SERIKALI KUENDELEA KUTEKELEZA WAJIBU WA KULINDA HAKI ZA BINADAMU NA WATU – WAZIRI NDUMBARO

                                    Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akizungumza                                     kwenye kilele cha Maadhimisho ya Miaka 20 tangu kuanzishwa kwa                                        Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
 
                                          Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary                                                                               Makondo  akizungumza kwenye kilele cha Maadhimisho ya Miaka 20                                        tangu kuanzishwa kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

                                        Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akipokea Tuzo                                     kwa niaba ya Rais Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.                                         Samia Suluhu Hassan.

XXXXXXXXXXXXXXX

Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema Serikali imeendelea kutekeleza wajibu wa kulinda haki za binadamu na watu kwa kutekeleza Sheria, Sera, Mipango, Mikakati na programu zinazotafsiri upatikanaji wa haki mbalimbali.

Dkt. Ndumbaro ameyasema hayo wakati wa kilele cha Maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora leo Septemba 15, 2022 katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma.

‘’Serikali imeendelea kutekeleza wajibu wa kulinda haki za binadamu na watu kwa kutekeleza Sheria, Sera, Mipango, Mikakati na programu zinazotafsiri upatikanaji wa haki mbalimbali kama vile haki ya afya na mazingira bora; haki ya kupata elimu; haki ya maendeleo na haki ya kumiliki mali’’ amesema Dkt. Ndumbaro.

Dkt. Ndumbaro aliongeza ‘’kuhusu haki afya Takwimu zinaonesha kuwa idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya vilivyosajiliwa imekuwa ikiongezeka. Katika kipindi cha Julai 2021 hadi Machi, 2022, vituo hivyo vimeongezeka kufikia 8,549 ikilinganishwa na vituo 8,458 mwaka 2020’’.

Pia kwa upande wa haki za kiuchumi Dkt. Ndumbaro amesema Serikali inatekeleza vipaumbele vya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026). Vipaumbele hivyo vinajumuisha kuchochea uchumi shindani na shirikishi, kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma, kukuza biashara na uwekezaji, kuchochea maendeleo ya watu na kuendeleza rasilimali watu. Mpango Kazi huu unatambua  haki za binadamu kama msingi wa kuleta maendeleo ya kudumu.

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary Mkondo amesema uwepo wa Tume hii ni ishara kuwa Serikali imeweka umuhimu katika masuala ya Utawala Bora katika ngazi zote za uongozi wa Taifa letu kama changamoto za utawala bora zikitatuliwa matatizo mengi kama vile rushwa, utawala wenye upendeleo na unyanyasaji wa wafanyakazi yatapungua na hatimae kuisha.

Bi. Makondo aliongeza ‘’utayari wa Serikali kuwa na chombo kama hiki kinachopima  na kuishauri Serikali kwenye utendaji kazi wake wa kulinda na kukuza haki za binadamu ni ushahidi kuwa Tanzania ni  nchi inayothamini demokrasia kuwa ina Serikali ambayo iko tayari kuwajibika kwa chombo kama hiki chenye sifa ya uchunguzi’’

Vilevile, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Mstaafu Mhe. Mathew Maimu wakati akimkaribisha Dkt. Ndumbaro ambaye ndiye mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho hayo amesema katika kipindi cha Serikali ya awamu ya sita hali ya Haki za Binadamu imeimarika na Tume imetekeleza majukumu yake kwa uhuru.

Aidha, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imempatia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan Tuzo kwa kutambua mchango wake katika kutetea na kuimarisha Haki za Binadamu na misingi ya Utawala Bora. Tuzo hiyo imepokelewa na Waziri Ndumbaro kwa niaba ya Rais.

 

 


Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YAIPONGEZA WIZARA KWA UTEKELEZAJI WA MAMA SAMIA LEGAL AID CAMPAIGN

TUFANYE KAZI KWA UADILIFU NA USHIRIKIANO - MHE CHANA