DKT. MWAKYEMBE KUONGOZA KAMATI YA WATU SABA KUCHUNGUZA MATOKEO LAW SCHOOL


 
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro akiongea na waandishi wa habari.

XXXXXXXXXXXXXXXX

Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imeunda Kamati ya watu saba kuchunguza na kushughulikia malalamiko ya matokeo ya wanafunzi wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro wakati akiongea na Vyombo vya Habari katika ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO Jijini Dodoma  tarehe 12 Oktoba, 2022.

Dkt. Ndumbaro amesema Serikali ya Awamu ya Sita inaposikia malalamiko inachukua hatua na hivyo imeamua kuunda kamati itakayotoa majibu ya malalamiko ya wanafunzi wa Chuo hicho.

Dkt. Ndumbaro amesema "Sisi kama Serikali ya Awamu ya Sita tunaposikia malalamiko tunachukua hatua, ili kama kuna tatizo lazima tulijue."

Dkt. Ndumbaro aliongeza "Serikali imeamua kuunda Kamati ya watu saba ambayo imepewa siku 30 kuanzia Oktoba 13, 2022 ili kutuambia tatizo liko wapi."

Dkt. Ndumbaro alisisitiza "Katika Kamati hii hakuna Mwalimu wala Mtumishi wa Law School wala Vyuo vya Sheria."

Wajumbe wengine katika Kamati hiyo ni Jaji Mstaafu Silius Matupa, Bw. Rashid Asah, Bi. Gloria Kalabamu, Bi. Alice Edward, Bi. Mary Mniwasa na Bw. John Kaombwe ambao wametoka katika Taasisi mbalimbali.

Awali akielezea ufaulu wa wanafunzi katika Taasisi hiyo, Dkt. Ndumbaro amesema asilimia 81 ya wanafunzi wamefaulu ambapo miongoni mwao kuna baadhi watarudia mitihani ya baadhi ya masomo na wanategemewa kufaulu. Asilimia 19 ndio waliofeli kabisa.

Uamuzi huu wa Serikali kuunda kamati hii umetokana na malalamiko kutoka makundi mbalimbali katika jamii ikiwemo wanafunzi, walezi, Mawakili wa kujitegemea, Waajiri, Umma wa Watanzania, Wanahabari, Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria Kwa Vitendo na Wanazuoni kutoka Vyuo vya Sheria.

Taasisi hiyo ina jumla ya Walimu 95 ambao miongoni mwao kuna Majaji, Mahakimu na Mawakili waliobobea hivyo Serikali haina shaka na ubora na idadi ya walimu waliopo.

 


Comments

Popular posts from this blog

KAMATI YAIPONGEZA WIZARA KWA UTEKELEZAJI WA MAMA SAMIA LEGAL AID CAMPAIGN

TUFANYE KAZI KWA UADILIFU NA USHIRIKIANO - MHE CHANA