KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA KATIBA YARIDHISHWA NA UJENZI MAKAO MAKUU YA MAHAKAMA


 Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. George Simbachawene akielezea jambo kwa Kamati ya kudumu ya Bunge ilipotembelea ujenzi wa Majengo ya Makao  Makuu ya Mahakama eneo la Tambukareli jijini Dodoma leo (14/2/22).


Mtendaji Mkuu wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel akitoa maelezo ya ujenzi wa majengo ya Makao Makuu ya Mahakama kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ilipotembelea kujionea ujenzi huo unaoendelea eneo la Tambukareli jijini Dodoma.


Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. George Simbachawene (kushoto) akibadilishana mawazo na Katibu Mkuu Bi. Mary Makondo (kulia) na Mtendaji Mkuu wa Mahakama Prof. Elisante Ole Gabriel wakati wakiwasubiri wageni wao ambao ni Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba walipotembelea ujenzi wa majengo ya Makao Makuu ya Mahakama jijini Dodoma.


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba Dkt. Joseph Mhagama akitoa shukran na kueleza kuridhishwa kwao na namna ujenzi unavyoendelea.


XXXXXXXXXXXXX

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria imeridhika na maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania unaoendelea eneo la Tambukareli jijini Dodoma.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dkt. Joseph Mhagama kwa niaba ya wajumbe wenzake wakati wa ziara yao ya siku moja ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa majengo matatu ya Mahakama.

Amesema kuwa wamefurahishwa na kazi kubwa ambayo imekwishafanyika katika kusimamia na kuutekeleza mradi huo kwa kiwango cha hali ya juu.

Dkt. Mhagama ameongeza kuwa kupitia mradi huo ambao unatokana na fedha zilizotolewa na Serikali inaonyesha dhamira ya dhati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, alivyokusudia ili miguu ya Mihimili yote ya Serikali iwe pamoja jijini Dodoma.

Aidha, Kamati hiyo imeridhika na hatua zinazochukuliwa za kuzingatia usalama wa wafanyakazi wanaotekeleza kazi kwenye mradi na utoaji fursa kubwa za ajira nyingi kwa watumishi ambao ni raia wa Kitanzania.

Naye Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe George Simbachawene amesema maendeleo ya ujenzi huo ni kielelezo na alama kuwa Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuhakikisha itatimiza ndoto za siku nyingi za kutaka mihimili yote ya Serikali iwe katika makao Makuu ya Nchi jijini Dodoma.

Amesema mihimili mingine kama vile Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali tayari imeshahamia Dodoma na kukamilika kwa Jengo la Mahakama mihimili yote itakuwa pamoja Dodoma.

“Pongezi tunazitoa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuuwezesha muhimili wa Mahakama kifedha ili nao uweze kuhamia Dodoma, hatua hiyo itaifanya Dodoma kuwa Capital City ya Tanzania kwa vitendo” amesisitiza.

Wakati huo huo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel amesema Mahakama ya Tanzania inatarajia kuhamia Dodoma mwaka huu baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa ujenzi wa majengo ya Mahakama.

Prof. Elisante alitoa kauli hiyo wakati akitoa maelezo ya maendeleo ya ujenzi wa majengo makubwa matatu ya Mahakama kwa Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria iliyotembelea mradi huo kukagua shughuli mbalimbali zinazotekelezwa.

Amesema majengo hayo ambayo hadi kukamilika yataragharimu kiasi cha shilingi bilioni 129.7 ambazo ni fedha zinatokana na mapato ya ndani ya fedha za Serikali.

Prof. Gabriel amesema ujenzi huo ambao utakuwa na jengo la Mahakama Kuu, Mahakama ya Rufaa na Mahakama ya Juu (Supreme Court) upo katika hatua nzuri ambapo kazi kubwa zimekamilika kwa asilimia kubwa.

Ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiwezesha Mahakama katika miradi mbalimbali ukiwemo huo kwa kutoa fedha kwa wakati jambo lililowafanya kasi ya ujenzi kuwa nzuri.

Kwa upande wa Msanifu Majengo kutoka Kampuni ya Arqes Afrika ambaye ndiye aliyechora michoro ya majengo hayo Rose Nestory amesema kuwa majengo hayo yatakuwa na Sakafu tisa na kutakuwepo na ukumbi wenye uwezo wa kuchukua watu 300 kwa wakati mmoja.

Amesema ujenzi wa majengo hayo umezingatia sehemu ya kuendeshea shughuli za Mahakama, Ofisi za Utawala na huduma nyingine.

Rose amesema katika eneo hilo kutakuwepo na Migahawa, Uwanja wa kutua Helkopta, Uwanja wa kuendeshea wiki ya Sheria na kujenga viwanja vya michezo na huduma nyingine muhimu kwa ajili ya wadau wa Mahakama.


Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YAIPONGEZA WIZARA KWA UTEKELEZAJI WA MAMA SAMIA LEGAL AID CAMPAIGN

TUFANYE KAZI KWA UADILIFU NA USHIRIKIANO - MHE CHANA