WAZIRI NDUMBARO AZINDUA RASMI KIKOSI KAZI CHA ULINZI KWA WATOTO DHIDI YA BIASHARA YA USAFIRISHAJI HARAMU WA BINADAMU
XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX
Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro amezindua rasmi kikosi
kazi cha Ulinzi wa watoto dhidi ya biashara ya Usafirishaji haramu wa
binadamu, hafla hiyo ya uzinduzi imefanyika leo tarehe 21 Julai, 2022
Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wadau kutoka katika taasisi na sekta
mbali mbali.
Dkt. Ndumbaro amesema Wizara ya Katiba na Sheria ndiyo
Wizara inayoshughulikia haki za binadamu hivyo siku ya leo ni siku
muhimu Sana katika historia ya haki jinai.
"Uhalifu huu ni mkubwa sana, ni uhalifu wa kupanga na wa kimataifa,
na uko maeneo makubwa, umevuka mipaka, wanasafirisha watoto hususani
wasichana." alisema Dkt. Ndumbaro.
Aidha, Waziri Ndumbaro amesema mradi huu ni wa miaka minne na kikosi
kazi hiki kitajengewa uwezo kuhakikisha kinakabiliana na wahalifu kwa
vitendo na kwa kila namna, amesema jukumu la kikosi kazi hiki ni
kuwashughulikia wahalifu pamoja na kuhakikisha wahalifu wanaohusika,
mkono wa Sheria unachukua nafasi yake.
Dkt. Ndumbaro ameagiza kikosi kazi hicho kutoa ulinzi na uhifadhi kwa
waathirika wa vitendo hivyo ikiwemo kutoa msaada wa kisaikolojia na elimu
pamoja na kuwalinda watu wote wanaotoa ushahidi.
Pamoja na hayo, Dkt. Ndumbaro ametoa wito kwa Wakurugenzi wa Mashitaka
Tanzania Bara na Zanzibar, kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa asilimia mia
moja, pamoja na kufanya tathmini mara kwa mara kubaini wapi panatakiwa
kufanyiwa marekebisho.
Naye Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum
Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema Wizara yake itakuwa mstari wa mbele kupigania
haki za watoto kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Aidha uzinduzi huo umehudhuriwa na Wadau wa Maendeleo kutoka IOM,
UNICEF, Ubalozi wa Uingereza, Umoja wa nchi za Ulaya pamoja na UNDP, ambao
wamepongeza jitihada za Tanzania katika kupambana na uhalifu mkubwa wa kupangwa
na wameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika vita dhidi ya biashara
ya usafirishaji haramu wa binadamu haswa watoto.
Comments
Post a Comment