanawake: Chachu ya Mabadiliko”, imekuja wakati muafaka na mahali sahihi kwani mara nyingi Wanawake Wataalamu hawatilii maanani ustawi wao, na hasa Maafisa wa Mahakama ambao muda wote hutingwa zaidi na majukumu yao ya msingi.

 

Kutokana na Kaulimbiu hiyo, mtaibua vitu vingine vilivyojificha na vinayowakabili Maafisa wa Mahakama amesisitiza katika mkutano huo kujadiliwa kwa kina kuhusu masuala yahusuyo afya za akili na mwili na kudadavua kuhusu uchumi, masuala ya kisaikolojia sambamba na kuangalia ukuaji katika maeneo ya utoaji haki.

 

“Maendeleo ya Mwanamke ni maendeleo ya wote. Hivyo ni lazima kumpa mwanamke kipa umbele. Ni muhimu sana kumpa mwanamke nafasi nyingi bila kujali kuwa ni haki yake ya msingi kwani pia ni kuonyesha matumizi mazuri ya uelewa wa uchumi.” Amesisitiza

 


WAKILI WA SERIKALI MWANDAMIZI WIZARA YA KATIBA NA SHERIA ATUNUKIWA SHAHADA YA UZAMIVU


 


Wakili wa Serikali Mwandamizi kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Anne George Malipula ametunukiwa shahada ya Uzamivu kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA DKT. MWIGULU AAGIZA RITA KUHAMIA DODOMA

 

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba akisisitiza jambo wakati akizungumza na watumishi wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) akiwa katika ziara ya kikazi.


Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Geofrey Mizengo Pinda akisisitiza jambo wakati akizungumza na watumishi wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) wakati alipoandamana na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt Mwigulu Nchemba katika ziara ya kikazi.


Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) Bi Emmy Hudson akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Wakala mbele ya Waziri na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria mara baada ya kuwasili kwenye ofisi za wakala kwa ajili ya ziara ya kikazi.


Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba pamoja na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Geofrey Mizengo Pinda wakikagua maktaba ya kumbukumbu za vyeti vya kuzaliwa na vifo wakati walipotembelea ofisi za Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) wakiwa katika ziara ya kikazi.

Sehemu ya watumishi wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA), Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Waandishi wa Habari wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba akisisitiza jambo wakati  akiwa katika ziara ya kikazi kwenye ofisi za Wakala jijini Dar Es Salaam.


XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Serikali imeitaka Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) wenye maskani yake Jijini Dar es salaam kuanza mchakato wa haraka kuhakikisha unahamia Jijini Dodoma.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba tarehe 21 Disemba 2020 wakati akizungumza na watumishi wa taasisi hiyo akiwa katika ziara ya kikazi Jijini Dar es salaam.

Waziri Mwigulu amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. John Pombe Magufuli ametoa maelekezo ya serikali kuhamia Jijini Dodoma hivyo taasisi zote zinapaswa kuhamia haraka iwezekanavyo.

“Bahati nzuri mmeniambia kuwa mna kiwanja Jijini Dodoma hivyo safari ya Dodoma inawahusu ni lazima mhamie Dodoma, zile Taasisi zinazochelewa kuhamia Dodoma itafikia wakati tutafanya uamuzi wa kuziuza mkiwa ndani ya ofisi” Amekaririwa Dkt Mwigulu

Waziri Mwigulu amemuagiza Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa RITA pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA kuhakikisha kuwa wanaweka mkazo kuhakikisha taasisi hiyo inahamia Dodoma haraka iwezekanavyo.

Ameongeza kuwa Rais Magufuli ameonyesha mfano kwa kujenga Ikulu ya Chamwino inayofanana na Ikulu ya Jijini Dar es salaam huku tayari akiwa amehamia Jijini Dodoma hivyo taasisi hiyo ni muhimu kuhamia Dodoma.

“Binafsi sitopenda ikifanyika sensa ya Taasisi ambazo zinastahili kuhamia Dodoma halafu zikutwe bado zipo Jijini Dar es salaam zikiwemo taasisi za Wizara ya Katiba na Sheria”

Kadhalika ameagiza kuhakikisha kuwa watendaji wa taasisi ya RITA wanatembelea mara kwa mara Jijini Dodoma katika shughuli za kikazi ili kuendelea kuzoea Jiji hilo wakati wanafanya maandalizi ya kuhama.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Katiba na sheria Mhe Geofrey Mizengo Pinda ameitaka taasisi hiyo kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi ili kurahisisha utendaji kazi kadhalika kuongeza uwezekano wa kujitangaza katika vyombo mbalimbali vya habari.

