DKT. KAZUNGU AAHIDI USHIRIKIANO NA WADAU KUTOKOMEZA UKATILI DHIDI YA WATOTO


 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Khatibu Kazunguakisoma hotuba yake wakati akifunga kikao kazi cha Haki Mtoto cha siku mbili cha Wadau wa Jukwaa la Haki Mtoto kilichofanyika kuanzia tarehe 20 hadi 21 Oktoba, 2022 jijini Arusha


Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Felistas Mushi akimkaribisha mgeni rasmi kufunga kikao kazi cha Haki Mtoto cha siku mbili cha Wadau wa Jukwaa la Haki Mtoto kilichofanyika kuanzia tarehe 20 hadi 21 Oktoba, 2022 jijini Arusha.


Washiriki wa kikao kazi wakimsikiliza mgeni rasmi.


Picha ya pamoja.

XXXXXXXXXXXX

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Dkt. Khatibu Kazungu ameahidi Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria kushirikiana na Wadau ili kushughulikia ulinzi na haki ya mtoto.

Dkt. Kazungu ameyasema hayo wakati akifunga kikao kazi cha Haki Mtoto cha siku mbili cha Wadau wa Jukwaa la Haki Mtoto kilichofanyika kuanzia tarehe 20 hadi 21 Oktoba, 2022 jijini Arusha.

Dkt. Kazungu amesema “Wizara yangu pamoja na kutekeleza yale yaliyo ndani ya mamlaka yake, inapenda kuwaahidi kuwa, tutaendelea kushirikiana na ninyi wadau wetu muhimu na tutawakutanisha kila uhitaji unapotokea ili kwa pamoja tuweze kushughulikia masuala muhimu ya ulinzi na haki ya mtoto”.

Aliongeza kuwa “Tunafahamu kwamba; masuala ya haki mtoto ni mtambuka, hivyo ninawaomba tujikite zaidi katika kuzuia;  na ikitokea matukio yameshatokea basi tufuate utaratibu mzuri wa kisheria katika kushughulikia masuala haya. Haki Mtoto imlinde zaidi mtoto aliye katika ukinzani na hata yule asiye katika ukinzani na sheria”.

Katika kikao hicho yapo mambo mengi yameibuliwa na kuleta mjadala miongoni mwao.  Baadhi ya mambo hayo yapo ya kisera, kisheria na mengine ya kiutendaji. Ikiwemo ufinyu wa bajeti, upatikanaji wa taarifa na takwimu sahihi za ukatili dhidi ya watoto, sheria ya mtoto katika uwezekano wa kubadili au kuboresha baadhi ya maeneo ya sheria hiyo.

Aidha, Naibu Katibu Mkuu huyo amewasihi kuwa, Jukwaa hilo liwe chachu ya mabadiliko chanya, na yale wanayoyajadili na kupendekeza yazingatie matakwa ya Katiba na sheria nyingine za nchi na yasirudishe nyuma jitihada za kumlinda mtoto, awe wa kike au kiume.

Naye Mwakilishi wa UNICEF Bi. Victoria Mponela amesema changamoto kubwa ya utekelezaji wa masuala yanayokubaliwa na Jukwaa la Haki Mtoto utekelezwaji wake unakwamishwa na ufinyu wa bajeti hivyo akaisihi Serikali iingize kazi zilizopo kwenye Mpango Mkakati ziingizwe kwenye bajeti za ndani ili malengo yafikiwe.

Awali akimkaribisha Mgeni rasmi Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Msaada wa Kisheria Bi. Felistas Mushi amesema majadiliano katika kikao hicho cha siku mbili yamekuwa yenye tija na Wadau wanajitahidi kufanya kazi katika maeneo yao kwa bajeti hafifu ili mradi kulinda haki ya mtoto.

Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YAIPONGEZA WIZARA KWA UTEKELEZAJI WA MAMA SAMIA LEGAL AID CAMPAIGN

TUFANYE KAZI KWA UADILIFU NA USHIRIKIANO - MHE CHANA