DKT. KAZUNGU AWATAKA WADAU WA MAZINGIRA WASHIRIKI KATIKA UPANDAJI NA UTUNZAJI WA MITI KATIKA MAZINGIRA WALIYOPO


 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Khatibu Kazungu akipanda mti katika zoezi la upandaji miti katika Maadhimisho ya Miaka 20 ya Kuanzishwa kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Khatibu Kazungu akiongoza maandamano katika zoezi la upandaji miti katika Maadhimisho ya Miaka 20 ya Kuanzishwa kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Khatibu Kazungu akizungumza katika zoezi la upandaji miti katika Maadhimisho ya Miaka 20 ya Kuanzishwa kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

XXXXXXXXXXXXXX


Naibu Katibu Mkuu wa  Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Khatibu Kazungu amewataka wadau wote wa Mazingira kushiriki katika upandaji na utunzaji wa miti katika mazingira waliyopo ili kutekeleza Mkakati wa Utekelezwaji wa Sera ya Taifa ya Uhifadhi wa Mazingira wa mwaka 2020/21.

Dkt. Kazungu ameyasema hayo wakati wa tukio la upandaji miti ikiwa ni mojawapo ya shughuli za Maadhimisho ya Miaka Ishirini tangu kuanzishwa kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora lililofanyika leo, Septemba 10, 2022 eneo la kwa Swai Nkuhungu, jijini Dodoma.

Dkt. Kazungu alisema moja ya changamoto za uhifadhi wa mazingira nchini ni ukataji miti na uharibifu wa misitu.

‘’Taarifa ya tatu ya mazingira nchini ya mwaka 2019 inaonesha kuwa takriban hekta 469,420 za misitu kwa mwaka hupotea kutokana na utegemezi mkubwa wa nishati ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia, kilimo na ufugaji wa kuhamahama’’ alisema Dkt. Kazungu.

Dkt. Kazungu aliongeza kuwa ‘’ inakadiriwa kuwa ili kurejesha eneo la misitu linalopotea kila mwaka inahitajika kupanda na kutunza miti katika eneo lenye ukubwa wa hekta 185,000 sawa na miti 2,280,000 kwa mwaka kwa muda wa miaka 17 mfululizo’’

Aidha, Dkt. Kazungu amesema Serikali imeandaa Mkakati wa Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uhifadhi wa Mazingira kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi 2032.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Jaji mstaafu Mhe. Mathew Maimu amesema utekelezaji wa haki za  binadamu ni muhimu kwa mazingira salama ili kuwezesha jamii kuishi mahali pa utulivu na usalama na kuwezesha kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa maendeleo ya nchi.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Jabir Shekimweri ameipongeza Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa zoezi la upandaji miti na kuwasihi kuwa katika maadhimisho hayo ya kutimiza miaka 20 wajitahidi kutatua changamoto  za wananchi wa Dodoma hasa kwenye sekta ya ardhi na mirathi.

Katika zoezi hilo la upandaji miti Miche 600 ya matunda na kivuli imepandwa katika eneo la ekari mbili.

Kauli mbiu ya Maadhimisho hayo ni ‘’Miaka 20 ya Kuhamasisha Ulinzi na Hifadhi ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa Maendeleo ya Nchi’’.


Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YAIPONGEZA WIZARA KWA UTEKELEZAJI WA MAMA SAMIA LEGAL AID CAMPAIGN

TUFANYE KAZI KWA UADILIFU NA USHIRIKIANO - MHE CHANA