KAMISHENI YA AFRIKA HAKI ZA BINADAMU NA WATU YAIPONGEZA TANZANIA KWA MIRADI MIKUBWA YA MAENDELEO

 


Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.Prof.Palamagamba Kabudi,akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma mara baada ya kumaliza kuwasilisha ripoti ya haki za binadamu katika kikao cha 68 cha Kamisheni ya Afrika ya Haki za binadamu na Watu uliofanyika kwa njia ya Mtandao.


XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Tanzania imewasilisha ripoti ya haki za binadamu kwenye kikao cha 68 cha Kamisheni ya Afrika ya haki za binadamu na watu, huku kamisheni hiyo ikiipongeza kwa kupiga hatua kubwa katika kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi hasa suala la kusambaza umeme vijijini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho kilichofanyika kwa njia ya mtandao kikijumuisha nchi zote wanachama na makao Makuu ya kamisheni ambayo ni nchi ya Gambia, Waziri wa Katiba na sheria Prof. Palamagamba Kabudi,amesema kuwa mara baada ya mawasilisho hayo Kamisheni imeipongeza Tanzania kwa kupiga hatua kubwa katika miradi ya maendeleo ambayo inagusa wananchi moja kwa moja katika kujiletea maendeleo.

“Moja wameridhika kwa kiasi kikubwa sana katika miradi ya maendeleo, ambapo mwenyekiti amerudia tena kupongeza katika suala la kusambaza umeme vijijini ambapo kwa miaka mitano tumefikisha vijiji 9112 vilivyopata umeme kutoka vijiji 2114 mwaka 2015, kati ya vijiji vilivyopo 12268 katika nchi yetu” amesema Prof.Kabudi.

Aidh amesema katika ripoti waliyoiwasilisha wameonyesha mambo makubwa yaliyofanyika ndani ya nchi ya Tanzania kuhusu haki za binadamu ambayo yanaunganisha haki za kisiasa, uchumi, kijamii, na kiutamaduni ambapo Tanzania imepiga hatua katika elimu na afya na huduma nyingine za kijamii kama maji safi hasa maeneo ya vijijini.

“Katika sekta ya elimu tumeeleza hatua kubwa tuliyoipiga hasa kwa kutekeleza elimu bila malipo ambapo kila mwezi tumekuwa tukitoa shilingi bilioni 24 katika kuhakikisha wanafunzi wanasoma bure na katika afya ujenzi wa hospitali, vituo vya afya, Zahanati na hospitali za rufaa za Mikoa ” amesema.

Suala lingine ni Kiswahili kuwa lugha rasmi ya mahakama katika kuandika sheria na kutoa hukumu na kazi mbalimbali za Mahakama, pia Tanzania kuwa nchi ya kwanza kwa Afrika Mashariki kutoa msaada wa huduma za kisheria kwa makosa ya kijinai na masuluhishi mbalimbali.

“Katika hili hivi sasa kila Halmashauri ya Wilaya hapa nchini wanae msajili msaidizi wa haki za binadamu ambapo kwa sasa tunawasajili 209 kwa Tanzania nzima katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kisheria” Prof.Kabudi

Kuhusu haki ya kupata habari amesema katika ripoti hiyo wameonyesha kuwa mpaka hivi sasa wananchi wanapata habari za kila aina kutoka vyombo mbalimbali ambapo Magazeti ni 250, Televisioni 44, Radio 198, Online Televisioni 440, Online Radio 23, na Blog 120, vyombo vyote hivi vikitoa habari za aina mbalimbali.

Ameongeza kuwa “Pia tumeeleza idadi ya wanawake katika vyombo vya maamuzi, ambapo kwa sasa tuna Rais Mwanamke, Naibu Spika mwanamke, vile vile katika Bunge asilimia 36 ni wanawake, katika ngazi za Mahakama za rufaa asilimia 44 ni wanawake, Mahakama kuu asilimia 33, mahakama za hakimu mkazi asilimia 50, asilimia 42.5 katika mahakama za mwanzo na asilimia 40 katika nafasi za wasajili wa mahakama” amesema.

Prof.Kabudi amesema kuwa mambo yote yametekelezwa ikiwa ni katika kuhakikisha haki katika makundi mbalimbali zinapatikana hasa katika kupata huduma za kijamii kwa wananchi wa Tanzania.

 

Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YAIPONGEZA WIZARA KWA UTEKELEZAJI WA MAMA SAMIA LEGAL AID CAMPAIGN

TUFANYE KAZI KWA UADILIFU NA USHIRIKIANO - MHE CHANA