SERIKALI YAITAKA JAMII KUTOA USHIRIKIANO KWENYE VITA DHIDI YA UKATILI WA KIJINSIA KWA WATOTO
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Katibu Mkuu wa Wizara ya
Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo amtoa wito kwa jamii kuwa mstari wa mbele
kupinga unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya watoto. Bi. Makondo ametoa rai hiyo
wakati akizindua Kampeni ya siku 10 za kupinga ukatili dhidi ya watoto leo
tarehe 6 juni 2022, jijini Dodoma.
Kupitia Kampeni hiyo Tume ya
Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa kushirikiana na wadau wa watoto wamehimiza
wazazi, walezi, jamii na wadau wengine kuheshimu haki za watoto na kuwapatia
ulinzi stahiki ili kuepusha vitendo vya ukatili vinavyoendelea katika maeneo
mbalimbali ya Nchi yetu.
Uzinduzi huo ulitanguliwa na
maandamano yaliyohusisha waalikwa wote yakianzia viwanja vya Nyerere Square
hadi zilipo ofisi za Tume eneo la Kilimani.
Kampeni hiyo ni sehemu ya
Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ambayo hufanyika Juni 16 ya kila mwaka,
msingi wake ukiwa ni utetezi wa Haki za Mtoto kama ilivyoelekezwa na Mkataba wa
Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto wa mwaka 1990, unaobainisha kuwa mtoto ana
haki ya kuishi, kulindwa, kuendelezwa, kushiriki na kutobaguliwa.
Kwa mujibu wa Takwimu za Jeshi
la Polisi Tanzania, katika kipindi cha Januari hadi Desemba, 2021 jumla ya
matukio 11,499 ya ukatili dhidi ya watoto yalitolewa taarifa katika vituo
mbalimbali vya Polisi. Mikoa iliyoongoza ilikuwa ni Arusha (808), Tanga (691),
Shinyanga (505), Mwanza (500) na Mkoa wa Kipolisi Ilala (489). Aidha, Makosa
yaliyoongoza kwa idadi kubwa ni ubakaji (5,899), mimba kwa wanafunzi (1,677) na
ulawiti (1,114).
“Imetosha kwa nchi yetu kushuhudia takwimu
kubwa kiasi hiki zikionyesha ukatili wa kijinsia juu ya watoto,” alisema Bi.
Makondo.
Aidha, Bi. Makondo ametoa rai
kwa watendaji wote wa Serikali katika ngazi mbalimbali pamoja na Wadau wa Haki
za Watoto kuunga mkono Kampeni hiyo, kwa sababu inasaidia kuongeza uelewa wa
watu kuhusu haki na ulinzi wa mtoto na hilo si jukumu la Tume pekee bali jukumu
la jamii nzima.
“Ni muhimu kupaza sauti kwa pamoja kukemea
vitendo vya ukatili dhidi ya watoto kutokana na kuongezeka kwa taarifa za
vitendo vya ukatili katika familia na jamii,” alisema.
Kauli mbiu inakayotumika
kwenye Kampeni hiyo ni ile itakayotumika katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa
Afrika ambayo ni “Tuimarishe Ulinzi wa Mtoto; Tokomeza Ukatili Dhidi yake,
Jiandae Kuhesabiwa”.
Kaulimbiu hii inaakisi lengo la kampeni hiyo
la kuhamasisha jamii kushiriki kuimarisha ulinzi wa mtoto na katika kupinga kwa
nguvu zote vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.
Akimkaribisha Mgeni Rasmi,
Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bw. Mohamed
Hamis alisema kwa majonzi kwamba Tume inapinga na kulaani vitendo vya ukatili
kwa watoto.
“hakuna siku ambayo inapita bila Vyombo vya
Habari kuripoti taarifa za ukatili wanaofanyiwa watoto” alisema Bw. Hamis.
Tume imekuwa ikifanya
uchunguzi wa malalamiko mbalimbali yanayohusu uvunjwaji wa haki za watoto na
kubaini kwamba watoto wengi wanakosa ujasiri wa kutoa taarifa za matukio ya
ukatili wanayokutana nayo. Vilevile, baadhi yao wamekuwa wakiyumbishwa na
wanafamilia wasio wema na hivyo kuficha maovu yanayotendeka katika jamii.
Naye Inspekta Yasinta Kayombo
Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto, Polisi Mkoa wa Dodoma aliwasihi watoto
wasiogope kutoa taarifa Dawati la Polisi wanapotendewa ukatili na endapo
watashindwa basi wawambie wazazi, mwalimu wanayemwamini au mtu mzima
wanayemwamini.
Comments
Post a Comment