Thursday, February 25, 2021

KIKAO CHA KUCHAMBUA TAKWIMU ZA MCHANGO WA UTAJIRI WA ASILI NA MALIASILIA ZA NCHI KATIKA PATO LA TAIFA


Wajumbe wa kikao kazi cha wataalam wa ndani na nje ya wizara wakijadili jinsi ya kuchambua takwimu za mchango wa Utajiri wa Asili na Maliasilia za Nchi katika pato la Taifa. Wataalam hao wanatoka Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Fedha na Mipango, Wakala wa Serikali Mtandao, Ofisi ya Taifa ya Takwimu, ESRF, REPOA na Baaza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi.


Sehemu ya wajumbe wa kikao kazi cha wataalam wa ndani na nje ya wizara wakijadili jinsi ya kuchambua takwimu za mchango wa Utajiri wa Asili na Maliasilia za Nchi katika pato la Taifa.


Mkurugenzi wa Kitengo cha Uangalizi wa Utajiri Asilia na Maliasilia za nchi Bi. Neema Mwanga akisisitiza jambo katika kikao kazi cha wataalam wa ndani na nje ya wizara wakijadili jinsi ya kuchambua takwimu za mchango wa Utajiri wa Asili na Maliasilia za Nchi katika pato la Taifa.

Mjumbe wa kikao kazi cha wataalam kujadili jinsi ya kuchambua takwimu za mchango wa Utajiri wa Asili na Maliasilia za Nchi katika pato la Taifa Bw. Emanoel Alfred ambaye ni Mchambuzi wa Sera kutoka Taasisi ya Uongozi akichangia mada.


Majadiliano kuhusu  uchambuzi wa takwimu za mchango wa Utajiri wa Asili na Maliasilia za Nchi katika pato la Taifa yakiendelea.

Friday, February 12, 2021

WANANCHI WAASWA KUANDIKA WOSIA KUEPUKA MIGOGORO NDANI YA FAMILIA

 

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Geophrey Pinda akizungumza kwenye semina ya kujenga uelewa kwa Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kwenye masuala ya Utajiri Asilia na Maliasilia za Nchi na Wosia na Mirathi.


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Ndg. Amon Mpanju akizungumza katika  semina ya kujenga uelewa kwa Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kwenye masuala ya Utajiri Asilia na Maliasilia za Nchi na Wosia na Mirathi.


Mwenyekiti wa  Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza  kwenye semina ya kamati hiyo kwenye masuala ya Utajiri Asilia na Maliasilia za Nchi na Wosia na Mirathi.


Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA Bi. Emmy Hudson akizungumza katika  semina ya kujenga uelewa kwa Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kwenye masuala ya Utajiri Asilia na Maliasilia za Nchi na Wosia na Mirathi.


Wajumbe wa  Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa kwao katika semina ya kuwajengea uelewa juu ya masuala ya Utajiri Asilia na Maliasilia za Nchi na Wosia na Mirathi.

Picha ya pamoja baada ya semina.

XXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria imetoa wito kwa wananchi kuandika  na kuhifadhi wosia katika taasisi ya RITA ili kuepuka migogoro ndani ya familia.

Kamati hiyo inayoongozwa na Mhe. Mohamed Mchengerwa imeona kuwa migogoro mingi inayosababishwa na ndugu kulazimisha kurithi mali za marehemu kinyume na taratibu na sheria zinazosimamia masuala ya mirathi inasababishwa na kutokuwepo na wosia.

Akizungumza katika kikao cha kamati hiyo jijini Dodoma Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Mohamed Mchengerwa amewahimiza wabunge wote ambao bado hawajaandika wosia kufanya hivyo ikiwa kama sehemu ya kuwahamasisha wananchi wao kuchukua hatua mapema na kulifanya jambo hilo kuwa ni kipaumbele kwani migogoro na kesi nyingi zinazohusu mirathi zinatokea katika majimbo yao na kwa kiasi kikubwa huchangiwa  na kutoachwa muongozo unaoelezea mgawanyo wa mali za marehemu.

Alisema "kwa kiasi kibubwa migogoro mingi hutokea na ukifuatilia chanzo chake unabaini kinasababishwa na kutoachwa muongozo unaotoa maelekezo kuhusu mgawanyo wa mali za marehemu" alisema Mhe. Mchengerwa.

