MABORESHO YA HAKI JINAI KUTATUA CHANGAMOTO ZA UPATIKANAJI HAKI – HOMERA
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera akizungumza katika ufunguzi wa Wiki ya Msaada wa Kisheria.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Zuberi Homera ( wa pili kushoto) akifurahia jambo wakati akipata maelezo kutoka kwa Wakili George Mollel (wa tatu kulia) alipotembelea banda la Wizara ya Katiba na Sheria kabla ya kuzindua rasmi Wiki ya Msaada wa Kisheria inayofanyika kitaifa Mkoani Mbeya.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe Juma Homera akipata maelezo alipotembelea banda la Haki za Binadamu.
Wananchi wakipata huduma katika mabanda mbalimbali katika viwanja vya Ruandanzovwe jijini Mbeya kwenye maonyesho ya Wiki ya Msaada wa Kisheria.
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera amesema maboresho ya
haki jinai yatasaidia kutatua changamoto za upatikanaji haki.
Mhe. Homera ameyasema hayo wakati akizindua Wiki ya Msaada
wa Kisheria yanayofanyika kitaifa Mkoani Mbeya.
Alisema, “pamoja na utoaji wa msaada wa kisheria katika maeneo ya vizuizi
ambayo hufanywa na wadau mbalimbali wakiratibiwa na Wizara ya Katiba na Sheria,
bado zipo changamoto za ucheleweshaji wa upelelezi, ucheleweshaji wa mashauri
mahakamani, mlundikano wa wafungwa na mahabusu magerezani, uchache wa watoa
huduma ya msaada wa kisheria na mengi yanayokwamisha utolewaji wa haki kwa
wakati hivyo inahitajika
maboresho ya mfumo wa haki jinai ili kupunguza changamoto nilizozitaja”.
Aliongeza anafahamu
kuwa yapo maboresho mengi sana
yaliyofanywa na Serikali katika mfumo wa haki jinai ikiwemo kutenganisha
shughuli za upelelezi na uendeshaji wa mashtaka na Ofisi za Mkurugenzi wa Mashtaka
kufunguliwa katika Mikoa yote Tanzania Bara. Jambo hili limewezesha huduma za
mashtaka kufanywa na Mawakili wa Serikali tofauti na hapo awali lilipokuwa
linafanywa na waendesha mashtaka wa Jeshi la Polisi. Pamoja na kupungua kwa
ubambikaji wa kesi, ofisi hizi bado hazijaenea katika Wilaya zote nchini ili
kuondoa kabisa changamoto na mtu mmoja kukamata, kupepeleza na kuendesha
mashtaka, jambo ambalo ni mgongano wa kimaslahi.
Alifafanua kuwa, Sambamba na hilo Sheria
mbalimbali zilifanyiwa marekebisho ili kushughulikia mashauri ya jinai kwa
wakati na kupunguza misongamano ya mahabusu na wafungwa magerezani. Marekebisho
hayo yaliweka utaratibu wa kuingia makubaliano ya maungamo ili kupata nafuu ya
adhabu, kufifisha makosa na kulipa faini zilizowekwa kwenye makosa hayo bila
shtaka kwenda mahakamani; usuluhishi katika makosa ya jinai kwa makosa yenye
kifungo kisichozidi miaka mitatu; uwemo wa majukwaa ya haki jinai kila Mkoa na
Wilaya ili kutatua changamoto za masuala ya jinai; matumizi ya adhabu mbadala
ikiwemo vifungo vya nje na kufanya kazi za jamii. Aidha, kutokana na
ucheleweshaji uliopo kwenye makosa mengi ya Jinai, Mkurugenzi wa Mashtaka
ametoa mwongozo wa kutokufungua baadhi ya kesi mahakamani hadi kwanza upelelezi
wake ukamilike. Haya yote ni kuhakikisha kauli ya Mhe. Mama Samia Suluhu
Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kupunguza mlundikano wa
mashauri mahakamani na misongamano mahabusu na wafungwa magerezani kwa mashauri
yasiyo na tija inatekelezwa.
Naye Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya
Katiba na Sheria Bw. Dunstan Shimbo alisema Wizara itaendelea kushirikiana na
wadau katika kuhakikisha sheria ya msaada wa kisheria inatekelezwa ili
kuendelea kutatua kero ya upatikanaji haki kwa wananchi, pia wizara inaendelea
kutoa elimu kwa watoa msaada wa kisheria ili waweze kufanya kazi hiyo kwa
ufanisi.
Aidha, Mwakilishi
wa Msajili wa Watoa Msaada wa Kisheria Bi. Ester Msambazi amesema Yapo maboresho mengi ambayo
yamefanyika katika sekta ya jinai ambayo yanalenga kutoa haki kwa wakati.
Maboresho haya yanajumuisha sheria na taratibu za kushughulikia mashauri ya
jinai ikiwa ni pamoja na matumizi ya adhabu mbadala zikiwemo faini na vifungo
vya nje.
Alisema, ”Tunafahamu kuwa vyombo vyetu vya
utoaji haki vinafanya kila liwezekanalo kupunguza msongamano Magerezani. Hata
hivyo, ziko tafsiri potofu miongoni mwa wananchi kuwa kila mhalifu ni lazima
afungwe gerezani. Wapo wananchi wanaoamini kuwa adhabu halali ni kifungo. Hii
inasababisha matumizi ya vifungo mbadala kutotumika na kwa kuhofia kuonekana
kuwa wamepokea rushwa. Hili ni jambo linaloturudisha nyuma kama sekta ya haki”
Aliongeza,”Kwa kutambua hilo, wadau wa
msaada wa kisheria wameamua kuufahamisha umma kuwa matumizi ya adhabu mbadala
ni halali kisheria na ni vema kutumia njia hizo kwa manufaa ya Taifa. Manufaa
ya Taifa yanatokana na ukweli kwamba wafungwa wanapopewa kifungo cha nje
wanapata fursa ya kujihusisha na kazi za kiuchumi kwa manufaa ya familia zao na
za Taifa kwa ujumla”.
Maadhimisho
haya yanaratibiwa na kusimamiwa na Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria
na kwa mwaka huu ni mara ya tano kufanyika tangu kuanzishwa kwake.
Comments
Post a Comment