SERIKALI MEZANI NA VYOMBO VYA USHAURI VYA UNESCO, WAJADILI KUHUSU MAENEO YA URITHI WA DUNIA
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro ameongoza timu ya
wajumbe kutoka Tanzania waliohudhuria kikao cha pamoja na UNESCO katika
Kituo cha Urithi wa Dunia kilichohusisha pia vyombo vya ushauri vya UNESCO
yaani IUCN, ICOMOS na ICCROM. Kikao hicho kilifanyika tarehe 13 Julai 2022,
Paris Ufaransa.
Katika kikao hicho, ujumbe wa Tanzania umeeleza na kujibu hoja
mbalimbali zinazohusu hatua shirikishi za Serikali za kuwaomba na kuwalipa
fidia jamii zilizokuwa zinaishi Ngorongoro kisha kuhamia kijiji cha Msomera
Wilaya ya Handeni ili kuondoa changamoto za Uhifadhi wa eneo la Ngorongoro
zilizosababishwa na uwepo wa idadi kubwa ya binadamu na mifugo ndani ya eneo la
hifadhi, hatua ambayo itaboresha Ikolojia ya eneo hilo na Utalii.
Kwa upande wa Mji Mkongwe wa Zanzibar mazungumzo yalijikita katika
Uhifadhi na Maendeleo bila kuathiri Urithi wa Utamaduni. Eneo la Hifadhi
ya Ngorongoro na Mji Mkongwe wa Zanzibar ni miongoni mwa maeneo Saba ya
Tanzania kwenye Orodha ya Urithi wa Dunia unaolindwa na Mkataba wa UNESCO wa
1972.
Dkt. Ndumbaro amekitaarifu kituo cha Urithi wa Dunia cha UNESCO kuwa
Tanzania imefanya kila jitihada kulinda maeneo hayo ya urithi wa Dunia kwa
kuzingatia maelekezo ya Mkataba wa UNESCO wa Urithi wa Dunia wa 1972
pamoja na Sheria za ndani ya nchi yetu na za kimataifa. Aidha, Dkt. Ndumbaro
amebainisha changamoto zinazojitokeza ni kutokana na upotoshaji unaofanywa ili
kuwapotosha wananchi na kuchelewesha utekelezaji wa mipango ambayo ina maslahi
mapana kwa wananchi husika, nchi yetu na dunia kwa ujumla.
Ujumbe wa Tanzania pia umepokea ushauri wa kituo cha UNESCO cha Urithi
wa Dunia na majadiliano yanaendelea juu ya namna bora ya kulinda na kuhifadhi
Urithi wa Dunia.
Pamoja na Waziri Mhe. Ndumbaro, Serikali ya Tanzania imewakilishwa
na Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Eliamani Sedoyeka, Katibu
Mkuu Wizara ya Urithi na Utalii Zanzibar, Bi. Fatma Mabrouk Khamis, Mh. Balozi
Samuel Shelukindo ambae ni Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa na Mwakilishi wa
Kudumu UNESCO.
Aidha walikuwepo Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Prof. Hamisi Malebo na Bw. Erick Kajiru, Afisa
Programu Mkuu katika Tume ya Taifa ya UNESCO ambaye pia ni Mratibu wa Masuala
ya Urithi wa Dunia nchini. Wengine katika ujumbe wa Tanzania ni Kaimu Mhifadhi
Mkuu wa NCAA Dkt. Christopher Timbuka, Bw. Joshua Mwankunda ambae ni Mhifadhi
Mwandamizi wa NCAA na Mhandisi Musa Aweso kutoka Mamlala ya Mji Mkongwe wa
Zanzibar.
Kwa upande wa UNESCO iliongozwa na Ndg. Lazare Eloundou Assomo,
Mkurugenzi wa Kituo cha Urithi wa Dunia, UNESCO.
Comments
Post a Comment