WAZIRI MWIGULU NCHEMBA AIPONGEZA MAHAKAMA KWA UFANISI
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba
akisisitiza jambo wakati akizungumza kwenye kikao kazi na Menejimenti ya
Mahakama akiwa katika ziara ya kikazi jijini Dar Es Salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Ernest Mchome akifuatilia hotuba ya Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba (hayupo pichani) akisisitiza jambo wakati akizungumza kwenye kikao kazi na Menejimenti ya Mahakama.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba akifuatilia taarifa ya utekelezaji wa maboresho ya mahakama pamoja na taarifa ya usikilizaji wa mashauri wakati wa kikao kazi na Menejimenti ya Mahakama.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba akisisitiza jambo wakati akizungumza kwenye kikao kazi na Menejimenti ya Mahakama.
XXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Serikali imeipongeza Mahakama ya Tanzania kwa
kazi kubwa yenye weledi uliotukuka inayoifanya kwa ajili ya kuwasaidia wananchi.
Pamoja na pongezi hizo kadhalika mahakama
imetakiwa kuhakikisha kuwa inatekeleza kwa haraka mipango inayojiwekea kwani
kutofanya hivyo husababisha utekelezaji wake kuwa wa gharama kubwa pasina
sababu za msingi.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu
Nchemba ametoa rai hiyo tarehe 23 Disemba 2020 wakati akizungumza na
Menejimenti ya Mahakama akiwa katika siku ya tatu ya ziara ya
kikazi Jijini Dar es salaam.
Dkt Nchemba amesema kuwa serikali itazifanyia
kazi changamoto zote zinazoikabili Mahakama kote nchini ili kuhakikisha kuwa
wananchi wanahudumiwa ipasavyo ikiwemo mashauri kufanyiwa kazi kwa haraka.
Ameongeza kuwa kunapokuwa na uwezekano wa
kutatua mambo kwa haraka ni vyema mahakama na taaisisi zote za serikali
kuzitatua bila kuwa na mkwamo wowote ili kuwarahisishia wananchi upatikanaji wa
huduma.
Dkt Nchemba amesisitiza kuwa Mahakama pamoja na
watendaji wote wa serikali wanapaswa kufanya kazi kwa uthubutu na kuchukua
hatua kama ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. John Pombe
Magufuli amekuwa akisisitiza kufanya maamuzi mbalimbali pasina kufanya uonevu
kwa wananchi.
Kuhusu kubadilisha sheria, Mwenendo wa
mashauri na Hukumu, Amesisitiza maelekezo yake aliyoyatoa wakati alipotembelea
Taasisi ya mafunzo ya uanasheria kwa vitendo Tanzania (Law School) kuhusu
kubadilisha sheria, Mwenendo wa mashauri pamoja na Hukumu kuwa katika lugha ya
Kiswahili.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Katiba na
Sheria Mhe Geofrey Mizengo Pinda ameipongeza mahakama kwa kazi kubwa ambayo
inazifanya kuhakikisha wananchi wanapata haki pasina uonevu.
“Kesi nyingi hazijaamuriwa kutokana na vyombo
vingi kuingia katika kukamilisha kazi zao ikiwemo Polisi, hivyo kuna kila
sababu ya ukamilishaji wa taarifa muhimu za upelelezi ili mahakama iweze
kukamilisha utoaji hukumu kwa haraka” Amesisitiza Mhe Pinda
Akizungumza kwa niaba ya Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe Jaji Prof. Ibrahim Khamis
Juma, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe Jaji
Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi ameshukuru kwa ushirikiano inaoupata kutoka
Wizara ya Katiba na Sheria kwani bila uongozi madhubuti huenda baadhi ya mambo
yangekuwa hayajakamilika.
Jaji Dt Feleshi amesema kuwa ushirikiano huo
umeongeza uwajibikaji na utekelezaji wa haraka wa majukumu yake.
Comments
Post a Comment