WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA DKT. MWIGULU AAGIZA RITA KUHAMIA DODOMA

 

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba akisisitiza jambo wakati akizungumza na watumishi wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) akiwa katika ziara ya kikazi.


Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Geofrey Mizengo Pinda akisisitiza jambo wakati akizungumza na watumishi wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) wakati alipoandamana na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt Mwigulu Nchemba katika ziara ya kikazi.


Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) Bi Emmy Hudson akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Wakala mbele ya Waziri na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria mara baada ya kuwasili kwenye ofisi za wakala kwa ajili ya ziara ya kikazi.


Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba pamoja na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Geofrey Mizengo Pinda wakikagua maktaba ya kumbukumbu za vyeti vya kuzaliwa na vifo wakati walipotembelea ofisi za Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) wakiwa katika ziara ya kikazi.

Sehemu ya watumishi wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA), Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Waandishi wa Habari wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba akisisitiza jambo wakati  akiwa katika ziara ya kikazi kwenye ofisi za Wakala jijini Dar Es Salaam.


XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Serikali imeitaka Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) wenye maskani yake Jijini Dar es salaam kuanza mchakato wa haraka kuhakikisha unahamia Jijini Dodoma.

Agizo hilo limetolewa na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba tarehe 21 Disemba 2020 wakati akizungumza na watumishi wa taasisi hiyo akiwa katika ziara ya kikazi Jijini Dar es salaam.

Waziri Mwigulu amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. John Pombe Magufuli ametoa maelekezo ya serikali kuhamia Jijini Dodoma hivyo taasisi zote zinapaswa kuhamia haraka iwezekanavyo.

“Bahati nzuri mmeniambia kuwa mna kiwanja Jijini Dodoma hivyo safari ya Dodoma inawahusu ni lazima mhamie Dodoma, zile Taasisi zinazochelewa kuhamia Dodoma itafikia wakati tutafanya uamuzi wa kuziuza mkiwa ndani ya ofisi” Amekaririwa Dkt Mwigulu

Waziri Mwigulu amemuagiza Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa RITA pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA kuhakikisha kuwa wanaweka mkazo kuhakikisha taasisi hiyo inahamia Dodoma haraka iwezekanavyo.

Ameongeza kuwa Rais Magufuli ameonyesha mfano kwa kujenga Ikulu ya Chamwino inayofanana na Ikulu ya Jijini Dar es salaam huku tayari akiwa amehamia Jijini Dodoma hivyo taasisi hiyo ni muhimu kuhamia Dodoma.

“Binafsi sitopenda ikifanyika sensa ya Taasisi ambazo zinastahili kuhamia Dodoma halafu zikutwe bado zipo Jijini Dar es salaam zikiwemo taasisi za Wizara ya Katiba na Sheria”

Kadhalika ameagiza kuhakikisha kuwa watendaji wa taasisi ya RITA wanatembelea mara kwa mara Jijini Dodoma katika shughuli za kikazi ili kuendelea kuzoea Jiji hilo wakati wanafanya maandalizi ya kuhama.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Katiba na sheria Mhe Geofrey Mizengo Pinda ameitaka taasisi hiyo kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi ili kurahisisha utendaji kazi kadhalika kuongeza uwezekano wa kujitangaza katika vyombo mbalimbali vya habari.

Pinda ameongeza kuwa serikali imekusudia kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi hivyo RITA inapaswa kuongeza urahisi wa upatikanaji wa huduma hususani katika utoaji wa vitambulisho kwa ngazi ya majimbo.

Awali akitoa taarifa ya Taasisi hiyo, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) Bi Emmy Hudson amesema kuwa taasisi hiyo ipo katika mpango mkakati wa kuharakisha ufungaji wa mirasi kwa wakati pamoja na kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara kwa kuhakikisha sheria ya ufilisi inakamilika na kupitishwa na bunge.

Sambamba na hayo amezitaja changamoto mbalimbali zinazoikumba taasisi hiyo ikiwemo kushindwa kuongeza ada ya utoaji wa vyeti vya kuzaliwa pamoja na upungufu wa watumishi kwani waliopo ni 203 kati ya 361 wanaohitajika.


Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YAIPONGEZA WIZARA KWA UTEKELEZAJI WA MAMA SAMIA LEGAL AID CAMPAIGN

TUFANYE KAZI KWA UADILIFU NA USHIRIKIANO - MHE CHANA