"HUKUMU ZINAZOTOLEWA MAHAKAMANI ZITEKELEZWE KWA WAKATI" WAZIRI SIMBACHAWENE


 Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. George Simbachawene akizindua ripoti ya wadau ya upatikanaji haki baada ya kufungua Kongamano la Msaada wa Kisheria la mwaka 2022. Wengine pichani ni Mkurugenzi wa kitengo cha  Msaada wa Kisheria ambaye pia ni Msajili wa Watoa Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Felistas Mushi (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Huduma za Kisheria Bi. Lulu Ng'w'anakilala.

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. George Simbachawene akipata maelezo kutoka kwa Wakili Neema Ahmed ambaye ni Mratibu wa TAWLA Mkoani Dodoma kabla Waziri Simbachawene hajafungua Kongamano la Msaada wa Kisheria linalofanyika jijini Dodoma.


Wakili wa Serikali Bi. Lilian Kilembe akitoa huduma kwa mteja Bw. Benjamin Sembelu aliyefika kwenye banda la Wizara hiyo ili kupata msaada wa Kisheria wakati wa Kongamano la Msaada wa Kisheria jijini Dodoma.

XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Waziri wa Katiba na Sheria George Simbachawene ataka kesi zilizotolewa maamuzi na mahakama maamuzi hayo yaheshimiwe na yafuatwe kwani kwani yasipotekelezwa yanashikilia uchumi wa watu.

Alisema "Hukumu zilizotolewa na hazijatekelezwa zinashikilia uchumi wa watu kwani wananchi wanashindwa kuendelea na shughuli zao kwa kusubiri utekelezwaji wa hukumu hizo, natamani Mkurugenzi wa watoa huduma ya msaada wa kisheria kutumia wadau wa kongamano hili kuona namna ya kutatua tatizo hili".

Mhe. Simbachawene aliyasema hayo wakati akifungua Kongamano la Msaada wa Kisheria la mwaka 2022 linalofanyika kwa siku mbili jijini Dodoma.

Aidha,Waziri Simbachawene alisema Wizara kwa kushirikiana na Mahakama imeweza kuweka utaratibu wa upatikanaji wa huduma ya msaada wa kisheria katika Madawati ya Msaada wa Kisheria yaliyopo katika Vituo Jumuishi vya Mahakama. Hii ni hatua kubwa katika kusogeza huduma kwa mwananchi asiyekuwa na uwezo ili anapokutana na suala linalohitaji ufafanuzi, maelekezo au ushauri aupate palepale katika maeneo ya Mahakama.

Alisema, "Ninafahamu kwamba, upo mpango unaoratibiwa na Mhimili wa Mahakama wa kuweka vyumba vya msaada wa kisheria katika majengo yote mapya ya Mahakama Kuu. Nitumie fursa hii kuwasihi watoa huduma ya msaada wa kisheria nchini washirikiane na Mahakama katika kuhakikisha juhudi hizi za Mhimili zinazaa matunda kwanza kwa kutumia fursa hiyo na pili kuwaelimisha wananchi kuhusu upatikanaji wa huduma hiyo katika maeneo ya Mahakama. Hii itasaidia wananchi wengi wanapopata nakala za hukumu Mahakamani kueleweshwa pale pale Mahakamani tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo mwananchi alihitaji kutafuta Wakili au wanasheria nje ya mahakama ambao wangempatia tafsiri hiyo hiyo au kupotosha. Aidha, itasaidia mwenye fursa ya kukata rufaa kufanya hivyo ndani ya muda kwani atakuwa ameshauriwa mapema". 

Awali akimkaribisha Waziri Simbachawene kufungua Kongamano hilo, Msajili wa watoa huduma ya msaada wa kisheria alisema "lengo la kukutana kama wadau wa utekelezaji wa sheria ya Msaada wa kisheria ni kutathmini wapi tulipotoka na tunapokwenda.

Aliongeza "kupitia mada tulizopata tumeona tumepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa sheria hii ya msaada wa kisheria".

Kauli mbiu ya Kongamano hilo ni 'Msaada wa Kisheria kwa jamii yenye haki na Jumuishi', pia kongamano hilo limeshirikisha wadau mbalimbali wa Msaada wa kisheria kutoka Tanzania Bara na Visiwani.

Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YAIPONGEZA WIZARA KWA UTEKELEZAJI WA MAMA SAMIA LEGAL AID CAMPAIGN

TUFANYE KAZI KWA UADILIFU NA USHIRIKIANO - MHE CHANA