UTOAJI HAKI UZIDI KUIMARISHWA HASA KWA WASIO NA UWEZO ASEMA PROF. KABUDI
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akiongea na watumishi wa Mkoa wa Katavi (hawapo pichani) alipotembelea ofisini hapo kabla ya kufanya ziara katika mahakama za hakimu mkazi katavi, wilaya ya mpanda na wilaya ya Tanganyika.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akisalimiana na watumishi wa Mahakama alipotembelea Mahakama ya Hakimu Mkazi Katavi na Mahakama ya Wilaya Mpanda.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akisisitiza jambo katika ziara hiyo.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi akitoa ushauri wakati akikagua ujenzi wa mahakama ya Wilaya Tanganyika.Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi asisitiza
kuzingatiwa kwa lengo la Rais la kuimarisha utoaji haki hasa kwa watu wa
vijijini ambao wengi wao hawana uwezo.
“Lengo la Rais ni kuimarisha utoaji haki hasa kwa watu wa
vijijini wasio na uwezo wa kuwalipa Mawakili” alisema.
Waziri Kabudi aliyasema hayo wakati akiongea na Mkuu wa Mkoa
wa Katavi Mhe. Mwanamvua Mrindoko na kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa Katavi
wakati alipomtembelea Mkuu wa Mkoa huyo ofisini kwake kabla ya kufanya ziara ya
kukagua mahakama za Hakimu Mkazi Katavi, Mahakama ya Wilaya Mpanda na kukagua
ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Tanganyika.
Aliongeza, kwa kuwa Mawakili hutoza gharama katika kazi zao na
hivyo kutegemewa zaidi na watu wa mijini, serikali inaangalia namna ya
kuboresha kazi za wasaidizi wa kisheria kwa kuwapatia elimu ili waweze kufanya
kazi zao kwa ufanisi zaidi na kuwasaidia
watu hasa wa vijijini wasio na uwezo wa kulipa mawakili.
Alisisitiza, mahakama mbalimbali zinaendelea kujengwa ikiwemo
mahakama ya Wilaya ya Tanganyika iliyopo Mkoani Katavi na mahakama za mwanzo
nchini kote lengo likiwa ni kusogeza huduma ya utoaji haki karibu zaidi kwa
wananchi na kuwawezesha kupata haki kwa wakati.
Waziri Kabudi alisema katika kuwapatia haki wananchi huduma
za utoaji haki zimeimarishwa kwani kwa sasa mahakimu wenye shahada wameanza kufanya
kazi katika ngazi ya mahakama za mwanzo na Mawakili pia wameruhusiwa kufanya
kazi katika Mahakama hizo.
Aidha, Prof. kabudi alipongeza utendaji kazi wa Mahakama za
Hakimu Mkazi Katavi na Mahakama ya Wilaya Mpanda kwa kutoa vifungo vya nje kama
adhabu mbadala kwa wafungwa 32 wanaotumikia adhabu hiyo kwa sasa ikiwa na lengo
la kupunguza msongamano magerezani.
Comments
Post a Comment