DKT. KAZUNGU AFUNGUA KIKAO KAZI CHA KUHAKIKI RASIMU YA MPANGO KAZI WA PILI WA KITAIFA WA HAKI ZA BINADAMU


                                     xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx



Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Khatibu Kazungu amefungua Kikao Kazi cha kuhakiki Rasimu ya Mpango Kazi wa Pili wa Kitaifa wa Haki za Binadamu leo tarehe 10 Mei, 2022, Jijini Dar es Salaam.

Madhumuni ya Mpango Kazi wa Kitaifa wa Haki za Binadamu ni pamoja na kuwa na mwongozo kwenye masuala ya haki za binadamu na haki za watu.

“Mpango kazi huu una malengo ya kukuza, kulinda na kuheshimu haki za binadamu na watu na hatimae kuleta tija katika maendeleo ya watu na nchi.” alisema Dkt. Kazungu

Mpango Kazi wa Kitaifa wa Haki za Binadamu ni mwitikio wa mapendekezo yaliyotolewa na Mkutano wa Dunia kuhusiana na Haki za Binadamu uliofanyika huko Vienna mwaka 1993 "Vienna Declaration and Program of Action"

Kikao hiki kimehudhuriwa na wawakilishi wa Asasi za Kiraia na Watetezi wa Haki za Binadamu kutoka Tanzania Bara na Tanzania Visiwani kwa lengo la kupitia rasimu ya Mpango kazi wa pili wa Kitaifa wa Haki za Binadamu na kutoa maoni ya kuboresha Mpango Kazi huo.

Hatua hii ya kutoa maoni ni awamu ya pili ya kukamilisha uandaaji wa Mpango Kazi. Mpango unaandaliwa kwa kuzingatia hatua tano; hatua zingine ni Uandaaji, Utekelezaji, Ufuatiliaji na hatua ya mwisho ni kufanya tathmini. Wakati Wizara ya Katiba na Sheria inaratibu uandaaji na utekelezaji wa Mpango kazi huu, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora itakuwa inafanya tathmini na ufuatiliaji.

Dkt. Kazungu ameyataja masuala yafuatayo kama vipaumbele kwenye Mpango; Haki za Kiraia na Kisiasa; Haki za Kiuchumi, Kiutamaduni na Kijamii (elimu, afya na maendeleo); Haki za Makundi Maalum (Watoto, wanawake, watu wenye ulemavu na wazee)

 

 

Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YAIPONGEZA WIZARA KWA UTEKELEZAJI WA MAMA SAMIA LEGAL AID CAMPAIGN

TUFANYE KAZI KWA UADILIFU NA USHIRIKIANO - MHE CHANA