Aidha katika kikao hicho Kamati hiyo pia ilipata nafasi ya kujengewa uelewa juu ya kitengo kipya kilichoanzishwa wizarani cheny jukumu la kusimamia Utajiri Asilia na Maliasilia za nchi

Friday, February 5, 2021

SERIKALI HAINA SHERIA KANDAMIZI, SHERIA ZOTE ZINAZOTUMIKA NCHINI ZIMETUNGWA NA BUNGE – MHE. GEOFREY PINDA

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Geophrey Pinda akijibu maswali bungeni wakati wa mkutano wa 12 Jijini Dodoma, Leo tarehe 5 Februari 2021.


XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX 

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Geophrey Pinda amewahakikishia watanzania kuwa Serikali haina Sheria Kandamizi hivyo Sheria zote zinazotumika nchini zilitungwa na Bunge tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo halijawahi kutunga Sheria Kandamizi.

Amesema kuwa Serikali kwa kuzingatia mahitaji ya wakati na watu wake, imekuwa ikiwasilisha mapendekezo ya marekebisho ya Sheria mbalimbali ili kuziboresha Sheria hizo.

Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe Zainab Katimba aliyetaka kufahamu Serikali ina mpango gani wa kurekebisha baadhi ya sheria kandamizi kwa wanawake ili ziendane na wakati, Mhe Pinda amesema kuwa Kutokana na wakati uliopo na mahitaji ya sasa Serikali imeanzisha mchakato wa kuzipitia baadhi ya sheria ili ziweze kufanyiwa marekebisho kuendana na wakati.

Amesema Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imeandaa muswada wa mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Ndoa utakaowasilishwa Bungeni ili kuiboresha, kwa lengo la kulinda makundi ya wanufaika na Sheria hiyo.

Aidha, Serikali inaendelea na hatua mbalimbali za kupitia Sheria ya Usimamizi wa Mirathi na Sheria za Kimila. Hatua hizo zikikamilika, Muswada wa mapendekezo ya kuzirekebisha sheria hizo utawasilishwa Bungeni, ili Wabunge wapate nafasi nzuri ya kujadiliana na kuyapitisha marekebisho hayo.  

Mhe Pinda amesema kuwa Wizara ipo katika mabadiliko makubwa ya kuhakikisha kunafanyika maboresho makubwa ya Sheria zetu ikiwemo kuzitafsiri kwa Kiswahili lakini pia kuweka vipengele kwenye sheria hizo vya kutoa hukumu kwa lugha ya Kiswahili jambo ambalo litaleta tija kubwa katika ukuaji wa uchumi wa Nchi yetu.

Hivyo amewaomba wabunge kuunga mkono juhudi za Serikali katika eneo hilo kwa lengo la kuimarisha utawala wa Sheria na upatikanaji wa haki nchini.

 

RAIS MAGUFULI ASISITIZA KUHARAKISHWA KWA MATUMIZI YA KISWAHILI MAHAKAMANI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Magufuli akizungumza wakati wa sherehe ya maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini iliyofanyika kitaifa jijini Dodoma Februari 01,2021.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Juma akitoa hotuba yake kwa viongozi na wananchi waliohudhuria sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Sheria na miaka 100 ya Mahakama Kuu ya Tanzania.

Baadhi ya viongozi na wananchi waliohudhuria sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Sheria na Miaka 100 ya Mahakama Kuu ya Tanzania.


XXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametoa rai kwa Mhimili wa Mahakama kuweka mkakati wa kutumia lugha ya Kiswahili Mahakamani kwa manufaa ya wananchi huku akimpongeza na kumteua Jaji Zephrine Galeba kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani kwa kuonyesha uzalendo wa kuandika hukumu kwa kutumia Kiswahili.

Rais Magufuli ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe za maadhimisho ya siku ya sheria nchini yaliyofanyika kitaifa jijini Dodoma, alisema kuwa Kiswahili ni miongoni mwa lugha kubwa duniani, ambayo inatumiwa na Watanzania wengi.

“Nitumie fursa hii, kumpongeza sana Mheshimiwa Jaji Galeba wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma kwa kutumia Kiswahili katika kutoa hukumu kwenye Kesi ya North Mara Gold Mine dhidi ya Gerald Nzumbi katika kesi ya Mapitio Na. 23 ya Mwaka 2020. Huyu ni Mzalendo wa kweli wa lugha ya Kiswahili kwenye Mahakama. Na kwa sababu 27 ya uzalendo wake, kuanzia leo, namteua kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa,” alisema Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais alisema kuwa kushindwa kuitumia Lugha hii kwenye masuala ya Kimahakama na Kisheria sio tu kunawanyima haki wananchi, bali pia kuwaongezea gharama kupitia ukalimani wa kutafsiri hukumu na mienendo ya kesi.

