WAZIRI NDUMBARO AKIWASILISHA BUNGENI HOTUBA YA MAKADIRIO YA BAJETI YA MWAKA 2022/2023
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
Waziri wa Katiba na
Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amewasilisha Bungeni Mapitio ya Utekelezaji wa
Mpango na Bajeti kwa mwaka 2021/22 na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka
2022/2023.
Akiwasilisha hotuba hiyo Bungeni leo Aprili 28,
2022, Dkt. Ndumbaro alisema mafanikio yaliyopatikana katika Wizara ni pamoja na
kuimarisha mfumo wa utoaji nchini kwa kutumia lugha ya Kiswahili katika
uandishi wa sheria na shughuli za utoaji haki mahakamani; kuongezeka kwa wigo
wa mfumo wa utoaji haki kwa kuwawezesha Mawakili wa Serikali kuanza kutoa
huduma za uwakili katika Mahakama za Mwanzo.
Aidha, Dkt. Ndumbaro alisema Serikali imeimarisha
mfumo wa utatuzi wa migogoro nje ya mahakama kwa kutumia njia mbadala ambazo
ni; majadiliano, maridhiano, upatanishi na usuluhishi; kuendelea na matumizi ya
lugha ya Kiswahili katika shughuli za Mahakama na uandishi wa nyaraka za
kisheria ambao umeongeza uelewa wa sheria kwa wananchi na hivyo kurahisisha
upatikanaji wa haki kwa wakati na kwa gharama nafuu.
Dkt. Ndumbaro aliongezea kuwa kuunganishwa kwa
Mfumo wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini na Mahakama imerahisisha
uhakiki wa amri za Mahakama kupitia njia ya mtandao.
Baada ya majadiliano Bunge limeidhinisha jumla ya
Shilingi 272,768,278,800.00 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na
miradi ya maendeleo.
Comments
Post a Comment