WAZIRI NDUMBARO ATAKA KASI YA UJENZI JENGO LA WIZARA IONGEZWE
Waziri wa Katiba na Sheria Dk. Damas Ndumbaro, akitoa maelekezo kwa wasimamizi wa mradi wa ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Wizara hiyo mara baada ya kufanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi huo katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma Juni 30, 2022.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas
Ndumbaro aagiza kasi ya ujenzi wa Jengo la Wizara ya Katiba na Sheria
linaloendelea kujengwa katika mji wa Serikali Mtumba Jijini Dodoma iongezwe ili
jengo likamilike kwa wakati.
Agizo hilo amelitoa leo tarehe 30/06/2022
wakati Waziri Ndumbaro alipofanya ukaguzi wa ujenzi wa jengo hilo.
Waziri Ndumbaro amesema “Tumekagua na tumeona
kazi inavyoendelea lakini hairidhishi, nasisitiza Mkandarasi ongeza kasi ya
ujenzi na Mshauri Mwelekezi ongeza usimamizi”
Aidha, Waziri Ndumbaro alimuagiza Meneja wa
mradi, Mkandarasi na Mshauri Mwelekezi kufikia tarehe 06, Julai, 2022
wawasilishe kwa Katibu Mkuu wa Wizara taarifa inayoelezea ni lini jengo hilo
litakabidhiwa kwa Wizara na kama kuna maombi ya kuongezewa muda waeleze wanataka
kuongezewa muda kiasi gani na sababu za kuongezwa muda.
Vilevile kutokana na umuhimu wa mradi huo
Waziri Ndumbaro amemuagiza Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Geophrey Pinda
kukagua maendeleo ya ujenzi huo mara moja kila mwezi ili kuhakikisha ujenzi
unaenda kwa kasi na kwa viwango.
Naye, Naibu Waziri Mhe. Geophrey Pinda
alimtaka Mkandarasi kuongeza vibarua ili kazi iweze kukamilika kwa wakati na
kama kuna changamoto za utekelezaji wa mradi basi zielezwe mapema ili kuona
namna ya kuweza kuzitatua na zisikwamishe utekelezwaji wa mradi.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi
huo Mratibu wa Majengo ya Serikali Bw. Meshack Bandawe alisema kwa ujumla
ujenzi unaendelea vizuri na ameipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuwa ni
moja ya Wizara zinazofanya vizuri katika ujenzi huo na amemsisitiza Mkandarasi
kuongeza vifaa na vibarua ili kuweza kukamilisha kazi kwa wakati.
Comments
Post a Comment