Aliendelea kwa kutoa rai kwa kuwasihi wadau wote wa Mahakama, ikiwemo Mahakama, Bunge, Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kuandaa Mkakati wa kuwezesha lugha ya Kiswahili kwenye masuala ya Sheria na Mahakama, ikiwemo kuendelea kuzitafsiri Sheria za zamani na kutunga Sheria mpya kwa lugha ya Kiswahili.

Kwa upande mwingine, Mhe. Rais alizungumzia pia tatizo la ucheleweshaji wa mashauri kuwa bado lipo, hususan mashauri yanayohusu masuala ya biashara na mikopo ambayo yanazorotesha ukuaji wa uchumi wa nchi.

“Ipo tabia ya baadhi ya wateja wa Benki kukimbilia Mahakamani na kufungua kesi nyingi au kuweka mazuio kwa lengo la kuchelewesha urejeshaji wa mikopo wanaodaiwa na benki. Kesi za namna hiyo zipo nyingi, na nyingine zina zaidi ya miaka mitano hazijaamuliwa,” alieleza Mhe. Rais.

Alitoa mifano ya kesi zilizofunguliwa Mahakamani na wateja wakubwa wa Benki nne ambazo ni Benki ya Posta Tanzania (TPB), Benki ya Azania (Azania Bank Ltd) na Benki ya Maendeleo (TIB).

“Hali hii ya wadaiwa kukimbilia Mahakamani na kesi kuchelewa kutolewa maamuzi, imekuwa na athari nyingi za kiuchumi kwa nchi yetu. Baadhi ya athari hizo ni kupungua kwa uwezo wa benki zetu kutoa mikopo kwa wateja; (ii) kuongezeka kwa gharama za riba kutokana na benki kulazimika kuongeza riba na kadhalika,” alieleza.

Aliongeza kuwa kwa mujibu wa taarifa Desemba 31, 2020 inaonyesha kuwa Azania Bank Ltd ina kesi 36 zilifunguliwa na wadaiwa wake zenye thamani ya shilingi bilioni 352.27; Benki ya Maendeleo (TIB) ina kesi 44 zenye thamani ya shilingi bilioni 167.267; Benki ya TPB ina kesi 16 zilizofunguliwa na wadaiwa wake zenye thamani ya shilingi bilioni 6.2; CRDB ina kesi 282 zenye thamani ya shilingi bilioni 113.25.

Akizungumzia Maadili ya Watumishi wa Mahakama, Mhe. Rais alimpongeza Mhe. Jaji Mkuu kwa hatua kinidhamu zilizochukuliwa na Mahakama dhidi ya Maafisa wake wanaoichafua Taasisi huku akitoa wito kwa Kamati za maadili za Maafisa wa Mahakama za Mikoa na Wilaya kukutana.

“Hata hivyo, nimesikitika sana na taarifa kwamba, Kamati za Maadili za Maafisa wa Mahakama za Mikoa na Wilaya, ambazo kisheria zinaongozwa na Wakuu wa Mikoa na Wilaya zimekuwa hazikutani; na hivyo, kushindwa kuchukua hatua za kinidhamu kwa watumishi wenye makosa. Napenda kutumia fursa hii kuagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya wote kuhakikisha Kamati hizo za Maadili 24 zinakutana ili kujadili masuala ya maadili ya watumishi wa Mahakama. Naagiza pia Wakuu wote wa Mikoa kuwasilisha Ripoti vya Vikao vya Kamati hizo mwezi huu,” alisisitiza Mhe. Rais.

Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameiomba Serikali na Bunge kuyapa kipaumbele mahitaji ya Mahakama yaliyooneshwa katika mpango wa miaka mitano wa maendeleo ya miundombinu ya Mahakama 2016/17-2020/2021 itakapojadili na kupitisha Mpango wa Taifa wa maendeleo wa miaka mitano.

 “Mhimili wa Mahakama peke yake hauwezi kutatua changamoto bila kuwezeshwa na Mihimili ya Serikali na Bunge inayosimamia rasilimali za aina zote, hapa  napenda kutambua namna mihimili ya Serikali na Bunge ilivyokubali jukumu la kutatua changamoto zinazoikabili Mahakama ya Tanzania”, alisema Jaji Mkuu.

Kwa mujibu wa Prof. Juma, mfano wa Mhimili wa Mahakama kuwezeshwa na Serikali ni kukamilishwa kwa mazungumzo na Benki ya Dunia kuhusu namna ya kusaidia kuendeleza juhudi za maboresho ya utoaji huduma za Mahakama kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha za kuboresha shughuli na huduma za Mahakama.

