IDARA NA SEKTA ZINAZOHUSIKA NA UTAJIRI ASILI NA MALIASILIA ZIFANYE KAZI KWA PAMOJA: BI. MAKONDO
Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Mary Makondo amezitaka Idara na Sekta za Serikali zinazohusika na usimamizi wa Utajiri Asili na Maliasilia za Nchi kufanya kazi kwa pamoja kuhakikisha wananchi wananufaika na utajiri asilia na maliasilia za nchi.
Bi. Makondo ameyasema hayo wakati akifungua
kikao kazi cha kujadili utekelezaji wa Mpango wa Kusimamia Utajiri Asili na
Maliasilia za Nchi (Natural Wealth and Resources Socio-Economic Governance
Programme) leo tarehe 6 Oktoba, 2022 Jijini Arusha.
“Najua mnawakilisha ofisi zenu, mnawakilisha
Wizara zenu lakini tukumbuke tu wamoja, tunajenga Tanzania moja hivyo tufanye
kazi kwa pamoja kuhakikisha mpango huu haupunguzi tu umaskini kwa
Watanzania bali pia unaongeza Pato la Taifa.” Alisema Bi Makondo.
Mradi huo unatekelezwa na Wizara ya Katiba na
Sheria kwa ufadhili wa Serikali na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa
(UNDP).
Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Katibu Mkuu
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Zainabu
Chaula, Wadau kutoka Sekta na Idara za Serikali zinazoshughulika na
Utajiri Asili na Maliasilia za Nchi pamoja na baadhi ya Wabia wa Maendeleo
kutoka UNDP.
Akitoa salaam zake, Dkt. Chaula amekumbusha
washiriki kwamba wana jukumu la kumsaidia Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupunguza changamoto za Watanzania hivyo
anayo matumaini makubwa kwamba mradi utafika mwisho na kutimiza malengo yake
mazuri ya kutatua changamoto za wananchi.
Naye ndugu Amon Manyama kutoka UNDP amesema
mradi huo ni mzuri unategemewa kunufaisha Watanzania kiuchumi, amesisitiza
ushirikishwaji wa wanawake, vijana na jamii ya chini kabisa ambako ndiko kuliko
na wananchi wengi.
Comments
Post a Comment