Pinda ameongeza kuwa serikali imekusudia kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi hivyo RITA inapaswa kuongeza urahisi wa upatikanaji wa huduma hususani katika utoaji wa vitambulisho kwa ngazi ya majimbo.

Awali akitoa taarifa ya Taasisi hiyo, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) Bi Emmy Hudson amesema kuwa taasisi hiyo ipo katika mpango mkakati wa kuharakisha ufungaji wa mirasi kwa wakati pamoja na kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara kwa kuhakikisha sheria ya ufilisi inakamilika na kupitishwa na bunge.

Sambamba na hayo amezitaja changamoto mbalimbali zinazoikumba taasisi hiyo ikiwemo kushindwa kuongeza ada ya utoaji wa vyeti vya kuzaliwa pamoja na upungufu wa watumishi kwani waliopo ni 203 kati ya 361 wanaohitajika.


SHERIA, MWENENDO WA MASHAURI NA HUKUMU ZIANDIKWE KWA LUGHA YA KISWAHILI – DKT MWIGULU NCHEMBA

Waziri wa katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba akisisitiza jambo wakati akizungumza na Menejimenti ya Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (Law School of Tanzania) alipofanya ziara katika taasisi hiyo.

 

Waziri wa katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba akisisitiza jambo wakati akizungumza na Menejimenti ya Taasisi ya mafunzo ya uanasheria kwa vitendo Tanzania (Law School of Tanzania).


Waziri wa katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba akikagua maktaba ya Taasisi ya mafunzo ya uanasheria kwa vitendo Tanzania (Law School of Tanzania).


Naibu Waziri wa katiba na Sheria Mhe Geofrey Mizengo Pinda akisisitiza jambo wakati akizungumza na Menejimenti ya Taasisi ya mafunzo ya uanasheria kwa vitendo Tanzania (Law School of Tanzania) alipofanya ziara ya kikazi hivi karibuni.


Mkuu wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (Law School of Tanzania) Jaji Dkt. Benhajj Masoud akimkaribisha waziri wa Katiba na  Sheria Dkt. Mwigulu Nchemba (hayupo pichani) kuzungumza na watumishi wa taasisi hiyo alipofanya ziara ya kikazi hivi karibuni.


XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Serikali imedhamiria kuwasaidia kwa umakini mkubwa wananchi katika tasnia ya sheria ambapo imeagiza kuanza haraka uandaaji wa sheria kwa lugha ya kiswahili ikiwemo mwenendo wa mashauri na hukumu.

 

Agizo hilo kwa katibu mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria limeelekeza kutafutwa haraka iwezekanavyo wataalamu watakaozitafsiri sheria zote zilizoandikwa kwa lugha ya kingereza na kuwa katika lugha ya Taifa ya kiswahili.

 

Waziri wa katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba ametoa agizo hilo tarehe 22 Disemba 2020 alipotembelea Taasisi ya mafunzo ya uanasheria kwa vitendo Tanzania (Law School of Tanzania) wakati akiwa katika siku ya pili ya ziara ya kikazi Jijini Dar es salaam.

 

"Kwenye kauli nzuri za kuvutia tunasema kiswahili ndio lugha nzuri tena ya kuvutia hivyo ni lazima tuanze kufundisha kwa kufuata muelekeo wa lugha ya Taifa ili kuachana na utumwa wa matumizi ya lugha za kikoloni katika sheria zetu" Amekaririwa Mhe Nchemba

 

Amesema kuwa Sheria ambayo mwananchi anahukumiwa imeandikwa kingereza, hukumu anayopewa imeandikwa katika lugha ya kingereza hilo ni eneo la haki za watu hivyo inapaswa kwanza lugha ya kiswahili ndiyo itumike kwenye sheria kisha lugha zingine kama kingereza ziwe nyongeza.

 

Dkt Mwigulu amesema kuwa Sheria zinaandikwa katika lugha ya kingereza na kuwaambia wananchi kutokujua kwao sheria sio sehemu ya utetezi jambo hilo ni kinyume na utaratibu hivyo lazima kufanya mapitio ya sheria zilizopo.

 

"Zipo nchi nyingi Duniani zimeendelea pasina kuwa zinajua lugha ya kingereza hivyo ni wajibu wetu sasa rasmi kuitumia lugha ya kiswahili" Amesisitiza

 

Waziri Mwigulu amesema kuwa katika mikutano mingi ya usaili wa kazi inatumika lugha ya kingereza wakati huo huo viongozi wakuu wa usaili wanatumia lugha ya kiswahili katika familia zao, na hata kazini.

 

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Geofrey Mizengo Pinda amesema kuwa uhitaji wa wataalamu wa kisheria katika maeneo mengi ni mkubwa hivyo taaluma hiyo inapaswa kutolewa kwa weledi mkubwa kwa maslahi makubwa ya Taifa.

