UENDESHAJI WA MASHAURI UFUATE HAKI – KATIBU MKUU MAKONDO
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Kukosekana usawa na haki katika uendeshaji wa mashauri
kunaweza kusababisha wanaostahili kuipata haki kunyimwa fursa hiyo ama mtu
kupewa haki asiyostahili.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa
Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bw. Issa Ng’imba
wakati akisoma hotuba kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi. Mary Makondo
ya ufunguzi wa kikao kazi cha kuandaa
hadidu rejea za kazi ya tathmini ya hali halisi ya
uendeshaji wa mashauri makubwa ya rushwa. Kikao kazi hicho kimefunguliwa
Juni 21, 2022, Mkoani Singida.
“Suala la usawa na haki katika
uendeshaji wa mashauri ya jinai nchini ni suala la msingi linalowezesha haki
kupatikana kwa kuzingatia matakwa ya Sheria nchini” Bw. Ng’imba alisema.
Aliongeza,
“Wizara imeandaa kikao hiki ili wadau wa haki jinai mjadili kwa kina dhana ya kufanya tathmini ya uendeshaji wa
mashauri makubwa kama inazingatia viashiria vya uhuru na haki sawa”.
Aidha
alisisitiza kuwa kupitia kikao hicho ni matarajio yake kuwa zitaandaliwa hadidu
rejea zitakazotumika na Wizara kuipata Taasisi huru itakayofanya tathmini ya
uendeshaji wa mashauri makubwa ya rushwa nchini.
Vilevile Bw. Ng’imba alitoa
shukrani zake za dhati kwa Serikali ya Uingereza kwa kuendelea kuiunga mkono
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kusaidia juhudi za kupambana na
Rushwa Nchini kupitia mradi wa kujenga uwezo wa Taasisi wa kupambana na rushwa
nchini (BSAAT).
Alisema, “Natambua kuwa ufadhili
unaotolewa kupitia mradi wa BSAAT umeiwezesha Wizara kuendelea kuratibu
maboresho ya Mfumo wa haki Jinai yanayolenga kuimarisha upatikanaji wa Haki
Jinai Nchini kwa kuzingatia Uhuru na
Haki sawa kwa pande zote zinazohusika na mashauri ya jinai nchini”.
Comments
Post a Comment