RAIS SAMIA ATAKA SHERIA YA KULINDA UWEKEZAJI IANGALIWE UPYA


 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza wakati akizindua Chama cha Mawakili wa Serikali tarehe 29 Septemba, 2022 jijini Dodoma.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiteta na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro kabla ya kuzindua Chama cha Mawakili wa Serikali tarehe 29 Septemba, 2022 jijini Dodoma.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizindua Mfumo wa Usajili wa Mawakili wa Serikali tarehe 29 Septemba, 2022 jijini Dodoma.


Sehemu ya Mawakili wa Serikali wakimsikiliza Rais.

XXXXXXXXXXXXXXXXXX

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ameagiza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuangalia upya sheria ya Uwekezaji nchini ili kuepuka migongano na migogoro kati ya nchi na Wawekezaji.

 

Rais Samia ameyasema hayo wakati akizindua Chama cha Mawakili wa Serikali katika viwanja vya Jakaya Kikwete Convention Centre leo tarehe 29 Septemba, 2022, ambapo yeye alikuwa Mgeni Rasmi.

 

Rais Samia amesema “Tumefungua nchi kwa kiasi kikubwa, wawekezaji wanakuja ili tuendelee na uwekezaji mkubwa na mzuri, Mawakili wa Serikali mjipange kutatua migogoro ya kibiashara kwa haraka kabla ya kufika mahakamani”.

 

Aliongeza, “Tukilinda uwekezaji tutatengeneza wigo mpana wa ukusanyaji mapato na kukuza uchumi utakaosaidia kuinua maslahi ya nchi”.

 

Vilevile, Rais Samia amewataka Mawakili wa Serikali kuwa waadilifu  na waaminifu wanapotenda kazi zao ili kuwezesha wananchi kupata haki wanazostahili.

 

Rais Samia amesema “ Mnapoaminiwa kusimamia sekta hii ya haki nendeni mkafanye uadilifu ili wananchi waweze kupata haki”

 

Aliongeza kuwa kumekuwa na malalamiko ya mlundikano wa mahabusu magerezani lakini Mawakili wakisimama kwenye haki na kusikiliza wananchi nje ya Mahakama, mlundikano huo utapungua kwani wasio na hatia wataachiwa huru

 

Alisema “Nawapongeza mlivyoanza kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya Habari, nawasihi Mawakili wa Serikali kushiriki kutoa elimu kwa umma hususan sheria zinazowagusa wananchi , na taratibu za namna ya kupata haki zao, lengo ni kupunguza mashauri ambayo hayana ulazima wa kwenda mahakamani”.

 

Mhe. Rais aliongeza “Suala la kusimamia haki lipo mikononi kwenu, ninyi ni mainjinia wa kucheza na vifungu vya sheria mna uwezo wa kumtoa mwenye kosa na kumhukumu asiye na kosa, fanyeni injinia ya sheria inayosimamia haki”

 

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro, akimkaribisha Mgeni Rasmi amesema sekta ya sheria ni muhimu katika utawala bora.

 

Dkt. Ndumbaro alisema Mkutano huo utakwenda kuleta tija kwa Mawakili ambao ndio watekelezaji wa majukumu mbalimbali kuhusiana na masuala ya kisheria na utoaji haki nchini.

 

Naye Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Prof. Hamis Juma aliwaasa Mawakili wa Serikali kutimiza malengo ya sheria kwani haina maana kuwa na sheria ambazo hazitimizwi.

 

Aliongeza kuwa “Tukubali kuwa zipo sheria ambazo ni vikwazo kwa maendeleo, jukwaa lenu ni muhimu katika kufanya sheria zetu ziende na wakati”

 

Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Eliezer Feleshi amesema kazi na wajibu wa Wanasheria ni kuwawezesha Rais, Spika na Jaji Mkuu kutekeleza majukumu yao.

 

Aliongeza zipo chanagamoto kwa baadhi ya Watendaji wa Serikali kutofuata sheria na kusababisha Serikali kupata kesi na hapo ndipo Mawakili wa Serikali wanaposhirikishwa kushughulikia kesi hizo.

 

Jaji Feleshi amesema “ Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia daftari la usajili atahakikisha anapata wanasheria bora ili kuongeza ufanisi.

 

Mkutano huo wa Mawakili wa Serikali wa mwaka 2022 umebeba kauli mbiu isemayo *“Utekelezaji wa majukumu ya Serikali kwa kuzingatia haki ni nyenzo muhimu kwa maendeleo ya Taifa”


Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YAIPONGEZA WIZARA KWA UTEKELEZAJI WA MAMA SAMIA LEGAL AID CAMPAIGN

TUFANYE KAZI KWA UADILIFU NA USHIRIKIANO - MHE CHANA