 

Amesema kuwa mahitaji ya msaada wa kisheria ni makubwa hivyo ni muhimu kuona ulazima wa kutembelea katika maeneo mbalimbali hususani vijijini kutoa msaada wa kisheria kwani kumekuwa na manyanyaso kwa wananchi wengi.

 

Ameongeza kuwa Taasisi ya mafunzo ya uanasheria kwa vitendo Tanzania ni sehemu ya ukombozi kwa wananchi hivyo kuna kila sababu ya kutengeneza chombo kama hicho kuwafikia wananchi kirahisi.

 


WAZIRI MWIGULU NCHEMBA AIPONGEZA MAHAKAMA KWA UFANISI


Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba akisisitiza jambo wakati akizungumza kwenye kikao kazi na Menejimenti ya Mahakama akiwa katika ziara ya kikazi jijini Dar Es Salaam.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba (Wa Pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe Jaji Prof. Ibrahim Khamis Juma (Wa Pili Kushoto), Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Geofrey Mizengo Pinda (Kushoto) na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi (Kulia) mara baada ya kufanya mazungumzo na Menejimenti ya Mahakama.Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Ernest Mchome akifuatilia hotuba ya Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba (hayupo pichani) akisisitiza jambo wakati akizungumza kwenye kikao kazi na Menejimenti ya Mahakama. 


Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba akifuatilia taarifa ya utekelezaji wa maboresho ya mahakama pamoja na taarifa ya usikilizaji wa mashauri wakati wa kikao kazi na Menejimenti ya Mahakama. 


Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba akisisitiza jambo wakati akizungumza kwenye kikao kazi na Menejimenti ya Mahakama.


XXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Serikali imeipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kazi kubwa yenye weledi uliotukuka inayoifanya kwa ajili ya kuwasaidia wananchi.

Pamoja na pongezi hizo kadhalika mahakama imetakiwa kuhakikisha kuwa inatekeleza kwa haraka mipango inayojiwekea kwani kutofanya hivyo husababisha utekelezaji wake kuwa wa gharama kubwa pasina sababu za msingi.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba ametoa rai hiyo tarehe 23 Disemba 2020 wakati akizungumza na Menejimenti ya Mahakama akiwa katika siku ya tatu ya ziara ya kikazi Jijini Dar es salaam.

Dkt Nchemba amesema kuwa serikali itazifanyia kazi changamoto zote zinazoikabili Mahakama kote nchini ili kuhakikisha kuwa wananchi wanahudumiwa ipasavyo ikiwemo mashauri kufanyiwa kazi kwa haraka.

Ameongeza kuwa kunapokuwa na uwezekano wa kutatua mambo kwa haraka ni vyema mahakama na taaisisi zote za serikali kuzitatua bila kuwa na mkwamo wowote ili kuwarahisishia wananchi upatikanaji wa huduma.

Dkt Nchemba amesisitiza kuwa Mahakama pamoja na watendaji wote wa serikali wanapaswa kufanya kazi kwa uthubutu na kuchukua hatua kama ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. John Pombe Magufuli amekuwa akisisitiza kufanya maamuzi mbalimbali pasina kufanya uonevu kwa wananchi.

Kuhusu kubadilisha sheria, Mwenendo wa mashauri na Hukumu, Amesisitiza maelekezo yake aliyoyatoa wakati alipotembelea Taasisi ya mafunzo ya uanasheria kwa vitendo Tanzania (Law School) kuhusu kubadilisha sheria, Mwenendo wa mashauri pamoja na Hukumu kuwa katika lugha ya Kiswahili.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Geofrey Mizengo Pinda ameipongeza mahakama kwa kazi kubwa ambayo inazifanya kuhakikisha wananchi wanapata haki pasina uonevu.

“Kesi nyingi hazijaamuriwa kutokana na vyombo vingi kuingia katika kukamilisha kazi zao ikiwemo Polisi, hivyo kuna kila sababu ya ukamilishaji wa taarifa muhimu za upelelezi ili mahakama iweze kukamilisha utoaji hukumu kwa haraka” Amesisitiza Mhe Pinda

Akizungumza kwa niaba ya Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe Jaji Prof. Ibrahim Khamis Juma, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi ameshukuru kwa ushirikiano inaoupata kutoka Wizara ya Katiba na Sheria kwani bila uongozi madhubuti huenda baadhi ya mambo yangekuwa hayajakamilika.

Jaji Dt Feleshi amesema kuwa ushirikiano huo umeongeza uwajibikaji na utekelezaji wa haraka wa majukumu yake.