Mwaka 2016, Benki ya Dunia iliridhia kuisaidia Mahakama ya Tanzania kupitia Serikali ya Tanzania kupata fedha za mkopo wenye masharti nafuu uliogharimu Dola za Marekani milioni 65 ambazo ni saw ana shilingi bilioni 139.5 za kitanzania.

Akizungumzia namna mhimili huo ulivyowezeshwa, Jaji Mkuu alisema miongoni mwa mafanikio yaliyotokana na uwezeshwaji huo ni kukamilika kwa ujenzi wa majengo ya Mahakama Kuu kanda za Kigoma na Musoma. Aliongeza kuwa, Mahakama inatarajia kukamilisha ujenzi wa majengo ya Mahakama Kuu nyingine sita katika miji ya Mwanza, Arusha, Dodoma, Morogoro pamoja na wilaya za Temeke na Kinondoni mkoani Dar es salaam.

Alisema katika kuendelea kusogeza huduma za Mahakama karibu zaidi na wananchi, Mahakama ya Tanzania inatarajia kuanza ujenzi wa majengo ya Mahakama za wilaya 25 katika mwaka wa fedha 2020/21. Alisema ujenzi huo utawapunguzia mzigo wananchi ambao hulazimika kupata huduma kwenye Mahakama za wilaya jirani. 

 


Wednesday, February 3, 2021

VIONGOZI MBALIMBALI WALIOTEMBELEA BANDA LA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA KATIKA MAADHIMISHO YA WIKI YA SHERIA


 Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Prof. Adelardus Kilangi akisaini kitabu cha wageni alipotembelea banda la Wizara ya Katiba na Sheria katika maadhimisho ya Wiki ya Sheria na Miaka 100 ya Mahakama Kuu.


Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Geophrey Mizengo Pinda akimuelekeza jambo Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Kisheria kwa Umma Bw. Griffin Mwakapeje alipotembelea banda la Wizara ya Katiba na Sheria katika maadhimisho ya Wiki ya Sheria na Miaka 100 ya Mahakama Kuu.


Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Geophrey Mizengo Pinda akisaini kitabu cha wageni  alipotembelea banda la Mahakama Kuu katika maadhimisho ya Wiki ya Sheria na Miaka 100 ya Mahakama Kuu.


 Mwenyekiti wa Tume ya Ushindani Mhe. Jaji Stephen Magoiga akipata maelezo kutoka kwa watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria alipotembelea banda la Wizara ya Katiba na Sheria  katika maadhimisho ya Wiki ya Sheria na Miaka 100 ya Mahakama Kuu.


 Kaimu Mtendaji Mkuu RITA akisaini kitabu cha wageni  alipotembelea banda la Wizara ya Katiba na Sheria  katika maadhimisho ya Wiki ya Sheria na Miaka 100 ya Mahakama Kuu.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Palamagamba Kabudi akisaini kitabu cha wageni  alipotembelea banda la Wizara ya Katiba na Sheria  katika maadhimisho ya Wiki ya Sheria na Miaka 100 ya Mahakama Kuu.TUMIENI MITANDAO YA SIMU KUELIMISHA MASUALA YA KISHERIA - MAKAMU WA RAIS


 Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan akishiriki matembezi ya maadhimisho ya Wiki ya Sheria na miaka 100 ya Mahakama Kuu.


Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Ibrahim Juma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome wakifurahia jambo wakati wa matembezi ya maadhimisho ya Wiki ya Sheria na miaka 100 ya Mahakama Kuu.


Watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria wakishiriki matembezi ya maadhimisho ya Wiki ya Sheria na miaka 100 ya Mahakama Kuu.

Baadhi ya watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria wakifuatilia hotuba ya Makamu wa Rais wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki ya Sheria na Miaka 100 ya Mahakama Kuu.

 Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Prof. Sifuni Mchome (waliokaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa wizara hiyo baada ya uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki ya Sheria na Miaka 100 ya Mahakama Kuu.

XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameushauri Mhimili wa Mahakama nchini kutumia Mitandao ya simu kutoa elimu ya sheria kwa wananchi kupitia jumbe fupifupi.

Akifungua rasmi Maonesho ya Maadhimisho ya Wiki ya Sheria na miaka 100 ya Mahakama Kuu ya Tanzania mapema leo jijini Dodoma, Makamu wa Rais amesema kuwa kwa kufanya hivyo wananchi wengi watapata ufahamu juu ya taratibu mbalimbali za kimahakama.

