ALIYOSEMA WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA, DKT. DAMAS NDUMBARO KUHUSU VIPAUMBELE VYA UTEKELEZAJI WA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA KATIKA BAJETI YA MWAKA WA FEDHA 2022/2023

 



XXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

Wizara ya Katiba na Sheria katika mwaka wa fedha 2022/23, Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha bajeti ya jumla ya shilingi 272,768,278,800.00 (Bilioni mia mbili sabini na mbili, milioni mia saba sitini na nane, laki mbili sabini na nane elfu na mia nane) kwa ajili ya Wizara na Taasisi zake ili kuiwezesha Wizara kutekeleza majukumu yake. 

Katika mwaka wa fedha 2022/2023 bajeti imeongezeka kwa asilimia 18 ya bajeti iliyopitishwa katika Mwaka wa Fedha 2021/22. 

Aidha, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Wizara na Taasisi zake itaendelea kuboresha utoaji wa huduma za kisheria kwa Umma ili kuendana na Dhima ya Wizara inayosema kuwa na mfumo madhubuti wa Kikatiba na Sheria wenye kufanikisha utekelezaji wa sera na mipango kwa maendeleo ya Taifa. 


Vipaumbele ambavyo Wizara imepanga kutekeleza Mwaka wa Fedha 2022/23 ni pamoja na;* 

▪️Kuendelea na kuanza kujenga vituo jumuishi vya Taasisi za Sheria nchini; vituo hivi vitamwezesha mwanachi kupata huduma katika jengo moja ambapo wadau wote wa sheria watapatikana hapo. 

▪️Kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala ya kikatiba na utawala wa sheria; hii itasaidia wananchi kuwa na uelewa mpana wa Katiba na kuelewa umuhimu wake katika kupata haki zao. 

▪️Kuendelea kuhamasisha matumizi ya njia mbadala za utatuzi wa migogoro ambazo ni usuluhishi, upatanishi, maridhiano na majadiliano ili kurahisisha na kuharakisha upatikanaji wa haki nchini; hii itawezesha kupunguza mlundikano wa kesi mahakamani na kuokoa muda kwa wananchi kuhudhuria mahakamani mara kwa mara. 

▪️Kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa huduma ya msaada wa kisheria nchini; kupitia wasaidizi wa kisheria na watoa huduma za msaada wa kisheria.

▪️Kutekeleza Programu ya Kutumia Lugha ya Kiswahili katika utoaji haki nchini; hii itaongeza uelewa kwa wananchi juu ya haki zao pale wanapotaka kushtaki, kushtakiwa au kupata uelewa juu ya haki zao. 

▪️Kuendelea kuimarisha usajili wa matukio muhimu ya binadamu na takwimu pamoja na shughuli za ufilisi na udhamini; usajili huu utafanikisha utambuzi wa mtu mmoja mmoja pale mwananchi anapopatiwa cheti cha kuzaliwa pia nchi itapata takwimu sahihi za mtiririko wa hali za ndoa na talaka. 

▪️Kuimarisha Taasisi ya Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) kuwa ya kidijitali ili kuunganisha RITA na taasisi nyingine kama vile NIDA na ANUANI ZA MAKAZI.

▪️Kuharakisha utatuzi wa mashauri ya kawaida na mkakati wa kumaliza mashauri ya muda mrefu, hii itasaidia mwananchi kupata haki yake kwa wakati na kumpa nafasi ya kuendelea kufanya shughuli zake za maendeleo. 

▪️Kuendelea kutekeleza mpango wa ujenzi na ukarabati wa Majengo ya Mahakama katika ngazi mbalimbali; itampunguzia mwananchi kutembea umbali mrefu kwa ajili ya kupata huduma ya kimahakama na kuweza kupata haki zake. 

Utekelezaji wa vipaumbele hivyo utahusisha utekelezaji wa mikakati mbalimbali ikiwemo, kuendelea kutoa elimu kwa Umma kuhusu Katiba na Sheria kupitia vyombo mbalimbali vya habari pamoja na kushirikisha Asasi za Kiraia ili kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu haki na wajibu wao katika kupata haki zao na Kuendelea kuboresha na kufungamanisha mifumo ya utoaji haki kwa vyombo vya utoaji haki nchini. 

Niwakumbushe wadau wote wa sekta ya sheria kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika tarehe 23 Agosti, 2022. 

Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YAIPONGEZA WIZARA KWA UTEKELEZAJI WA MAMA SAMIA LEGAL AID CAMPAIGN

TUFANYE KAZI KWA UADILIFU NA USHIRIKIANO - MHE CHANA