CHETI CHA KUZALIWA NI HAKI YA MTOTO RAIA NA ASIYE RAIA – WAZIRI KABUDI
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akiongea katika hafla ya uzinduzi wa usajili wa watoto chini ya miaka mitano katika mikoa ya Katavi na Rukwa. Hafla hiyo imefanyika katika viwanja vya shule ya msingi Kashatu Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi.Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi akizindua mpango wa usajili wa watoto chini ya miaka mitano katika mikoa ya Katavi na Rukwa.
Waziri Kabudi akitoa vyeti vya kuzaliwa watoto kwa wazazi waliofika katika viwanja vya shule ya msingi Kashatu Mkoani Katavi kusajili watoto wao.
Mkurugenzi wa Idara ya Haki za Binadamu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Nkasori Sarakikya ambaye alikuwa Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria kwenye hafla hiyo akitoa salamu za wizara.
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Cheti cha
kuzaliwa ni haki ya kila mtoto aliyezaliwa Tanzania awe raia au asiwe raia, hii
itasaidia utambuzi wa wananchi na kuwezesha Serikali kupanga mipango ya
maendeleo ipasavyo kulingana na idadi ya wananchi waliopo.
Hayo
yamesemwa na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi wakati wa
hafla ya Uzinduzi wa Mpango wa Usajili wa Watoto wa Umri Chini ya Miaka Mitano
ulioambatana na utoaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto hao katika Mikoa ya
Katavi na Rukwa uliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Kashatu Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi tarehe 24,
Novemba, 2021.
Waziri
Kabudi ambaye alikuwa mgeni rasmi katika
uzinduzi huo, amesema Serikali imechukua hatua madhubuti na kufanya maboresho ya sheria,
rasilimali fedha pamoja na wataalam wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
TEHAMA kwa lengo la kuharakisha
upatikanaji wa huduma za usajili wa matukio muhimu ya binadamu ikiwemo vizazi
kwa watoto wa umri chini ya miaka mitano.
“Usajili wa matukio muhimu ya binadamu
hufanyika duniani kote ili kufahamu taarifa sahihi na kupanga mipango bora ya
kuhudumia wananchi” alisema Prof. Kabudi.
Wakati
huohuo Waziri Kabudi ametoa maagizo kwa
viongozi wa Mikoa inayopakana na nchi jirani wasimamie zoezi hilo kwa ufanisi
ili watoto wanaostahili kusajiliwa tu ndio wasajiliwe na kupatiwa vyeti vya
kuzaliwa huku akisisitiza Kamati za
Ulinzi na Usalama zishirikishwe katika kila hatua ya zoezi hilo na kwamba
udanganyifu wowote wa taarifa ni kosa kisheria na atakayefanya hivyo atachukuliwa
hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kifungo.
Kwa upande
wake Mwenyekiti wa Bodi ya ya ushauri ya Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini
(RITA) Prof. Hamis Dihenga amesema
usajili wa watoto wanaozaliwa ni muendelezo wa usajili wa matukio muhimu ya
binadamu na kwamba itawezesha upatikanaji wa takwimu sahihi na kwa wakati
badala ya kutegemea Sensa na makisio katika upangaji wa mipango ya maendeleo.
Aliongeza
kuwa kabla ya kampeni hii kuanza kwa Mkoa wa Katavi asilimia 6.3 na Rukwa
asilimia 5.8 ya watu ndiyo wamesajiliwa
hivyo baada ya wiki mbili za kampeni hii tunategemea watoto ambao
hawajasajiliwa watakuwa wamesajiliwa kwa asilimia 100 Kwani kupitia zoezi hili
la usajili wazazi au walezi wenye watoto
wa kundi hilo hawatotozwa gharama yoyote ya malipo ya huduma ya usajili na kupatiwa cheti cha kuzaliwa kwani
tayari serikali kwa kushirikiana na wadau na mashirika ya maendeleo ya
Kimataifa wameshagharamia.
“ Mpango huu umerahisisha upatikanaji wa
kuduma kwani vyeti hivyo vinatolewa katika ofisi za kata na vituo vya tiba
vinavyotoa huduma ya mama na mtoto pamoja na matumizi ya Teknolojia ya Habari
na Mawasiliano imesaidia kurahisisha
taarifa kutoka katika vituo vya usajili kutumwa moja kwa moja hadi kwenye kanzidata ya RITA Makao Makuu’’..Alisema Prof.
Dihenga
Nae Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na
Sheria Bi. Nkasori Sarakikya alitoa salamu za Wizara kwa kuipongeza RITA kwa
kuwezesha watoto kupata haki yao ya kupatiwa vyeti vya kuzaliwa na kuwasihi wananchi
wa Katavi na Rukwa kutumia fursa hiyo ipasavyo.
“Vyeti vya
kuzaliwa ni ufunguo wa maendeleo kwa watoto kwa kuwa vinahitajika katika hatua
muhimu za binadamu hivyo tuwasajili watoto wetu” alisema Bi. Sarakikya
RITA kupitia
Wizara ya katiba na sheria inatekeleza na kusimamia mpango huo wa usajili wa
watoto wa umri chini ya miaka mitano na mpaka sasa tayari Mikoa 22 inatekeleza
mpango huo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo,Ofisi ya Rais
TAMISEMI, Idara ya Uhamiaji, Wizara ya Afya Ustawi wa Jamii Wazee na Watoto,
Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA) na wadau wa maendeleao Shirika la
kuhudumia watoto Duniani UNICEF, Shirika la maendeleo la Canada na kampuni ya
simu za mkononi Tigo.
Comments
Post a Comment