“Hivi sasa mitandao ya simu imekuwa na desturi ya kutuma meseji mbalimbali kuhusu huduma kadhaa inazotoa, hivyo tumieni pia fursa hiyo pia kutumia mitandao ya simu kutoa elimu kuhusu taratibu za Mahakama ili wananchi wapate uelewa,” alisema Makamu wa Rais.

Akizungumzia matumizi ya lugha ya Kiswahili, Mhe. Suluhu ameiomba Mahakama kutumia Kiswahili hata katika machapisho yake kueleza taratibu mbalimbali za mhimili huo ili wananchi waweze kuelewa.

“Haitopendeza kuona Taifa huru ambalo Mahakama Kuu inatimiza miaka 100 bado wananchi wake walio wengi wanakosa haki zao za msingi kutokana na changamoto ya lugha Mahakamani,” alieleza.

Aidha, Makamu huyo wa Rais alitoa rai kwa Mahakama kuhakikisha kuwa katika mikakati yake ihakikishe kuwa sheria za nchi zinakuwa na tafsiri sahihi na malengo na azma ya kutungwa kwao na kuwa.

Kwa upande mwingine, Makamu wa Rais aliipongeza Mahakama kwa kutimiza miaka 100 ya Mahakama Kuu nchini tangu kuanzishwa kwake huku akimsifu Mhe. Jaji Mkuu kwa mageuzi na marekebisho mbalimbali katika sekta ya sheria.

“Mhe. Jaji Mkuu nafahamu tangu uteuliwe umesukuma mageuzi na marekebisho mbalimbali ya sheria kwenye Mahakama ili kuweza kuufanya mhimili huu kwenda na wakati lakini pia kuhimili mabadiliko. Nakupongeza sana wewe binafsi na Mhimili wote wa Mahakama kwa kutimiza miaka 100 mkiwa mmeimarisha vyema utendaji wa chombo chenu,” alisisitiza Mhe. Suluhu.

Kwa ujumla Mhe. Makamu wa Rais alipongeza pia maboresho mbalimbali ya Mahakama yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika huku akiahidi ushirikiano kutoka Serikalini ili huduma ya utoaji haki iendelee kutenda haki.

Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania-Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka wananchi kutumia tovuti ya Mahakama kupata taarifa zinazohusiana na Mahakama.

“Nitumie nafasi hii kuwakaribisha wananchi wote watembelee Tovuti za Mahakama na za wadau wa sekta ya Haki ili kupata taarifa muhimu kila siku, wakati wowote na watoe maoni na mapendekezo kila siku yenye lengo la kuboresha utoaji haki nchini,” alisema.

Aidha, aliwataka wananchi kutembelea maonesho hayo na kuongeza kuwa wasiridhike na maboresho yaliyopo bali waendelee kudai maboresho zaidi yanayolenga kuwawezesha kupata haki.

Akizungumzia matumizi ya Kiswahili Mahakamani, Mhe. Jaji Prof. Juma alisema jitihada za kuhakikisha kuwa lugha ya Kiswahili inatumika katika ngazi zote za Mahakama zilianza tangu wakati TELFORD PHILIP GEORGES alipokuwa Jaji Mkuu wa Tanzania kati ya mwaka 1965 na 1971.

“Mahakama ya Tanzania imeanza matayarisho ya awali ili kumbukumbu za mashauri na hukumu za Mahakama katika ngazi za Mahakama za Wilaya, za Hakimu Mkazi, Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani ziweze kupatikana papo hapo, katika lugha ya Kiswahili na kwa lugha ya kiingereza kabla ya mwisho wa mwaka huu,” alieleza Mhe. Jaji Mkuu.

Katika hafla hiyo, Mhe. Suluhu alizindua pia miongozo mbalimbali ya Mahakama ikiwemo muongozo wa Dhamana, mwongozo wa utekelezaji wa mashauri, mwongozo wa usimamizi wa uondoshaji wa vielelezo, mwongozo wa madalali na Wasambaza nyaraka za Mahakama.

Mingine ni mwongozo wa watumiaji wa huduma za Mahakama, Mwongozo wa utoaji hukumu kwa Maofisa wa Mahakama na Mwongozi wa kushughulikia mashauri yanayohusu makundi maalum.

Maadhimisho ya wiki ya sheria yaliyozinduliwa rasmi Januari 24 na kilele cha Siku ya Sheria Nchini, huashiria kuanza kwa mwaka mpya wa Kimahakama ambao ni mwanzo wa shughuli za Mahakama katika mwaka. Maonesho hayo ambayo yanafanyika kitaifa katika Viwanja vya Nyerere ‘Square’ yameshirikisha wadau mbalimbali kama Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka na wengineo.